LOWASA NA MZINDAKAYA WAZUNGUMZIA SWALA LA KATIBA MPYA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

LOWASA NA MZINDAKAYA WAZUNGUMZIA SWALA LA KATIBA MPYA

Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa.
 WATANZANIA wanapaswa kupata elimu ya angalau mwaka mmoja juu ya Katiba, kabla ya kuanza kukusanya maoni yao.

Ushauri huo umetolewa na Mbunge mstaafu wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya ambaye pia alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kusoma ‘alama za nyakati’ kuhusu Katiba mpya.

Dk. Mzindakaya alishauri kuwa Tume itakayoundwa na Rais kuanza mchakato wa kupata Katiba mpya, haina budi kwanza kuhakikisha elimu hiyo inatolewa ili wananchi waijue vizuri Katiba na kuwa na fursa nzuri ya kutoa maoni yao.

Akimpongeza Rais Kikwete alisema uamuzi wake kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba ulitolewa wakati muafaka ili kuepusha vurugu zilizokuwa zikichochewa chini kwa chini na wakati mwingine waziwazi kwa mgongo wa mabadiliko.

Mwanasiasa huyo mkongwe aliyesema kuwa amestaafu ubunge lakini si siasa, aliponda madai ya baadhi ya wana CCM, kuwa Rais hakupitia vikao vya chama katika kutoa uamuzi huo na kufafanua kuwa siasa inaangalia zaidi muktadha wa jambo husika.

Alisema hata ndani ya chama hakukuwa na namna ya kukataliwa kwa jambo hilo kutokana na kuwa tayari kuna taasisi nje na ndani ya nchi zilizotaka kutumia suala hilo kuchochea vurugu.

"Kuna vurugu nyingi nchini, zinatokea kutokana na uchochezi tu, sasa suala hili la Katiba liliishakuwa na msukumo kutoka nje na iwapo Rais angekawia kutoa tamko lingesababisha vurugu ndani ya nchi, hivyo Rais Kikwete alitumia utashi mkubwa wa kisiasa kutoa msimamo,” alisema Mzindakaya.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Viwanja vya Bunge, Mzindakaya alisema uamuzi wa Rais ni wa busara na wenye kuonesha upeo mkubwa, hivyo kilichobaki ni kuacha malumbano na kusubiri Tume itoe mawazo ili yafanyiwe kazi.

Alisema katika siku za karibuni, wanasiasa,viongozi wa dini na wanataaluma, wamekuwa wakitoa mawazo mbalimbali jambo ambalo si wakati wake, bali ni kutaka kusababisha malumbano ya kutaka serikali ngapi huku jambo la msingi likiwa ni kusubiri Tume.

Alisema Tume ikishaundwa, ambayo alisema anaamini itakuwa ni kwa maslahi ya nchi, haitakuwa na kazi ya kuandika Katiba bali ni kutoa elimu na kukusanya maoni ya wananchi na kuyapeleka bungeni, hivyo kuwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi.

Alishauri kuwa muda wa utoaji elimu ya Katiba usipungue mwaka mmoja, kutokana na umuhimu wa jambo lenyewe, kwani Watanzania wa sasa ni tofauti na wa miaka ya nyuma wanaelewa, hivyo watatoa maoni yao.

Dk. Chrisant Mzindakaya.
Mzindakaya ambaye alikuwa Mbunge kwa miaka 44, alisema Tume itakayoundwa licha ya kukusanya maoni ya watu, pia itaangalia katiba za nchi zingine kwani Rais ameshakubali kuwa na Katiba mpya hivyo hapana sababu ya kuweka viraka.

Alisema kwa uzoefu alionao kwa kipindi chake cha ubunge, tume mbalimbali ziliundwa
kukusanya maoni na kupelekwa bungeni na tena kurudishwa kwa wananchi kabla uamuzi haujafikiwa, hivyo hakuna sababu ya hofu na serikali katika kuunda Tume.

Alisema lazima serikali iratibu mchakato huo kwa kuunda Tume yenye watu watakaoweka maslahi ya nchi mbele, ambapo Serikali, wananchi na Bunge, lazima washirikishwe kwa kiasi kikubwa katika mchakato huo.

Naye John Mhala, anaripoti kutoka Arusha, kwamba Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, amempongeza Rais Kikwete kwa kukubali mabadiliko ya Katiba na kutoa mwito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao wakati ukifika.

"Rais wetu hakusubiri wananchi waandamane, na ndiyo maana kaamua kutangaza rasmi kuunda Tume ya kuratibu Katiba, naomba wakati ukifika wananchi jitokezeni na kazi hiyo ifanyike kwa amani na utulivu,” alisema Lowassa.

Alitoa kauli hiyo katika Kijiji cha Manyire, Mlangarini, wilayani Arumeru alipozungumza katika sherehe za kupongeza na kuwashukuru wananchi wa kata hiyo kwa kumchagua mgombea wa CCM, Mathias Manga kuwa Diwani wao.

Lowassa aliwataka wabunge na madiwani waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu uliopita, kutekeleza kwa vitendo ahadi walizowapa wananchi, ili kubadilisha hali zao na kuwa na imani na Serikali iliyoko madarakani.

Aliwataka viongozi kuweka kipaumbele katika kujali matumbo ya wapiga kura wao ikiwa ni pamoja na kuwa na utaratibu mzuri wa kuwakopesha, ili waanzishe miradi ya kujikwamua kiuchumi kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili wananchi wengi nchini kwa sasa.

"Wakati umefika kwa viongozi katika maeneo mbalimbali nchini kubadilika na kuacha tabia na mazoea ya kujinufaisha wao na familia na jamaa zao na kuhakikisha wanajikita zaidi kutumikia wananchi hususan kujali wanakula nini," alisema Lowassa.

Naye Diwani wa Kata hiyo, Manga aliwashukuru wananchi kwa kumchagua na kusema hawakukosea na atawalipa kwa utendaji wake, kwa kujitahidi kutatua kero sugu ambazo
zimekuwa zikiwakabili kwa muda mrefu.

 CHANZO: HABARILEO

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages