IGP Mwema, katika picha ya Maktaba
Na Francis Godwin.
Na Francis Godwin.
Ajali zinazidi kushika kasi nchini baada ya kutokea ajali mbili mfululizo na kuua watu 13, wasanii wa kundi la Five Star na watatu siku ya pili baada ya ajali hiyo, na leo ajali nyingine iliyohusisha Coaster yenye namba za usajili T. 566 AZP, imeua watu 16 na kujeruhi 18 mkoani Pwani.
Watu hao wamefariki dunia katika ajali mbili tofauti zimetokea leo kwa kuhusisha magari matano, ikiwamo Coaster iliyokuwa ikitokea Morogoro kwenda Dar es Salaam.
Ajali ya Coaster ilitokea eneo la Mbala wilayani Bagamoyo, ambapo basi hilo lililigonga kwa nyuma lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 353 AAG lililokuwa limeegeshwa pembeni.
Kwa mujibu wa walioshuhudia ajali hiyo iliyotokea majira ya saa 3:45 usiku wamedai kuwa basi hilo lilikuwa likitaka kulipita lori ambalo lilikuwa limeegeshwa pembeni mwa barabara lakini dereva wa basi hilo aliliona gari jingine likitokea mbele.
Walisema gari lililokuwa likija mbele lilikuwa ni lori aina ya Fuso lenye namba za usajili T 398 ATB, hivyo kumfanya dereva wa Coaster kuamua kurudi nyuma na kugonga tela la Scania pamoja na kukwaruzana na Fuso hiyo na baadaye kupinduka.
Mashuhuda hao walisema kuwa baada ya ajali hiyo watu 14 walifariki dunia papo hapo huku wengine 12 walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali Teule ya Tumbi.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Absalom Mwakyoma, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema waliofariki dunia katika ajali hiyo ni wanaume 12, mwanamke mmoja pamoja na mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 11.
Mwakyoma, aliwataja maiti waliotambuliwa kuwa ni Salehe Rashidi (21) mkazi wa Chaalinze, Rajabu Mnyalikwa (35) mkazi wa Ubena, Ediluck Mluge (28) mkazi wa Mbala Chalinze na Amina Saidi (35) mkazi wa Mbala.
Wengine ni Charles Mhando (35) mkazi wa Mbala Chalinze, Gift Charles ambaye hajajulikana alikokuwa akiishi, huku maiti wanane bado hawajatambuliwa na wamehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Tumbi.
Aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo waliolazwa katika hospitali hiyo ni Mkunduge Mganga (29) mkazi wa Dumila, Godwin Sakarani (55), Haruni Mgangaruma (24) mkazi wa Mbarali (Mbeya) na Khalid Hamza (29) mkazi wa Mawenzi, Morogoro.
Wengine ni Edwin Mbele (49) Ofisa ununuzi Kilombero, Madaraka Rashidi (42) mkazi wa Bunju jijini Dar es Salaam, Leornad Mkoba (45) mkazi wa Vingunguti jijini Dar es Salaam, Ester Shija (38) mkazi wa Dar es Salaam, Juma Omari (29) mkazi wa Morogoro na Justine Mathew (31) mkazi wa Dar es Salaam.
Alibainisha kuwa majeruhi wawili ambao hawajatambuliwa hali zao si nzuri, wamekimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Katika tukio jingine, ajali nyingine iliyotokea eneo la Ubena Zomozi, barabara kuu ya Dar es Salaam - Morogoro, imesababisha vifo vya watu watatu baada ya magari matatu kugongana.
Katika tukio hilo gari lenye namba za usajili T 817 AZU /T 951 AMZ Scania lori likiwa limebeba mbao likitokea mkoani Iringa kwenda Dar es Salaam lililigonga kwa nyuma lori lenye namba za usajili T 890 aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa likitokea Kiteto kwenda Dar es Salaam.
Baada ya kugongwa gari hilo lililokuwa likiendeshwa na Anthony Matende (56) mkazi wa Dodoma nalo lilikwenda kugonga gari lenye namba za usajili T 317 ATN Mitsubishi Fuso lililokuwa limeharibika.
Kamanda Mwakyoma alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa tisa usiku na kuwataja waliofariki dunia katika ajali hiyo ni pamoja na utingo wa gari lenye namba T 317 ATN Rober Luwena (30) mkazi wa Mtoni Dar es Salaam na Miraji Mwinyi (22) mkazi wa Ngusero, Kiteto.
Mwingine aliyefariki dunia alijulikana kwa jina moja la Joseph, ambaye ni fundi aliyekuwa anatengeneza gari namba T 317 ATN lililokuwa limeegeshwa pembeni baada ya kuharibika.
Kamanda Mwakyoma aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Anthony Matende dereva wa gari lenye namba za usajili T 890 AUR, Aman Hamis (28) mkazi wa Matui, Kiteto na Myemo Hamis (19) mkazi wa Matui, Kiteto.
Wengine ni Leokadia Leonard (24) mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam, Ibrahimu Zakayo (42) mkazi wa Matui Kiteto, Charles Mhina (42) mkazi wa Matui, Kiteto wote walikuwa abiria wa gari lenye namba za usajili T 890, ambao wamelazwa katika kituo cha afya Chalinze.
Maiti wamehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Tumbi. Chanzo cha ajali kimeelezwa kuwa ni mwendo kasi wa dereva wa gari lenye namba za usajili T 817 AZU/T 951 AMZ Scania.
Na Francis Godwin
Na Francis Godwin
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)