JUKWAA LA SANAA LAMPA KAZI MH SUGU - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

JUKWAA LA SANAA LAMPA KAZI MH SUGU

 
Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi maarufu kwa Jina la Sugu akiongea na wadau wa Jukwaa la Sanaa mapema wiki hii wakati alipohudhuria kwa mara ya kwanza toka achaguliwe kuwa mbunge. Sugu ni moja ya wadau wa Jukwaa hilo linalofanyika kila Jumatatu Ukumbi wa BASATA.
 
Na Mwandishi Wetu
Jukwaa la Sanaa BASATA limempongeza kwa ushindi wa nafasi ya ubunge na kumpa kazi ya kutetea  wasanii Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye pia ni mmoja ya waasisi wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu.

Akizungumza Kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa BASATA kwa niaba ya wadau wote,Profesa Amandina Lihamba kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye alikuwa ni Mratibu wa Jukwaa hilo alisema kwamba,wadau wa Jukwaa la Sanaa wanampongeza kwa dhati kwa ushindi wake na wanamtuma bungeni kutetea haki zao na kwamba asiwatupe.

“Tunajua toka ushinde leo ni mara yako ya kwanza kuonana na hadhira ya wasanii hivyo tunachukua fursa hii kukupongeza kwa dhati,uendelee na moyo huo huo wa kuwapigania wasanii na usiwatupe” aliongeza Profesa Lihamba.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alisema kwamba, pamoja na BASATA awali kutuma barua ya pongezi kwake na kwa wabunge wengine wasanii bado Jukwaa la Sanaa lina kila sababu ya kumpongeza na kumtuma kwenda kutetea haki za wasanii na kuhakikisha maslahi ya sekta ya sanaa yanalindwa.

“Naomba niungane na wenzangu kutambua uwepo wa Joseph Mbilinyi,Mbunge wa Mbeya Mjini,msanii mwenzetu naimani sasa tunapozungumza hapa katika Jukwaa tunazungumza na mtu ambaye sasa atakuwa bungeni akiwakilisha wasanii.Pamoja na barua ya kumpongeza tuliyomtumia yeye na wasanii wengine walioingia bungeni,tunampongeza tena kwa dhati” alisema Materego.

Naye Mbilinyi aliyeambatana na Katibu wake Fred Maliki maarufu kwa jina la usanii la Mkoloni alimshukuru Materego kwa pongezi zake lakini akapongeza juhudi anazochukua katika kuwahabarisha na kuwapa fursa ya elimu wadau wa sanaa.Aliahidi kuendeleza harakati za kupigania haki za wasanii kwani ndicho kitu ambacho ataanza nacho.

“Harakati za kupigania haki za wasanii nimezianza kwa muda mrefu nawaahidi kwamba sitarudi nyuma na kwa sasa napenda niwaambie kwamba, mapambano ndiyo kwanza yameanza kwani sasa ndiyo tumekabidhiwa rungu” alimalizia Mbilinyi ambaye aliwahi kutamba na nyimbo kama za Mikononi mwa polisi,Deiwaka, Dar moto chini, Wananiita Sugu,Hold  On  na nyingine nyingi.

Awali kabla ya pongezi kwa Mbilinyi kulikuwa na Darasa maridhawa Juu ya tasnia ya filamu nchini lililoendeshwa na timu wa watu wa wanne ambao ni Profesa Amandina Lihamba, Dkt.Mona Mwakalinga kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wasanii Yvone Cherry (Monalisa, Singo Mutambalika (Rich) na Agnes Lukanga,Rais wa Shirikisho la Sanaa za Maonyesho.

Katika darasa hilo la aina yake somo kuhusu  historiia ya filamu hapa nchini lilielezwa na Dkt.Mwakalinga ambapo alisema kwamba ukiacha Afrika Kusini,Tanzania ni ya kwanza barani Afrika kuanza kutengeneza sinema ambapo kwa mara ya kwanza sinema nchini ilitengenezwa mwaka 1935 ambayo ilihusu mafunzo kwa waafrika katika kuwatumikia wakoloni mashambani na zaidi ya nakala 35 zilizalishwa na kusambazwa.

Kwa upande wao, wasanii Monalisa na Rich walisema waziwazi kwamba, kwa sasa tasnia ya filamu inapoteza dira kutokana na kuingiliwa na mdudu wa usambazaji anayejali fedha tu pasipokujali ubora wa filamu bali majina ya washiriki.Walikiri kwamba, filamu zinazotengenezwa zina ubora wa chini na zisizo na maadili hivyo juhudi za makusudi zinahitajika katika kusawazisha hali ya mambo.

Hata hivyo, wadau wengi wa Jukwaa la Sanaa akiwemo Mwalimu Rashid Masimbi waliwapongeza wasanii wa filamu kwa uthubutu wao ambapo walisema kwamba, wameweza kusababisha filamu za kitanzania zizungumziwe na kujadiliwa na huo ni mwanzo mzuri katika kufikia maendeleo ya kweli ya tasnia.

 
Profesa Amandina Lihamba kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichokoza mada kuhusu tasnia ya Filamu hapa nchini kwenye Jukwaa la Sanaa BASATA Jumatatu ya wiki hii.Kulia kwake ni Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego.
 
Kushoto ni Msanii wa Filamu nchini  Yvone Cherry (Monalisa) akizungumzia masuala wanayopambana nayo katika tasnia ya filamu nchini.Alisema kwamba,tatizo kubwa katika filamu ni uwepo wa msambazaji mmoja hali ambayo inanyima fursa kwa wasanii wengi kustawi.
 
Dkt.Mona Mwakalinga akiwaeleza wadau wa Jukwaa la Sanaa historia ya tasnia ya filamu nchini.Kushoto kwake ni Msanii Rich na wengine kutoka kulia kwake ni Msanii Mrisho Mpoto na Katibu wa Shirikisho la Filamu nchini,Wilson Makubi
Makamu wa Rais wa Shirkisho la Muziki nchini ambaye pia ni msanii wa nyimbo za asili,Che Mundugwao akiuliza swali kwenye Jukwaa la Sanaa.
 
Wadau wa Jukwaa la Sanaa wakifuatilia majadiliano.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages