ZIJUE KAMATI ZA BUNGE....LOWASA BOSI WA SITTA NA MEMBE - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

ZIJUE KAMATI ZA BUNGE....LOWASA BOSI WA SITTA NA MEMBE

 
*LYATONGA AMRITHI DK SLAA, ZITTO, SERUKAMBA, JANUARI NAO WAULA
WABUNGE jana waliwachagua wenyeviti wa kamati 16 za Bunge zilizotangazwa juzi usiku na Spika wa Bunge, Anne Makinda, huku waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa (pichani) akichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Hatua hiyo inamweka Lowassa kuwa bosi mpya wa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kwani watalazimika kuripoti kwake masuala yote yanayohusu wizara zao katika vikao vya kamati hiyo nyeti.

Habari zinasema Mbunge wa Ilala Mussa Azan Zungu amechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa kamati hiyo. Zungu alikuwa akishikilia nafasi hiyo wakati wa bunge la tisa, wakati kamati hiyo ilipokuwa ikiongozwa na Mzee John Malecela.

Taarifa za uhakika za uchaguzi wa wenyeviti wa kamati hizo unaonyesha kuwa Zitto Kabwe, John Cheyo na Augustino Mrema wametwaa uenyekiti wa Kamati za Fedha ambazo kwa mujibu wa kanuni za Bunge hushikiliwa na wabunge wa upinzani.

Kadhalika Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, akiongoza kamati inayosimamia Wizara ya Ujenzi, inayoongozwa na Waziri, Dk. John Magufuli na Naibu wake, Dk. Harrison Mwakyembe, pia Wizara ya Uchukuzi inayoongozwa na Waziri, Omar Nundu na Naibu wake Dk. Athuman Mfutakamba.

Juzi Spika Makinda alitangaza kamati hizo zikiwa na sura na wajumbe mchanganyiko, pamoja na wajumbe kati ya 15 na 28 wengi wakiwa wapya na mabadiliko ya sura katika kamati hizo yakikutanisha wabunge wa vyama tofauti.

Hali hiyo inaweza kuzifanya kamati hizo kuwa na changamoto kubwa katika kazi zake kutokana na wabunge hao wa vyama tofauti kuwa na itikadi na mitazamo tofauti ya kisiasa na utendaji wa shughuli za umma katika kamati hizo.

Matokeo yanaonyesha kuwa, Zitto  amerejeshwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma,huku  Mrema akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa ambayo Bunge lililopita ilikuwa ikiongozwa na Dk Willibrod Slaa wa Chadema.

Cheyo naye amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, nafasi ambayo aliishika pia katika bunge la tisa.

Habari hizo zinaonyesha kuwa Januari Makamba(CCM)aliyembwaga William Shellukindo jimbo la Bumbuli uchaguzi mkuu uliopita ataongoza Kamati ya Nishati na Madini na Jenista Mhagama akiongoza Kamati ya Maendeleo ya Jamii.

Kabla ya kubwagwa na Makamba, William Shellukindo alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini katika Bunge la tisa lililoishia mwaka 2010.

Kamati ya kanuni za bunge tayari inaongozwa na Spika Makinda na naibu wake Job Ndugai akiwa makamu.

Mpangilio wa kamati hizo, inaonyesha kuwa kiongozi wa upinzani bungeni Freeman Mbowe (Chadema) ni mjumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi, akiwa na mtangulizi wake, Hamad Rashid Mohamed (CUF) aliyekuwa kiongozi wa upinzani katika bunge la tisa.

Katika kamati hiyo yenye wajumbe 23 wapo pia Abdallah Kigoda, Rostam Aziz na Mohamed Missanga wote wa CCM.

Lowassa katika kamati anayoingoza, pia wapo wabunge wawili wa majimbo ya Ilala, Zungu na Eugen Mwaiposa wa jimbo la Ukonga wote wa CCM wakikutanishwa na Rachel Mashishanga (Chadema) na Khalifa Suleiman Khalifa (CUF) katika kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama pamoja na wajumbe wengine ambao jumla yao ni 20.

Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ina wajumbe 20 huku baadhi ya wajumbe watakaokutanishwa na kamati hiyo wakiwa, Nimrod Mkono, Andrew Chenge wa (CCM), Tundu Lisu, Halima Mdee na Mustafa Akunaay wa Chadema, pamoja na Felix Mkosamalali wa NCCR.

Cheyo wa UDP anayeongoza Kamati ta Hesabu za Serikali yenye wajumbe 15, baadhi ya wajumbe wake ni Hezekiah Chibulunje (CCM), Vicent Nyerere na Lucy Owenya wa Chadema.

John Mnyika (Chadema), Zainab Kawawa (CCM), Rukia Kassim Ahmed wa CUF watakutanishwa katika kamati ya Sheria Ndogo ambayo pia inaundwa na wajumbe 15.

Kwa mujibu wa matangazo ya Bunge, Kamati ya Miundombinu ambayo itaongozwa na Serukamba, itakuwa na wajumbe 26 huku baadhi wakiwa Anne Kilango,Mohamed Shabiby(CCM), Said Amour Arfi (Chadema), Regia Mtema (Chadema) ambapo pia wamo Mohamed Habib Mnyaa(CUF) na Moses Machali wa NCCR.

Christopher Ole Sendeka na Makamba wa CCM pamoja na wajumbe wengine jumla wakiwa 27 wanaunda Kamati ya Nishati na Madini inayomjumuisha pia Profesa Kulikoyela Kahigi wa Chadema na Yusuph haji Khamis wa CUF.

Baadhi ya watakaokutanishwa katika Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma inayoongozwa na Zitto (Chadema) ni Jerome Bwanausi (CCM) na  Amina Mohamed Mwidau (CUF)ambapo kamati hiyo ina wajumbe 15.

Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa inayoongozwa na Mrema itakuwa na wajumbe 15 huku baadhi ya watakaokutanishwa wakiwa ni Zabein Mhita, Godfrey Zambi wa CCM, Joseph Selasini na Susan Kiwanga (Chadema) na Kurthum Juma Mchuchuli wa CUF.

Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira itawakutanisha wajumbe 28 baadhi wakiwa ni Philemon Ndesamburo (Chadema) Magdalena Sakaya (CUF), Hamad Yusuph Masauni, Zhakia Meghji na James Lembeli wa CCM.

Profesa David Mwakyusa, Profesa Peter Msolla, Nameloki Sokoine wa CCM, Rose Kamili wa Chadema, Salim Hemed Khamis wa CUF watakutanishwa katika kamati ya Kilimo, Mifugo na Mazingira yenye wajumbe 27, ambapo Livingstone Lusinde (Kibajaji), Jenista Mhagama wote wa CCM, Joseph Mbilinyi(Chadema) na Moza Abedy Saidy wa CUF watakutanishwa katika kamati ya Maendeleo ya Jamii yenye wajumbe 24. 

Kamati ya  Viwanda na Biashara yenye wajumbe 26 itawakutanisha Chiku Abwao, Godbles Lema na Ezekiel Wenje(Chadema), Gaudence Kayombo na Stella Manyanya pamoja na wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo huku wajumbe 14 wakitoka CCM na 12 vyama vya upinzani.

Kamati nyingine zilizoundwa ni kamati ya huduma za jamii ikiwa na wajumbe26, kamati ya masuala ya ukimwi ina wajumbe 20 na kamati ya Haki,Maadili na Madaraka ya Bunge iliyo na wajumbe16.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages