KONA YA MCHOCHEZI: IPO SIKU FFU WATAMTWANGA RISASI WAZIRI KWA KISINGIZIO CHA KUTULIZA GHASIA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

KONA YA MCHOCHEZI: IPO SIKU FFU WATAMTWANGA RISASI WAZIRI KWA KISINGIZIO CHA KUTULIZA GHASIA

 
Ijumaa ya Februari 4, mwaka huu, kuna jambo nilijifunza kwa vitendo juu ya kufyatuka akili kwa baadhi ya askari wa kikosi cha kutuliza ghasia, maarufu kwa jina la FFU.

Nalijiridhisha kuwa wenzetu hawa wakati wanatekeleza kilichowapa ajira huwa wanalegeza nati za ubongo wao na kuwa sawa na wendawazimu wasioweza kupambanua hata vitu wanavyovitazama au kusikia.

Tukio langu la ushahidi ni lile lililotokea siku niliyoitaja hapo juu pale niliposhuhudia kundi la FFU likivamia ofisi za Kampuni ya Global Publishers, wachapishaji wa Magazeti ya Uwazi, Ijumaa, Amani, Risasi, Championi na Ijumaa Wikienda na kuanza kuwapiga waandishi na wafanyakazi bila sababu.

Askari hao ambao naomba niwaite wahuni, walivamia ofisi hizo kwa kile walichodai kuwa wanatuliza ghasia za maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliokuwa wakishinikiza nyongeza ya posho kutoka serikalini.

Kimsingi, ilikuwepo haja ya polisi kuingilia kati maandamano hayo lakini linapokuja suala la wao kuingia kwenye ofisi za watu kwa nguvu tena zilizo mbali kabisa na eneo la tukio na kuanza kupiga wafanyakazi na wananchi waliokuwa wakijenga taifa, bila shaka huo ni ukosefu wa akili.

Najiuliza, askari anapoingia chumba cha habari na kukuta wafanyakazi wakiwajibika, halafu bado wakawa na ujasiri wa kuanza kuwaburuza  na kuwatoa nje kwa kipigo, lengo lake hasa ni kutuliza ghasia au ni kuchochea?

Nasema hivi kwa sababu nimeshuhudia hata eneo ambalo halihitaji nguvu kubwa wala mabomu, walinzi hawa wamekuwa wakifanya hivyo kwa visingizio vya kutuliza ghasia.

Nikitoa mfano wa siku walipovamia Global, polisi walidiriki kumpiga hata msichana anayehudumu jikoni licha ya kuwa alikuwa amevaa mavazi rasmi ya kazi yake.

Swali linakuja kama akili za FFU wetu hazikuweza kutambua umuhimu wa chumba cha habari na waandishi, tena kwenye vurugu ndogo tu za maandamano ya wanafunzi wachache, polisi hawa wanawezaje kuheshimu haki za vyombo vya habari inapotokea hali kama ya Misri?

Nachelea kusema kuna siku polisi hawa wendawazimu watampiga risasi waziri au kiongozi yeyote wa nchi kwa kisingizio dhaifu cha kutuliza fujo.

Natafakari na kuamini kuwa kuna haja ya jeshi la polisi kujivua ujinga huu na kujivika werevu utakaolisaidia taifa letu kuendelea kuwa na utulivu.

Ni wazi kwamba kwenye ulimwengu wa harakati tulionao sasa, nchi zinazotaka kudumisha amani hazihitaji aina ya askari tuliowaona siku ile kwa sababu kizazi hiki ni cha mageuzi hivyo haki na uhuru wa watu lazima vipewe kipaumbele zaidi ya nguvu, risasi virungu na mabomu ya machozi.

Huu ni wakati wa viongozi wa jeshi hili kujifunza mbinu za kisasa za kudhibiti maandamano na ghasia kwa sababu historia inaonesha kuwa nyakati hizi watawala hawawezi tena kujilinda kwa nguvu za mabomu, vifaru na mizinga. Umma ukiamua kutafuta haki hauwezi kuogopa maji ya kuwasha au virungu vya polisi.

Inashangaza kuona maandamano ya wanafunzi yakizimwa kwa staili ya polisi kusimamisha magari ya abiria na kufanya upekuzi wa vitambulisho ambavyo kwenye nchi yetu hatujazoea utaratibu huo.

Lakini  jambo baya zaidi ni askari wenyewe kusababisha fujo zinazoleta uharibifu na upotevu wa mali ambazo baadaye wahusika huamua kuzitetea. Naogopa kuwatuhumu polisi kwa uporaji lakini pia wana tatizo hili kwa sababu yupo mbunge aliwahi kulalamika kuporwa simu.

Wakati naandika haya, nakumbuka mauaji yaliyofanywa na FFU jijini Arusha kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kutuliza ghasia, ambapo sababu zilikuwa ni maandamano ya watu kudai haki.

Leo tena polisi wanavamia chumba cha habari, wanapiga waandishi kwa kisingizio kile kile, najiuliza kesho watafanya nini kwa sababu hii hii?

Kama nilivyosema, hiki ni kizazi cha mageuzi, maandamano hayakwepeki. Kama polisi wanaona ni matukio ya ajabu, wafahamu kuwa wako nyuma ya wakati.

Wanachotakiwa kufanya ni kujifunza mabadiliko kwa vile vuguvugu linaendelea kukua. Wakiishia kudhani wana uwezo wa kupiga watu, ipo siku watajikuta barabara zote zimetapakaa waandamanaji, kitakachotokea sikijui.

Ningependa kumalizia uchochezi huu kwa kuwashauri viongozi na wakuu wa polisi ambao binafsi nawaamini sana, kuhakikisha kuwa wanafuatilia matendo ya polisi kwa raia na kuchukua hatua zinazostahili panapotokea uvunjifu wa haki za binadamu.

Wananchi wanalalamikia rushwa ndani ya jeshi la polisi, kubambikiwa kesi na uonevu, mambo ambayo sidhani kama yanahitaji siasa kwa vile yanazaa chuki kati ya polisi na raia.

Nachochea tu ndugu zangu kwa sababu walipolala Watunisia na Wamisri ipo siku tutaamkia sisi, ni vyema tukajisafisha mapema.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages