KILI MUSIC AWARD, HUU NI UTANI - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

KILI MUSIC AWARD, HUU NI UTANI

Na Saleh Ally
UTOAJI wa tuzo za muziki za Kilimanjaro uliofanyika Jumamosi iliyopita unaweza kusema umefana na tunapaswa kuwapongeza waandaaji kutokana na mafanikio waliyofikia.

Msomaji wa Championi Jumatano, nataka kukukumbusha kuwa nimekuwa nikipambana mara kadhaa kuhusiana na uozo ambao unajitokeza ndani ya tuzo hizo ingawa kuna watu wamekuwa wakiniona kama adui yao, hilo halinitishi.

Kwa kuwa tuzo hizo zinahusisha Tanzania, maana yake nchi yetu. Basi nina kila sababu ya kuzungumza kwa kupongeza na kukosoa kwa maana ya kujenga. Ndiyo maana leo nimeanza kwa kupongeza.

Angalia suala la msanii 20% amechukua tuzo tano, kitu ambacho kinaonyesha ni ukomavu mkubwa katika utoaji wa tuzo hizo. Zamani ilikuwa inaonekana ni kama suala la kupendelea kufanya hivyo, wakati kinachotakiwa ni kuangalia suala la uhakika, ubora wa kazi na si ‘ku-balance’, nawapongeza katika hili.

Hakika wamejitahidi, pamoja na mazuri mengi ambayo nimeyaona katika tuzo za mwaka huu. Bado nimeshangazwa sana na ushindi wa Mpoki katika kipengele cha Wimbo Bora wa Asili wa Tanzania!

Awali nilianza kuzungumza kuhusiana na wimbo huo kuingizwa katika tuzo hizo, kwangu niliona ungeweza kupewa nafasi ya kuingia. Lakini si katika kipengele cha wimbo wa asili. Naona ni kama wimbo fulani kwa ajili ya vichekesho.

Hata Mpoki mwenyewe ambaye ni msanii mwenye kipaji cha juu katika uchekeshaji, sidhani kama anaona ni sahihi wimbo huo kuwa hapo. Kibinadamu inaweza kuwa ni vigumu kujikosoa, lakini kwangu naona kama watoa tuzo wanafanya utani.

Ninaona kama wanafanya utani kwa kuwa, hebu angalia katika kipengele hicho cha Wimbo Bora wa Asili kulikuwa na nyimbo kama ‘Adela’ wa Mrisho Mpoto, ‘Kariakoo’ wa Mataluma, ‘Ahmada’ wa Offside Trick waliomshirikisha Bi Kidude na ‘Wa Mbele Mbele’ wa Ommy G.

Sioni kigezo chochote kinachoweza kutumika kuupa tuzo wimbo wa ‘Shangazi’, kama utaufuatilia utagundua ubunifu wake umetokana na wimbo mwingine unaoitwa ‘Mjomba’ wa Mrisho Mpoto’. Alichofanya Mpoki ni kukopi na kubadilisha maneno.

Uimbaji na kila kitu, unavyoanza hadi unavyoisha, huku yeye zaidi akionekana kutania akigeuza maneno ya Mpoto, unaweza kusema alikuwa anapandia mule mule tu. Sasa inashangaza eti kuambiwa ndiyo wimbo ulioshinda. 

Ukiangalia vigezo vya kumpata mshindi vilivyowekwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), utaona vitu vinavyoangaliwa ni midundo ambayo Mpoki amekopi ya wimbo mwingine na inajulikana. Mashairi yanatakiwa kuwa na mafunzo na burudani, ukiangalia ya kwenye ‘Shangazi’, sioni kama yana mafunzo hata chembe.

Ubunifu ni sehemu ya vigezo, kama kuiga au kugeuza wimbo wa mwingine ni ubunifu, watakuwa sawa. Pamoja na mpangilio mzuri ambao mimi kweli naona ni mzuri lakini unauliwa na kipengele cha ubunifu kwani alipangilia kwa ubunifu wa mwingine.

Sioni kigezo chochote katika kipengele hicho kinachoonyesha kuwe na vichekesho. Kwani ‘Shangazi’, kwangu haifundishi zaidi ya kuchekesha, yaani inaburudisha. Na inakosa vigezo vingi vya muziki wa asili.

Sitaki nikufanye uamini wimbo huo wa Mpoki ni mbaya. Mimi ni kati ya wanaopenda kuusikiliza ili nicheke, kweli unaburudisha. Lakini kwa kuwania tuzo hasa katika kipengele hicho cha nyimbo za asili ninaamini kabisa majaji walifanya utani au walitaka kutuchekesha.

Achaneni na kisingizio cha kura za mashabiki ambacho ninaamini mmekuwa mkikifanya kama nguzo yenu. Wengine tunajua utaratibu wa upigaji kura unavyokwenda na zina asilimia ngapi katika kumtoa mshindi. Lawama ziwaendee majaji kwa kushindwa kuwa makini.

Waandaaji bado ninawapongeza ingawa nao ninawapa angalizo kwa tuzo za mwakani (tuombe uzima), kwamba wanachotakiwa kuwa makini zaidi. Pia ninawaongezea wahakikishe wanasimamia kwa ukaribu suala la nafasi ya wapiga picha. Ukiangalia sherehe ya utoaji tuzo hizo zilizokuwa zinaonyeshwa kwenye runinga, utaona wapiga picha wanaranda ovyo na kuharibu ladha kabisa.

Huwezi kuwalaumu wapiga picha hao kwa kuwa nao wanataka kupata kilicho bora. Wanafanya hivyo kwa kuwa hawakuwekewa utaratibu mzuri na sehemu ya kufanyia kazi zao. Mnaweza kufanya kitu kizuri lakini mkaharibu kwa kingine kidogo tu ambacho mlikidharau.

Mwisho nawakumbusha, utani kama huo wa ‘Shangazi’ wa Mpoki usijirudie siku nyingine!
Kwa Msaada Wa Global Publisher Tanzania

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages