KIKOSI cha Jeshi la Ukombozi la watu wa China leo kitaanza kutoa huduma za afya kwa magonjwa mbalimbali katika vituo vya Lugalo, Kigamboni na bandarini.
Akizungumza na Waandishi wa habari katika meli hiyo ya China yenye sehemu mbalimbali za kutolea huduma za afya, Mkuu wa msafara katika meli hiyo Bao Yuping alisema kuwa meli hiyo itakuwepo jijini kwa siku nne. Yuping alisema kuwa katika kudumisha mahusiano katika nchi ya Tanzania na China wameamua kuja kutoa huduma hizo za afya bure katika vituo hivyo. Alisema kuwa katika msafara huo kuna jumla ya wahudumu 450 ambao kati yao kuna madaktari 56, manesi 26 na wengine ni wahudumu wa afya katika vitengo mbalimbali “Kuna jumla ya wahudumu wa afya 450 madaktari 56, manesi 26 na wengine ni wahudumu katika vitengo vingine na wahudumu hao watatoa huduma kwa kushirikiana na madaktari kutoka Tanzania,” alisema Yuping.
Alisema kuwa meli hiyo ina vifaa na dawa za kutosha na kutoa huduma zake katika vituo hivyo ambapo watakaogundulika na matatizo makubwa watapelekwa kwenye meli iliyoko bandarini kwa ajili ya matibabu zaidi. Alisema watatibu magonjwa yote ikiwa ni pamoja na upasuaji wa ubongo na shingo, mifupa ya fahamu na magonjwa ya ngozi kasoro magonjwa ya meno. Awali Mkuu wa hospitali ya Lugalo, Meja Jenerali Salim Salim alisema kuwa kutokana na uhusiano huu madaktari wa nchini watapata nafasi za kujifunza kutoka kwa madaktari wa China na kuweza kuongeza ukaribu wa nchi hizo mbili.
Aliongeza kuwa meli hiyo imekuja na vifaa vya kisasa na kuwatoa hofu baadhi ya watu katika mawasiliano wakati wa huduma hizo kwani timu hiyo imekuja na wakalimani watakaowezesha kuwasiliana baina ya muhudumu na mgonjwa ambapo itaweka kambi jijini kwa muda wa siku nne hadi Septemba 22.
Imeandaliwa na Mahija Mpera, Aziza Masoud na Hidaya Omary





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)