UVCCM KUPAMBANA NA KINA SITTA, SUMAYE - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

UVCCM KUPAMBANA NA KINA SITTA, SUMAYE

 
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema utahakikisha kwamba vigogo ambao wamekuwa wakizungumza nje ya utaratibu wa vikao wanatupwa nje ya ulingo wa siasa za chama hicho tawala.

Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Benno Malisa wakati akisoma maazimio ya Mkutano wa Baraza Kuu uliomalizika jana mjini Dodoma.

Katika siku za karibuni baadhi ya makada wa CCM wakiwamo, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe, Mawaziri Wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa wamekuwa wakinyooshewa vidole na baadhi ya wanaCCM wakiwatuhumu kuzungumza mambo ya chama hicho nje ya vikao.

Bila ya kuwataja majina vigogo hao, Malisa alisema tabia ya baadhi ya vigogo wa CCM kuropoka mambo nje ya utaratibu wa vikao vya chama, inaonyesha kuota mizizi hali inayokifanya kidharauliwe.Alisema wakati ukifika vijana watawataja kwa majina na kuwaambia Watanzania kuwa hao wamepoteza sifa za kuchaguliwa kwa kuwa hawana nidhamu ndani ya chama.

“Sisi vijana tunasema kuwa watu kama hao wasipewe nafasi kabisa ndani ya chama hiki. Nasema tutapigana ndani na nje ya vikao vya chama kuhakikisha kuwa watu wa aina hiyo hawapati nafasi yoyote ya kuchaguliwa,” alisema na kuongeza,“Kama ni utovu wa nidhamu basi ni afadhali tuitwe sisi kwenye vikao vya maadili tukasutwe ila msimamo ni kuwa hatutakubali kulala usingizi na kuruhusu watu hao wapewe nafasi.”

Alisema katika vita hiyo, wapo viongozi ambao ni wakorofi na ambao hawatakubali hivyo mkakati wa vijana ni kuwapinga hadharani kuanzia ngazi ya vikao vya chini hadi vya uteuzi na ikishindikana majina yao yakapitishwa basi vijana watazunguka nchi nzima kuwaambia wanaCCM wasiwape kura.

Sumaye azungumza
Kwa upande wake, Sumaye, alisema anajiandaa kutoa kile alichokiita msimamo wake kuhusiana na kauli za UVCCM.Sumaye akinekana kuwa mwenye taarifa za ‘makombora’ hayo ya vijana alisema ataitisha mkutano wa waandishi na kutoa msimamo wake."Nataka nitafute siku rasmi niitishe mkutano na ninyi mkiwa wengi kutoa msimamo wangu kuhusu jambo hilo," alisema.

Hivi karibuni, Sumaye alikitaka chama hicho tawala kujibu hoja za Chadema na kiache kutumia dola kuzima hoja.
Sumaye alisema hayo alipozungumza na Gazeti dada la Mwananchi Jumapili kwamba, hoja za Chadema ni za kisiasa kwa lengo la kukamata dola hivyo zinapaswa kujibiwa kisiasa na si vinginevyo.

Kauli hiyo iliwachefua viongozi wa CCM na kupitia kwa Mkuu wa Kitengo cha Propaganda, Hizza Tambwe kilitoa kauli kikimwelezea Sumaye kama mtu anayesaliti chama kutokana na kushindwa kutoa kauli ndani ya vikao husika.Hata hivyo, Sumaye alijibu shutuma hizo akisema tatizo CCM kwa sasa ni kuwa na baadhi ya watu wenye upeo mdogo na wasiojua historia ya chama kilikotoka.

Kupambana na Chadema
Akizungumzia maandamano yanayofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema UVCCM kitapambana na chama hicho kikuu cha upinzani kwa madai kuwa sasa kimevuka mipaka.

Alisema kwa hali ilipofikia kwa sasa ni wazi kuwa vitendo vya Chadema haviwezi kuvumiliwa na akaitaka Serikali kukichukulia hatua za haraka chama hicho cha upinzani, vinginevyo jeshi la vijana wa CCM litapambana nao.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM na Serikali kutoa vitisho kwa Chadema kuhusu maandamano kinayoyaendesha.

Chadema kilianza kuendesha maandamano Kanda ya Ziwa kwa kupinga mfumuko wa bei pamoja na malipo kwa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans. Kilitangaza kufanya maandamano nchi nzima.Lakini jana, Malisa alisema kuwa Chadema watashughulikiwa kwa namna yoyote ingawa vijana wa CCM watafanya hivyo bila ya kuvunja sheria za nchi.

Hata hivyo, hakutaja mikakati wala njia zitakazotumika kukishughulikia Chadema: “Hatuwezi kutaja mikakati yetu kwani mtu hawezi kutangaza mbinu zake za kivita lakini tutafanya maajabu bila ya kuvunja amani ya nchi.”

Alisema Baraza Kuu la UVCCM liliwapa maagizo vijana wote nchini kupambana na Chadema kwa kuwa Serikali inaonyesha kusuasua kuwadhibiti.

Kamati ya kurejesha uhai
Katika hatua nyingine, Baraza Kuu la UVCCM limeunda kamati maalumu ya kushughulikia uhai wa Umoja huo ambao lilisema kuwa unaanza kupoteza mwelekeo.

Kamati hiyo ya watu wanane itakuwa chini ya uenyekiti wa Hussein Bashe. Pamoja na mambo mengine, itazunguka nchi nzima katika kipindi cha miezi minne kupata maoni ya watu mbalimbali juu ya namna gani jumuiya hiyo inaweza kurudisha heshima yake kwa Watanzania kama ilivyokuwa mwanzo.

Kamati hiyo inatarajia kumaliza kazi yake na kuiwasilisha Julai mwaka huu, wakati baraza hilo litakapokutana kupitisha jina la mgombea uenyekiti wa UVCCM ambaye uchaguzi wake utafanyika Agosti mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutangazwa, Bashe alisema kamati yake itakutana na makundi mbalimbali likiwamo Jukwaa la Wahariri wa vyombo vya habari ili kupata maoni yao.

Katika kamati hiyo Bashe atasaidiwa na wenyeviti wa mikoa Antony Mavunde (Dodoma), Rogers Shemwelekwa (Tanga) na Fadhili Ngajilo (Iringa). Wengine ni Riziki Pemba na Daudi Ismail kutoka Zanzibar na Ashura Seng’ondo na Zuberi Bundara kutoka Bara.
CHANZO: MWANANCHI MACHI 21, 2011

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages