RAISI JAKAYA KIKWETE ZIARANI MAURITANIA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

RAISI JAKAYA KIKWETE ZIARANI MAURITANIA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini asubuhi ya leo, Jumapili,Februari 20, 2011, kwenda Nouakchott, Mauritania, kushiriki katika Mkutano wa wakuu wa nchi sita za Afrika waliopewa jukumu la kutafuta suluhisho la kisiasa katika nchi ya Afrika Magharibi ya Ivory Coast.

Mkutano huo wa kundi la nchi zinazojulikana kama High Level Panel for the Resolution of the Crisis in Ivory Coast utamshirikisha Rais Kikwete na marais wenzake wa Mauritania, Burkina Faso, Chad, Afrika Kusini, Equatorial Guinea ambayo inashikilia uenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) kwa sasa na, Nigeria ambayo ni uenyekiti wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS).



Baada ya kumalizika kwa mkutano wa leo, kesho viongozi wa nchi zote sita wa kundi hilo watasafiri kwenda Abidjan, Ivory Coast ambako watakutana na viongozi hao wawili wa Ivory Coast wanaovutana kuhusu uongozi wa nchi hiyo.

Kundi la nchi hizo sita lilichaguliwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia, mwezi uliopita kutafuta suluhisho la mzozo wa kisiasa katika Ivory Coast ambao ulizuka baada ya Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Novemba 29, mwaka jana.

Katika kura zilizopigwa katika raundi ya pili ya uchaguzi mkuu huo kati ya aliyepata kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, Alassane Quattara, na Rais Laurent Gbagbo, Bw. Quattara alitangazwa kuwa mshindi na Tume Huru ya Uchaguzi ya nchi hiyo kwa kupata asilimia 54.1 kulinganisha na asilimia 45.9 za Rais Gbagbo aliyekuwa anatetea kiti chake.

Matokeo hayo yalithibitishwa na Ujumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa katika Ivory Coast, ambao ulipewa jukumu la kusimamia na kuhakikisha unafanyika uchaguzi huru na wa haki nchini humo kulingana na Makubaliano ya Linas-Marcoussis ya mwaka 2004 na, kwa mujibu wa Makubaliano ya Kisiasa ya Ouagadougou ya mwaka 2007. Matokeo hayo pia yanakubaliwa na jumuia ya kimataifa, Umoja wa Ulaya (EU), Jumuia ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), na Umoja wa Afrika (AU).

Hata hivyo, Baraza la Katiba la nchi hiyo lilibatilisha matokeo hayo, likafuta matokeo ya kura kutoka majimbo saba ya kaskazini mwa Ivory Coast ambako ndiyo ngome ya Quattara na hatyimaye kumtangaza Bw. Gbagbo mshindi.

Kutokana na hali hiyo, kila upande ulitangaza Serikali yake hata kama vyombo vya habari vya serikali, jeshi, utumishi wa umma na taasisi nyingine nyeti za Serikali zinabakia kwenye udhibiti wa Bw. Gbagbo.

Mkutano wa kutwa leo mjini Noaukchott utafunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania Mheshimiwa Mohamed Ould Abdel Aziz na viongozi wote sita wanaoshiriki katika mkutano huo wanatarajiwa kutoa maneo ya ufunguzi.

Imetolewa na
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu
.
Dar es Salaam
.
20 Februari, 2011

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages