Askari Pamoja Na Raia Wakikitahidi Kuondoa Mwili Wa Kichanga Hiko Katika Mto
Askari Wakiondoa Mwili wa kichanga na Kukiweka Kwenye Kanga tayari kukipeleka Hospiali
NA DUNSTAN SHEKIDELE, GPL MOROGORO
UKATILI wa kutisha umetokea leo mjini Morogoro ambapo mwanamke mmoja ambaye hakufahamika jina lake mkazi wa mkoani hapa, amejifungua mtoto chini ya daraja na kuamua kumtupa ndani ya maji.
Tukio hilo la kuhudhunisha limetokea leo alfajiri mtaa wa River Side kata ya Mwembesongo mkoni hapa, ambapo mwanamke huyo anadaiwa kujifungua mtoto huyo wa kiume chini ya daraja la Kichangani kisha kikizamisha kichanga hicho ndani ya mto huo.
Baadhi ya kina mama waliokuwepo eneo hilo la tukio huku wakiwa na huzuni kubwa walipohojiwa na matandao huu, walidai kwamba majira ya saa 5 asubuhi walishuhudia kiumbe hicho kikielea kwenye maji ya mto huo huku kikiwa tayari kimeshakufa.
"Sisi tuna bustani zetu za mchicha zilizopo pembezoni mwa mto huu,hivyo tulipokuwa tukichota maji ya kumwagilia tukashuhudia kichanga hicho kikiwa kimezamishwa kwenye maji huku pembeni kuna damu nyingi hivyo tukahisi mwanamke amejifungua leo alfajiri kwani jana jioni tulikuwa eneo hili hatukuona hali hii.Huu ni ukatili mkubwa sana," alisema kwa uchungu Bi. Asha Said mjasiriamali wa mboga mboga.
Aliongeza kusema kwamba kwa siku za hivi karibuni madaktari wengi wamekuwa waoga wa kutoa mimba kubwa hivyo hutumia ujanja wa kuwachoma sindano za uchungu wanawake na kisha kuwashauri wakazalie nje ya eneo la hospitali zao.
"Huyu mwanamke kazalia hapa hapa darajani baada ya kupigwa sindano ya uchungu,damu na uchafu vyote hivi hapa," alisema Bi. Asha.
Mwandishi wetu alifanikiwa kuzungumza na mjumbe wa serikali ya mtaa wa River Side, Bw. Saleh Kuzegele ambapo alidai kwamba tukio hilo limetokea mpakani mwa mtaa wake na mtaa wa J50.
"Mimi mtaa wangu ni huku tunatenganishwa na daraja hivyo alikozalia mama huyo ni mtaa wa J50 lakini naweza kuzungumza kwakuwa tukio hilo nimelishuhudia, ni kwamba majira ya saa 5 kina mama wanaofanya shughuli za kumwagia mchicha walinipa taarifa kwamba chini ya daraja kuna mtoto mchanga katupwa nilipofika nikamkuta mtoto huyo na kutoa taarifa polisi," alisema kiongozi huyo wa mtaa.
Alipoulizwa kwamba katika mtaa wake hakukuwa na mwanamke aliyekuwa mjamzito ambaye kwa sasa hana mtoto alisema, hilo kwa sasa ni mapema sana lakini atafanya utafiti katika mtaa wake kwa kusaidiana na wananchi wa mtaa huo pamoja na ule wa J50.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)