Lori laua watu watano wanaouza vitu barabarani - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Lori laua watu watano wanaouza vitu barabarani


Joseph Lyimo, Manyara

WAFANYABIASHARA ndogondogo watano wa Kata ya Endasaki wilayani Hanang’ mkoani Manyara wamepoteza maisha na mmoia kujeruhiwa baada ya gari kampuni inayotengeneza  barabara kuacha njia na kuwagonga wakati wakiendelea na biashara zao.

Akidhibitisha kutokea kwa vifo hivyo, Kaimu kamanda wa Polisi,mkoani Manyara,Eurelia Msindai alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 11 jioni katika barabara kuu ya Endasaki-Babati wilayani Hanang’.

Kaimu kamanda ,alisema gari hilo likiwa barabarani liliacha njia na kuwagonga wafanyabiasha hao waliokuwa pembeni mwa barabara hiyo wakifanya biashara ndogondogo.

Alisema ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Stay,ambayo haina namba za usajili mali ya kampuni ya Sinosyoro inayojenga barabara ya Singida-Dareda na ilikuwa inaendeshwa na dereva wa kampuni hiyo (jina linahifadhiwa), mkazi wa mkoani Manyara.

Aliwataja wafanyabiashara wawili waliofariki  papohapo kwenye ajali hiyo ni Polkeria Ugo (45) mkazi wa Dareda wilayani Babati, Maria (35) ambaye alitambulika kwa jina moja na pia mkazi wa Dareda wilayani Babati.

Wengine waliofia kwenye hospitali ya Dareda mission baada ya ajali hiyo ni Safari Tsere (30) mkazi wa Endasaki wilayani Hanang’,Pascalina Gurtu (61) mkazi wa Sabilo wilayani Babati na Said Athumani (60) mkazi wa Endasaki wilayani Hanang’.

Kaimu kamanda Msindai alisema Abeid Lotti (20) mkazi wa Endasaki alijeruhiwa kwenye ajali hiyo baada ya kuvunjika mkono na amelazwa kwenye hospitali ya Dareda mission na hali yake inaendelea vizuri.

Alisema chanzo cha ajali hiyo hakijajulikana ila uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa gari hilo lilikuwa na matatizo ya breki na jeshi hilo linamshikilia dereva wa gari hilo na atafikishwa mahakamani pindi uchunguzi utakapokamilika.

Katika tukio lingine mzee mwenye umri wa miaka 70, Hadii Maida mkazi wa Bashai wilayani Mbulu amefariki dunia baada ya kupigwa na fimbo kichwani.

Kaimu kamanda Msindai alisema tukio hilo lilitokea juzi jioni katika kijiji cha Mulvadawi wilayani Hanang’.

Alisema mzee huyo alipigwa fimbo ya kichwa na mwalimu wa shule ya msingi Mulvadawi wilayani Hanang’  ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.

Kaimu kamanda Msindai alisema chanzo kilichosababisha kifo hicho hakijajulikana na jeshi hilo linamshikilia mwalimu huyo na anatarajiwa kufikishwa mahakamani pindi uchunguzi wa tukio hilo utakapokamilika.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages