CHADEMA YATOA MASHARTI YA KURUDI BUNGENI - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

CHADEMA YATOA MASHARTI YA KURUDI BUNGENI

Chadema yatoa masharti kurudi bungeni
Mwenyekiti wa chadema , Freeman Mbowe
Kiongozi wa Upinzani bungeni, Freeman Mbowe akiteremka kwenye gari lake la kazi alilopewa na serikali bungeni Dodoma juzi. Picha na Emmanuel Kwitema
----

Imeandikwa na Anastazia Anyimike

ILI waingie bungeni, wabunge wa Chadema wameweka masharti ambayo yakitekelezwa na Serikali watakuwa hawana tatizo tena.



Masharti hayo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ni Serikali kutoa tamko kuhusu hoja yao ya kutungwa Katiba mpya, kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na kutoa msimamo juu ya madai ya kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi mkuu wa hivi karibuni.

Katika mahojiano maalumu na HABARILEO jana, Mbowe alisema: “Matendo ya leo yanaleta matukio ya kesho.

Suala la msimamo wetu kushiriki vikao vya Bunge lijalo utategemea na mapokeo ya hoja zetu.

“Kwa sisi kugomea hotuba ya Rais, tunajua ujumbe wetu umefika kwa wahusika wakiwamo bwana mkubwa mwenyewe (Rais Kikwete), viongozi wa mashirika na taasisi mbalimbali na mabalozi, kuonesha kuwa kuna tatizo la msingi ambalo Chadema inataka lishughulikiwe.

“Tunajua kuna watu wameudhika, na tunajua kuwa hatukumfurahisha Rais, lakini ujumbe wetu umefika.

Kuna baadhi ya watu wamepotosha kuwa tunampinga Rais. Haikuwa nia yetu kutaka avuliwe urais au aondolewe ofisini, tulitaka aone kuwa kuna tatizo ambalo linatakiwa kushughulikiwa na yeye ndiye mhusika.”

Mbowe alisema hoja ya kwanza ya Chadema ni kuona umuhimu wa kuwa na Katiba mpya
itakayoliwezesha Taifa kujenga misingi imara ya demokrasia na kuifanya nchi kuwa na amani, itakayokalika na kila mtu bila kujali kabila, dini au chama chake cha siasa.

“Tunataka Katiba ambayo itamfanya kila Mtanzania aishi kwa amani na upendo, mfano mzuri ni Zanzibar, walikuwa na tatizo kama hilo lakini sasa wamelishughulikia, kwa kuwa na Katiba nzuri na wamekubaliana kuendesha mambo yao … si unaona kila mtu anafurahia hili na wote wanaishi kwa amani kabisa?” alihoji.

Mbowe alisema kilio chao cha pili ni kuundwa kwa Tume ya Uchaguzi iliyo huru ili kufanya uchaguzi ujao usiwe na dosari.

“Ndiyo uchaguzi umekwisha, lakini tunataka Tume ya Uchaguzi iliyo huru, hatutaki kasoro zilizojitokeza uchaguzi huu zijitokeze katika uchaguzi mwingine, hatutaki Tume ambayo mpaka watu waandamane au wakeshe ndipo watangaze matokeo.”

Alisema hoja ya tatu ni kuundwa kwa Tume huru itayochunguza malalamiko yao kuhusu kasoro zilizojitokeza kwenye uchaguzi mkuu na kutoa mapendekezo ya kufanyiwa kazi dosari zitakazokuwa zimebainishwa.

“Tuna madai ya msingi kabisa, na tumetumia njia hiyo ili kufikisha ujumbe wetu kwa kufuata taratibu na tumewasilisha kilio chetu kwa amani kabisa, hatujatukana mtu, lakini baadhi ya watu wanatubeza na wengine wanasema tuundiwe azimio la kufukuzwa bungeni, sijui kama wanaelewa taratibu na kanuni.”

Aliongeza: “Katika vipaumbele 13 vilivyotolewa na Rais, hatujasikia suala la marekebisho ya Katiba ambalo limekuwa likilalamikiwa kwa takribani miaka 15 sasa, na hakuna hatua inayochukuliwa, sasa tunataka haya tunayoyadai yawemo kwenye hivyo vipaumbele.

Alhamisi iliyopita, wabunge wa Chadema waliondoka kwenye ukumbi wa Bunge mara baada ya Rais Kikwete kuanza kuhutubia kwa mara ya kwanza tangu kufanyika uchaguzi mkuu, Oktoba 31.

Akizungumzia madai ya kuwapo mgawanyiko ndani ya Chadema, katika kufikia uamuzi huo wa kususia hotuba ya Rais, Mbowe alisema uamuzi huo ulipitishwa ndani ya kikao cha chama hicho.

“Uamuzi ule umetokana na kikao halali cha chama, katika masuala kama hayo, si lazima watu wote wakubali na ndiyo maana unaweza kufikia hatua ya kupiga kura, lakini mwisho wa yote uamuzi wa wengi ndio unaofuatwa.”

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages