Zitto Zuberi Kabwe (Mb),
Naibu Katibu Mkuu (Bara)-CHADEMA
----------------
Ndugu zangu,
Tunalaani matumizi ya ovyo ya nguvu za Dola
Kwa mara nyingine tena, jana Jumatatu tarehe 05 Januari 2010, Jeshi la Polisi lilivuruga na kusambaratisha mkutano halali wa hadhara uliondaliwa na chama halali cha siasa jijini Arusha. Katika kuvuruga na kusambaratisha mkutano huu, jeshi la polisi liliua na kuwaumiza vibaya baadhi ya wananchi. Miongoni mwa wananchi walioumizwa ni pamoja na Mwenyekiti wa CHADEMA Mhe Freeman Mbowe, mbunge wa Arusha Mjini Mhe Godbless Lema na mke wa Katibu Mkuu wa CHADEMA mama Josephine Slaa. Wengi wa wananchi walioumizwa ni watoto na akina mama. Kama vile haitoshi, Jeshi la Polisi kwa ubabe na ukatili wa hali ya juu, liliwafuata na kuwakamata Katibu Mkuu wa CHADEMA Mhe Dk Willibrod Slaa na Mbunge wa Moshi Mjini Mhe Philemon Ndesamburo wakiwa katika Hoteli ya Mount Meru. Wabunge hawa wamedhalilishwa na jeshi la polisi bila kujali kinga ya bunge walio nayo.
Tunalaani kwa nguvu zetu zote ubabe na matumizi ya ovyo ya vyombo vya dola. Tunalaani Jeshi la Polisi kuendelea kukubali kutumiwa na wanasiasa katika kuficha udhaifu wao wa kisiasa na kiuongozi. Serikali hii imeshindwa kudhibiti ujambazi nchini kwa kisingizio kuwa haina askari na vifaa vya kutosha, lakini wana askari kedekede na vifaa lukuki vya kudhibiti na kuua wananchi wasio na hatia kwa sababu tu wanaonyesha mapenzi yao kwa vyama vya upinzani badala ya chama tawala. Jeshi la Polisi limeendelea kuvunja sheria kwa kuzuia maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa vya upinzani. Badala ya kutoa ulinzi katika mikutano ya hadhara, jeshi la polisi limegeuka kuwa watoa vibali!
Watawala na jeshi la polisi watambue kuwa hakuna nguvu ya risasi itakayoshinda nguvu ya umma inayotaka mabadiliko, na wala CCM haitaweza kulazimisha kubaki madarakani kwa nguvu ya risasi. CHADEMA tutaendelea na juhudi za kuhamasisha wananchi kudai haki zao za kidemokrasia, ikiwemo kuwajibisha viongozi waliowachagua kuwaletea maendeleo. Matumizi mabovu ya nguvu za dola kunakofanywa na watawala wa CCM ni ushahidi mwingine muhimu wa kwa nini tunahitaji Katiba Mpya kwa haraka iwezekanavyo.
Katika kipindi hiki kigumu, tukiendelea na juhudi za kuwatoa nje viongozi waliowekwa ndani kwa udhalimu, ninawaomba wananchi, wapenzi na wanachama wa CHADEMA wawe wastahimilivu na waendelee na shughuli zao. CHADEMA tutahakikisha haki inatendeka na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya askari waliosababisha maafa yaliyotokea.
Zitto Zuberi Kabwe (Mb)
Naibu Katibu Mkuu (Bara)-CHADEMA
Nimetoa kauli hii Mwanza saa 1300hrs
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)