MAHAKAMA ya hakimu makazi mkoa wa Iringa kwa mara ya pili imemwachia huru aliyekuwa mshindi wa kura za maoni ndani ya chama cha mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 Frederick Mwakalebela na mkewe Celina baada ya kuonekana hawana kesi ya kujibu katika shitaka lililofunguliwa na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Iringa.
Mwakalebela na mkewe walifikishwa kwa mara ya pili mahakamani hapo na Takukuru baada ya kushinda kesi hiyo kwa mara ya kwanza miezi miwili iliyopita kabla ya Takukuru mkoa wa Iringa kuifungua upya kesi hiyo ya kuwakamata kwa mara ya pili watuhumiwa hao.
Hakimu wa mahakama hiyo Mary Senapee alisema kuwa mahakama hiyo inawaachia huru watuhumiwa hao kutokana na kutokuwa na kesi ya kujibu katika shitaka hilo la rushwa lililofunguliwa na Takukuru na kuitaka Takukuru kama haijaridhika kukata rufaa. Mwakalebela na mkewe walifikishwa mahakamani hapo na Takukuru kwa kosa la kutoa rushwa ya shilingi 100,000 kinyume na sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kifungu cha 15(1)(b) kinachokwenda sambamba na sheria ya gharama za uchaguzi namba 6 ya mwaka mwaka 2010 kifungu namba 21 (1) (a) na kifungu cha 24(8). Takukuru kupitia mwendesha mashtaka wake Imani Mizizi ilidai kuwa Juni 20, mwaka jana mshitakiwa Mwakalebela alidaiwa kutoa hongo ya sh. 100,000 kwa mwenyekiti wa kijiji cha Mkoga ,Hamis Luhanga ili awagawie wajumbe wa CCM 30 ambao waliitwa kwenye kikao hicho cha kujipanga kushinda kura za maoni CCM huku akitambua wazi kufanya hivyo ni kosa .
Hata hivyo kesi hiyo ambayo ilionyesha kuwa na mvuto zaidi kwa wakazi wa mkoa wa Iringa ambao walifika mahakamani hapo kutaka kujua hatma ya kesi hiyo ,imekuwa ni kesi ya aina yake na kupelelea ndugu kutoka kwa shangwe zaidi katika mahakama hiyo kutokana na TAKUKURU kuendelea kubwagwa mahakamani .
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia ndugu na marafiki wa karibu wa Mwakalebela wakiondoka mahakamani hapo kwa furaha kubwa huku wakimpongeza Mwakalebela na mkewe kwa kushinda katika kesi hiyo tena. Katika kesi hiyo Mwakalebela na mkewe Celina walikuwa wakitetewa na wakili wa Basil Mkwata ambaye aliwasilisha pingimizi la awali la kisheria ukiomba kesi hiyo iondolewe mahakamani kutokana na mapungufu ya kisheria yaliofanywa na upande wa mashitaka kabla ya Takukuru kuendelea kung’ang’ania kuendelea na kesi hiyo. (Imeandikwa na Francis Godwin-Iringa) |
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)