WAZIRI WA NISHATI NA MADINI WILLIAM NGELEJA AKUTANA NA KAMPUNI YA KUTENGENEZA MITAMBO YA KUFUA UMEME JIJINI DAR ES SALAAM - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI WILLIAM NGELEJA AKUTANA NA KAMPUNI YA KUTENGENEZA MITAMBO YA KUFUA UMEME JIJINI DAR ES SALAAM


Waziri wa Nishati na Madini alipokutana na Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya General Electric ya nchini Marekani kuzungumzia fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati nchini.
--
Na.Mwandishi wetu.
Kampuni ya General Electric (GE) ya nchini Marekani imekutana na Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es salaam jana kwa lengo la kujitambulisha na kuzungumzia fursa ambazo kampuni hiyo inaweza kuwekeza katika sekta ya nishati nchini.
Makamu Mwenyekiti wa kampuni hiyo , John Rice alisema kuwa kampuni hiyo ya GE inajishughulisha na utengenezaji wa mitambo ya kufua umeme. Alifafanua kuwa mitambo inayotengenezwa na kampuni hiyo ni ile ya kutumia mafuta ya taa, dizeli, gesi asili, upepo, jua na joto ardhi (geothermal) kwa ajili ya kufua umeme.

Aidha, alisema kampuni hiyo inajishughulisha  katika uwekezaji wa miundombinu ya kusafisha na kusafirisha gesi na akabainisha kuwa wako tayari kuanza kufanya kazi hiyo mara moja endapo watafanya mazungumzo na Serikali ama kupitia Shirika la Ugavi wa Umeme  Tanzania (TANESCO) na kukubaliana kama kutakuwa na mahitaji ya mitambo ya aina hiyo.
“Sisi tupo tayari kuja kuwekeza Tanzania kwani tuna uzoefu wa kutosha na tumewekeza katika nchi mbalimbali ulimwenguni na kwa hivi sasa tunatarajia kuwekeza nchini Kenya ambapo tayari mazungumzo yameanza na serikali ya nchi hiyo” aliongeza.

Kampuni Rice aliongeza kuwa kwa kawaida kampuni ya GE hufanya mpango wa kufadhili miradi ili kufanikisha uwekezaji, alisema “sisi tupo tayari kushirikiana na serikali kwaajili ya kutafuta wafadhili wa miradi mbalimbali ya nishati, hivyo tukikubaliana tu tunaanza mchakato wa kutafuta ufadhili”
Naye Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alifurahishwa sana na ujio wa wawakilishi wa kampuni hiyo na kusema kuwa kampuni hiyo imekuja wakati muafaka. “Tunawakaribisha kwa dhati kabisa ili muwe sehemu ya wawekezaji” alisema.

Waziri Ngeleja alisema kuwa serikali inafuraha sana kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na watengenezaji wa mitambo ya kufua umeme badala ya kupitia kwa wakala kama ilivyo kwa hivi sasa.

Aliongeza kuwa “hii itasaidia sana katika kupunguza gharama za ununuzi wa mitambo hiyo na kwa wakati huohuo itasaidia kupunguza mlolongo hivyo mitambo itakuwa inafika kwa wakati muafaka pale tunapohitaji kwa kupitia Tanesco”

Wakati huohuo waziri Ngeleja aliwaelekeza Tanesco kuchangamkia fursa hii kwa kuanza mawasiliano na kampuni hiyo moja kwa moja na hasa kuhusu kupata mitambo ya kuzalisha umeme ama kwa kununua au kwa kukodi mitambo hiyo kwa kadri wao Tanesco watavyoona inafaa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini  (TANESCO), William Mhando alimuhakikishia waziri Ngeleja kuwa shirika litafanya mawasiliano zaidi na kampuni hiyo ili kuwa na mpangilio madhubuti zaidi.

Waziri Ngeleja alimalizia kwa kuishauri Kampuni ya GE kuendelea kufanya mawasiliano na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ili kuangalia namna mashirika hayo yanavyoweza kukubalian na kampuni hiyo ili kuwekeza nchini.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages