MUSWADA HUU WA KATIBA YA NCHI TUSIPOANGALIA UTALETA VURUGU, UVUNJIFU WA AMANI - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MUSWADA HUU WA KATIBA YA NCHI TUSIPOANGALIA UTALETA VURUGU, UVUNJIFU WA AMANI

TUMSHUKURU Mungu wetu aliyetuumba kutokana na kutuweka hai, hakika ametupendelea na bado anatulinda.

Baada ya kusema hayo naona ni vyema nianze moja kwa moja na mada ya leo ambayo inahusu Muswada wa Marekebisho ya Katiba  ya Tanzania, mjadala ambao umeanza kuvuruga umoja wa kitaifa na kutugawa kwenye makundi.

Ndugu zangu, hakika hili la katiba ni jambo zito. Tumeshuhudia tangu muswada huo uanze kujadiliwa na wadau mbalimbali siku kadhaa zilizopita, mambo yanayojitokeza. Watanzania wengi, pasipo kujali tofauti ya itikadi na imani zao, wameghadhabishwa na muswada huo kutokana na ukweli kwamba, unabeba maudhui yenye lengo la kukidhi matakwa na maslahi ya wachache katika nchi yetu. 

Hakika kuna mayowe yanapigwa kutoka kwa wananchi karibu  kila kona ya nchi yetu kuupinga muswada huo. Wengi wanasema kuna kundi la vigogo wenye uroho wa madaraka halitaki kukosolewa na hivyo kuweka pamba masikioni. Kundi hilo linasema wananchi watake wasitake, muswada huo ndiyo pekee utakaokuwa msingi wa mchakato utakaozaa katiba mpya ya nchi. Rais amefanywa kuwa ndiye mwamuzi wa mwisho.

Yapo manung’uniko kuwa, wananchi hawakushirikishwa katika mchakato wa kuandaa muswada huo, kwa maana ya kutoa mawazo yao ili yazingatiwe katika kuutayarisha. Kwa mfano huko Zanzibar, tulisikia mijadala ya muswada huo ilivyojaa vitimbi, ghadhabu na jazba kwa kiwango cha kutisha.

Baadhi ya wananchi walidiriki kuchanachana na wengine kuchoma moto nakala za muswada huo mbele ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi na ya Muungano, akiwemo Waziri wa Afrika Mashariki, Samweli Sitta.

Baada ya matukio hayo, nashangazwa kuona viongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar wamekaa  kimya kana kwamba hakuna kilichotokea. Tafadhalini viongozi wa pande zote za muungano lioneni hili, kuna hatari kubwa baadaye ikiwa malalamiko ya wananchi hayatapatiwa ufumbuzi.

Nasema hivyo kwa sababu katika mijadala hiyo tumeshuhudia Wazanzibari wengine wakienda mbele zaidi kwa kusema kuwa hawautaki muungano, kwa maelezo kuwa Zanzibar inaendelea kuburuzwa na kwamba mustakabali wa nchi yao bado unaamuliwa kutoka Tanzania Bara. Hii ni dhana ambayo ipo miongoni mwa Wazanzibari wengi kwa siku nyingi sasa.

Haya ni madai ya msingi ambayo lazima yafanyiwe kazi iwapo tunataka muungano uendelee kustawi na kuwepo kwa utashi wa wananchi wa pande zote mbili. 

Ndugu zangu, madai hayo mazito yamepewa nguvu zaidi kutokana na kauli ya hivi karibuni ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ). Mwanasheria huyo alieleza kuwa, serikali hiyo ilipeleka mapendekezo 14 katika Serikali ya Muungano kuhusu muswada huo wa katiba mpya lakini ni mawili tu yaliyokubaliwa. Hakuna sababu zozote zilizotolewa kuhusu mapendekezo 12 yaliyokataliwa.

Wazanzibari wanalalamika kuwa na idadi ya mambo ya Muungano iliyoongezwa kinyemela kutoka 11 hadi 22 bila ridhaa ya Wazanzibari, hili lazima litafutiwe ufumbuzi.

Niliwahi kutoa wito na kuwakumbusha viongozi kuhusu amani ya nchi hii. Naamini kuwa, kama serikali ingepuuza maoni ya wananchi wanaotaka katiba mpya, uwezekano wa kusambaratisha taifa ulikuwa mkubwa. Nitumie nafasi hii kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuchukua uamuzi mgumu, najua kuna baadhi ya viongozi hasa wale wenye uroho wa madaraka wanaumia kimoyo moyo. Tunajua serikali katika kuamua hilo imeangalia maslahi ya taifa.

Serikali iwaache wananchi waamue jinsi ya kutawaliwa maana katiba ndiyo inayosimamia viongozi wote akiwemo rais wa nchi. Nasisitiza mijadala hii ifanyike bila kutishia mtu au kundi la watu ili tupate katiba mpya inayokidhi mahitaji ya wengi.

Ndugu zangu, nilipongeze bunge kupitia kamati yake ya Katiba na Utawala Bora kwa kuongeza muda wa kuuchambua muswada huo wa Sheria ya Mapitio ya Marekebisho ya Katiba, badala ya kufanywa haraka haraka kama ilivyopangwa awali.

Sasa nawaomba Watanzania wote wakiwemo wasomi, wafanyakazi, wakulima, wanafunzi, wanavyuo, walemavu, madhehebu ya dini, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO), vyama vya siasa na makundi mengine ya kijamii, wawe huru kujadili mapendekezo ya muswada huu utakaoletwa ukiwa katika lugha ya Kiswahili.

Wanasheria wetu serikalini wajiulize, waliuandika kwa Kiingereza kwa faida ya nani? Hilo ni kosa. Siku za nyuma tumeshuhudia nchi yetu ikiingizwa kwenye matatizo mazito kutokana na wanasheria kufanya mambo ndivyo sivyo. Mfano ni mikataba mbalimbali ya serikali ambayo imeiingiza nchi katika malipo ya mabilioni ya shilingi. Msifanye hivyo, vinginevyo mtadharaulika.

Jipu limepasuka siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages