RAISI KIKWETE AFANYA MAZUMGUMZO NA VIONGOZI WA VYAMA VYA WAFANYAKAZI NCHINI - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

RAISI KIKWETE AFANYA MAZUMGUMZO NA VIONGOZI WA VYAMA VYA WAFANYAKAZI NCHINI


  Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akikutana na viongozi wa vyama huru vya wafanyakazi ikulu jijini Dar es Salaam leo mchana kuzungumzia jinsi ya kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi nchini.Katika mkutano huo Mawaziri wa Kazi na ajira Gaudensia Kabaka, Tamisemi George Mkuchika, pamoja na watendaji wakuu kutoka Hazina walihudhuria.
 Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwaongoza viongozi wa vyama huru vya wafanyakazi nchini kusimama kwa muda kumkumbuka aliyekuwa katibu mkuu wa TRAWU marehemu Sylivester Rwegasira aliyefariki hivi karibuni, wakati Rais Kikwete alipokutana na viongozi hao ikulu jijini Dar es Salaam leo mchana kuzungumzia jinsi ya kutatua changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi nchini.Picha na Freddy Maro-IKULU
 ---
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Aprili 20, 2011, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini.

Mkutano huo wa kawaida kati ya Rais Kikwete na vikundi mbalimbali vya jamii kikiwemo kile cha viongozi wa wafanyakazi umefanyika Ikulu, Dar es Salaam katika mazingira ya kuelewana.


Mkutano huo umechukua kiasi cha saa tano na kuhudhuriwa na viongozi 20 wa wafanyakazi, mawaziri wanaohusika na masuala na haki za wafanyakazi na watumishi wengine waandamizi wa Serikali.


Viongozi wao wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Bwana Ayoub Omar Jumaa umeshirikisha viongozi kutoka TUCTA yenyewe, Chama cha Walimu Tanzania (CWT), TPWU, TEWUTA, DOWUTA, TRAWU, CHODAWU, TUICO, TASU, TAMICO TUGHE na COTWU.


Mawaziri waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Waziri wa Kazi na Ajira, Mheshimiwa Gaudencia M. Kabaka, Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi Umma, Mheshimiwa Hawa A. Ghasia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Mheshimiwa George Huruma Mkuchika.


Katika kikao hicho, pande hizo mbili zimejadili masuala mengi yanayohusu haki na maslahi ya wafanyakazi na masuala mengine muhimu ya taifa yakiwamo madai ya malimbikizo ya malipo ya wafanyakazi ikiwamo mishahara.


Rais Kikwete na viongozi hao pia wamejadili kuhusu uwezekano wa Serikali kuongeza mishahara ya watumishi kwa kuzingatia upandaji wa gharama za maisha, uwakilishi wa wafanyakazi katika mchakato wa kuandaa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na uwezekano wa Serikali kupunguza kodi kwa wananchi ili kutoa ahueni zaidi ya maisha kwa wananchi.


Kuhusu sera ya Serikali ya kupunguza kodi ili kutoa ahueni ya maisha kwa wananchi, Rais Kikwete amewaambia viongozi hao wafanyakazi: “Hili tulikwishakubaliana kuwa lazima tuchukue hatua za mara kwa mara kuongeza unafuu wa maisha kwa wananchi wetu. Tutaendelea nalo hili kwa sababu ni muhimu sana. Suala kubwa hapa ni kutekeleza sera ya kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi. Lazima tufanye kila liwezekanalo kufanikisha hili.”


Kuhusu ombi la viongozi hao kuwa Serikali itoe dhamana kwa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) ili kuliwezesha shirika kuwa na uwezo wa kukopa fedha katika mabenki kusaidia kuliimarisha, Rais Kikwete ameigiza Wizara ya Fedha kuchukua hatua za haraka kuhakikisha hili linafanikiwa. “Tulifanye hili haraka sana, halina sababu ya kucheleweshwa kwa sababu TTCL ni shirika muhimu sana.”


Mwisho.


Imetolewa na:


Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,


Ikulu,


DAR ES SALAAM.


20 Aprili, 2011

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages