MREMA ATUA LOLIONDO KUIMARISHA AFYA YAKE - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MREMA ATUA LOLIONDO KUIMARISHA AFYA YAKE

 
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Augustine Mrema.
MWENYEKITI wa TLP, Augustine Mrema, ametinga Loliondo kwa Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT),  Ambilikile Mwasapile kunywa dawa na kutamba ni kwa ajili ya kuongeza nguvu ya mwili kupambana na ufisadi.

Mrema, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), alisema jukumu alilokabidhiwa kuzunguka nchi nzima ni kubwa linalohitaji kuimarisha afya yake.

“Kazi niliyokabidhiwa ni kubwa, kuzunguka nchi nzima kupambana na ufisadi kunahitaji kuimarisha afya yangu,” alisema Mrema na kuongeza:

“Bila kuimarisha afya huwezi kufanya kazi hii niliyokabidhiwa, waeleze Watanzania kuwa nimeimarisha afya sasa nikupambana na mafisadi kwenye halmashauri nchini kwa kwenda mbele.”

Alisema Watanzania wanatakiwa kumshukuru Mungu kwa ‘kuwashushia’ Mchungaji mstaafu Ambilikile Mwasapile (76), kwa sababu hawatumii gharama kubwa zaidi ya 500.

“Kama angekuwa Marekani tungeenda kwa Sh500? dawa yake haina kuchakachua unakunywa. Dawa nimekunywa na nimerudi na picha nimepiga naye ” alisema Mrema kwa kujiamini.

Hata hivyo, Mrema hakubainisha magonjwa yanayomsumbua hadi kwenda kwa Mchungaji Mwasapile, ingawa anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa muda mrefu. Siku za hivi karibuni vigogo wengi wa Serikali na CCM wamekuwa wakienda Loliondo kwa ajili ya tiba.

Serikali itegemee maajabu
CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema Serikali itegemee maajabu zaidi ya tiba za asili kuliko ya Loliondo, kwa kuwa wananchi wamechoka na ubabaishaji wa sekta ya afya.Profesa Lipumba alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, umati unaoendelea kufurika kwa Mchungaji Mwasapile ni kiashiria kwamba Watanzania wamekata tamaa na huduma za afya zinazotolewa na Serikali.

“Ikiwa Serikali haitajali huduma muhimu za afya kwa wananchi wake, tutarajie mengi zaidi ya haya ya Loliondo,” alisema Lipumba.

Alisema wananchi wakichoka na kukata tamaa na chombo chenye dhamana ya kuwahudumia, watatafuta njia mbadala ya kujikwamua na tatizo kama ilivyokuwa Loliondo.

Profesa Lipumba alieleza kuwa kasi ya watu kwenda kutafuta tiba mbadala kwa mchungaji, inaonyesha kuwa Watanzania wameshakata tamaa na huduma za afya zinazotolewa hospitalini.

"Kimsingi hii ni dalili ya wazi kuwa, sekta ya afya imeshindwa kazi. vinginevyo isingewezekana watu watoroke hospitalini kwenda Loliondo," alisema.

Profesa Lipumba alisisitiza kuwa watu kukimbia tiba za hospitali na kwenda kutafuta tiba mbadala ni aibu kwa taifa hasa kwa sekta ya afya ambayo imeajiri watu na kuwalipa mishahara kwa kazi hiyo.

“Ni kiashirio kibaya sana kwa taifa  kuona watu wakiwa wanatorosha wagonjwa wao hospitalini  kutafuta tiba mbadala," alisema.

Profesa Lipumba aliongoza kuwa umati uliojaa Loliondo unaonyesha picha halisi kuwa, Watanzania wengi ni wagonjwa, lakini sekta ya afya haina uwezo wa kuwahudumia.

Profesa Lipumba ametoa kauli hiyo huku maelfu ya watu yakiendelea kumiminika Loliondo kupata tiba ya mchungaji huyo aliyoeleza kuwa aliigundua kwa njia ya maono.

Ongezeko la watu wanaoelekea Loliondo limezidi hasa baada ya Serikali kubariki tiba hiyo inayotolewa katika  kijiji cha Samunge wilayani Ngorongoro.

Mchungaji, Mwasapila juzi alipongeza uamuzi wa Serikali kuondoa tishio la kuzuia kutoa dawa kwani watu wengi wamekuwa wakinufaika na dawa na mahitaji yanaendelea kuwa makubwa.

“Tunamshukuru Waziri William Lukuvi kwa kuruhusu dawa iendelee kutolewa na kutoa ahadi ya kuleta huduma mbalimbali muhimu katika kijiji hiki,” alisema Mchungaji Mwasapile.

Chakula, malazi
Mmoja wa wasaidizi wa mchungaji huyo, Peter Dudui alisema jana kuwa kuanza kupatikana hudumu muhimu katika eneo hilo kama chakula, vyoo na mahala pa kulala kumechangia kupunguza wimbi la vifo vya wagonjwa.

“Sasa vifo hakuna, wagonjwa wanaokuja wanapata huduma kama chakula na maji na pia wanapata mahali pa kulala. Ingawa sehemu za kulala ni chache zinasaidia sana,” alisema Dudui.

Ijumaa wiki iliyopita, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alitangaza kuwa Serikali imeruhusu Mchungaji Mwasapile kuendelea na huduma zake za tiba na kwamba itatoa ushirikiano wa kusimamia na kujenga mazingira mazuri ya kuendelea kutoa huduma.

Tamko hilo lilitolewa wakati ambapo tayari kulikuwepo na tetetsi kwamba Serikali imekusudia kumsimamisha Mchungaji huyo hadi hapo uchunguzi maalumu wa kitaalamu utakapofanywa kwa dawa yake.

Tangazo hilo la Serikali ambalo limetolewa wakati bado wataalamu wa afya wanachunguza dawa hiyo, limehamasisha maelfu kwa maelfu kumiminika kupata tiba.

Msururu mirefu ya magari yanayotoka Arusha mjini kuelekea katika kijiji hicho ambacho sasa kinaiitwa 'Kijiji cha Babu', jana ilionekana katika barabara ya Arusha hadi Ngorongoro.

Walioshuhudia msafara huo mrefu walisema kitu kibaya walichoshuhudia kwenye msafara huo ni madereva walombele kutoruhusu wenzao wanaookuja nyuma yao kwa kasi kutokana na kila mmoja kujaribu kuwahi kufika kabla ya mwingine kunywa dawa.

Baadhi ya watu walioshuhudia misafara hiyo, walisema ni vigumu madereva kuwaruhusu wenzao wanaokuja nyuma kwa hofu ya kuchelewa kwenye foleni ya dawa.
CHANZO: MWANANCHI MACHI 14, 2011

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages