JK NA UMANGIMEZA, TAFSIRI YANGU - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

JK NA UMANGIMEZA, TAFSIRI YANGU

 
Ndio, usiku huu nimemsikiliza Jakaya Kikwete kupitia runinga ya TBC1. Kikwete ameongea na watendaji wakuu serikalini kule Dodoma. Na walikuwa wengi ukumbini; Mawaziri , Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu na wengine.

Tafsiri yangu; kwanza kabisa, nimeipenda sana hotuba ya Kikwete ingawa TBC1 hawakuweza kuimalizia kutokana na matatizo ya kiufundi. Nitaitafuta niisome kwa ujumla wake.
Vinginevyo, katika kile nilichokisia nilimwona Rais aliyekuwa critical kweli kweli kwa watendaji wake.

Naam. Rais ‘ aliwasema’ kweli watendaji wake, kama nitatumia lugha ya sebule zetu. Kikwete niliyemwona, pasi na shaka, alikuwa mkweli kwa nafsi yake. Alitoa duku duku lake. Watendaji wale walionekana kuwa kimya wakati wote. Kuna ambao waliinamisha vichwa. Hotuba ya Kikwete ilikuwa na ukweli mwingi juu ya hali halisi. Kikwete alikuwa anaongelea sehemu ya kero ya wananchi kwa watendaji wao. Mle ukumbini kuna watakaotoka wakinung’unika; “ Bwana Mkubwa katuumbua!” Watajisemea.

“ Kazi ya Waziri si kusoma mafaili tu” Anasema Kikwete. Kisha anaongeza; Tokeni!” Na hilo ndilo neno lililosikika mara kwa mara kwenye hotuba ile. Kikwete alilisitiza sana umuhimu wa watendaji kutoka na kwenda kwa wananchi.

“ Ni nani kati yenu kazi yake iko ofisini tu?” Aliuliza Mkuu wa Nchi. Kama ilivyotarajiwa, hakuna aliyenyosha kidole.

Na naweza kubashiri, kuwa kuna gazeti litakalotoka kesho na kichwa cha habari; ” JK Awaanika Watendaji Wake”. Kikwete anasema; ” Tubadilike jamani”. Lakini, nilichokiona kwenye sura za wengi wa watendaji wale ni ugumu uliopo wa kubadilika. Inahusu ’ Change of Mindset” na bila shaka JK mwenyewe analijua hilo. Swali ni hili; “ How can you change from a fixed mindset to a growth one?” Mbwa mzee hafundishwi kukaa, au? Inawezekana kama mbwa mwenyewe akiwa na utayari wa kijifunza. Ndio inawezekana.

Watendaji wale baadhi yao wanasumbuliwa na maradhi ya kuendekeza ‘ Ubwana na Umangimeza” . Si ndio, wanapenda sana ‘ Ubosi’. Na ndio maana itawawia ugumu kweli Waheshimiwa hao kukaa chumba kimoja na vijana Maafisa Habari wao. Si vijana wadogo tu, tena wamemaliza vyuo vikuu juzi tu. Eti bosi mzima a-brief kijana Afisa Habari juu ya habari za Wizara kasha kijana huyo azungumze na umma. Urgently needed, change of mindset! Vinginevyo tutabaki pale pale na kauli za; “ Mimi si msemaji wa Wizara!”

Lakini, tutakosea pia tukidhani kuwa baadhi ya watendaji wale wako busy tu maofisini wakisoma mafaili, maana kuna ukweli mwingine, ni huu; baadhi ya watendaji wetu wako busy sana kufanya mambo yao binafsi, ndani na nje ya ofisi. Si tunajua, kuwa baadhi ya watendaji wetu ni wafanyabiashara na wengine wanaendesha hata viwanda vya uzalishaji.

Katika utaratibu wa sasa na hasa baada ya kuondokana na kanuni na maadili ya uongozi ya enzi za Mwalimu, ni vigumu ukawa na mawaziri na watendaji wengine wasio na miradi ya biashara, mashamba na hata viwanda ambayo wao wenyewe ndo wasimamiaji. Hivi, Waheshimiwa hawa watapata wapi muda wa kusimamia biashara, mashamba na viwanda vyao kama si kuiba muda wa kuwatumikia wananchi na hata kutumia rasilimali za umma?

Inahusu swali hili; Ni nani atauzima mshumaa wa Serikali? Na hapa kuna kisa cha kusimulia;
Naam, miongoni mwa viongozi waliopata kuongoza dola ya Kiislam hususan baada ya Mtume Muhammad (SAW) na baada ya masahaba ni Amir muuminina Khalifa Umar bin Abdulaziz. Wanazuoni wa Kiislam wanatwambia, kuwa utawala wa Khalifa Umar bin Abdulaziz ulijaa uadilifu. Si kwa viongozi tu, hata kwa raia wake.

Inasemwa, kuwa moja ya mafanikio makubwa ya utawala wa Khalifa Umar bin Abdulaziz ni kukusanya zakka. Katika Uislam, zakka ni ibada ya lazima kwa mwenye nacho kuwapa masikini, yatima, wajane, wasafiri, raia na wengineo wenye kuhitaji.

Watu walijengewa imani kubwa, kiasi hakuna aliyethubutu kukwepa kutoa zakka. Hata wale waliopokea zakka walikuwa waadilifu, hawakupokea zakka mara mbili kama walishapokea kabla. Wote waliostahili kupata zakka , walipata zakka. Hakika, zakka zilitolewa zikajaa mabohari.

Siku moja raia mmoja alikwenda kwenye ofisi ya Khalifa Umar bin Abdulaziz. Wakati wa maongezi yao, Khalifa Umar alikuwa akihangaika kuupuliza na kuuzima mshumaa mmoja na kuwasha mwingine. Alikuwa na mishumaa miwili mezani. Kadri mazungumzo yalivyoendelea, Umar aliendelea kufanya hivyo. Alipuliza mshumaa mmoja ukazimika, kisha akawasha mwingine.

Jambo hilo lilimstaajabisha sana mgeni wa Khalifa Umar bin Abdulaziz. Akauliza; "Je, ni kwa nini unazima mshumaa huu na kuwasha mwingine, kisha huo nao unauzima na kuwasha ule wa kwanza?
Khalifa Umar bin Abdulaziz akamjibu; "Mshumaa huu ni wa Serikali, wewe unaponiuliza habari za Serikali nauwasha. Lakini naona mara unauliza habari za familia yangu, ndio maana nauzima wa Serikali na nauwasha mshumaa wangu mwingine nilioununua kwa pesa za mfukoni mwangu. Nachelea nisije fanya dhuluma kwa mali ya nchi."

Ndugu zangu, bila shaka, hicho ni kisa chenye kutupa mafundisho muhimu juu ya dhana nzima ya Maadili katika Utumishi wa Umma. Tafakari.

Maggid
Iringa
Jumatatu Mei  9, 2011
http://mjengwa.blogspot.com

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages