KIKWETE: NI MWAKA WA KATIBA MPYA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

KIKWETE: NI MWAKA WA KATIBA MPYA

Raisi Jakaya Mrisho Kikwete

Neville Meena na Fedy Azzah
Rais Jakaya Kikwete ametangaza kuanza mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya. Katika salamu zake za mwaka mpya kwa Taifa jana, Rais Kikwete alisema "...nimeamua kuunda Tume maalum ya Katiba, yaani  Constitutional Review Commission.  Tume hiyo  itakayoongozwa na mwanasheria aliyebobea, itakuwa na wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali katika jamii yetu kutoka pande zetu mbili za Muungano".

Alisema jukumu la msingi la Tume hiyo litakuwa ni kuongoza na kuratibu mchakato utakaowashirikisha wananchi wote vikiwemo vyama vya siasa, wanasiasa, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya dini, wanataaluma na makundi mbalimbali ya watu wote, katika kutoa maoni "wayatakayo kuhusu Katiba ya nchi yao".

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, baada ya kukamilisha kukusanya maoni, Tume itatoa mapendekezo yake yatakayofikishwa kwenye vyombo stahiki vya Kikatiba kwa kufanyiwa maamuzi. "Baada ya makubaliano kufikiwa, taifa letu litapata Katiba mpya kwa siku itakayoamuliwa ianze kutumika,"alisema Rais Kikwete.

Rais alisema lengo la kuandikwa kwa Katiba mpya ni kuiwezesha nchi kuwa na Katiba inayoendana na taifa lenye umri wa nusu karne na kwamba mchakato huo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara na kwamba Katiba inayokusudiwa ni ile itakayolipeleka taifa miaka 50 ijayo kwa salama, amani, umoja na kuwepo  maendeleo makubwa zaidi.

"La nne ambalo tulilokubaliana kufanya ni kuanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya Nchi yetu kwa lengo la kuihuisha ili hatimaye Katiba yetu ya sasa tuliyoachiwa na waasisi wa taifa letu, imeifanyia nchi yetu mambo mengi mazuri na kuifikisha Tanzania na Watanzania hapa tulipo," alisema KIkwete na kuongeza:

".....mwaka 2011, nchi yetu inatimiza miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, miaka 47 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar na miaka 47 ya Muungano wa nchi zetu mbili.  Yapo mabadiliko mengi yaliyotokea katika nyanja mbalimbali za maisha ya nchi yetu na watu wake katika kipindi hiki.  Kwa ajili hiyo ni vyema kuwa na Katiba inayoendana na mabadiliko na matakwa na hali ya sasa". 

Kwa taarifa Zaidi  BOFYA HAPA
Source Mwananchi Newspaper

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages