LIGI KUU BARA YAANZA TENA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

LIGI KUU BARA YAANZA TENA

BAADA ya kusimama kwa muda wa wiki moja kupisha mchezo wa timu ya taifa Taifa Stars dhidi ya Morocco Ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaendelea leo kwa michezo miwili kati ya Azam FC dhidi ya Majimaji ya Songea na Ruvu Shooting kukwaana na AFC ya Arusha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.

 Azam FC iliwasili Songea na wachezaji 18 na viongozi huku ikiongeza nguvu kwenye kikosi chake na wachezaji wake watatu waliokuwa majeruhi Ibrahim mwaipopo, Ibrahim Shikanda na Kally Ongala aliyekuwa akisumbuliwa na malaria.

Akizungumza na Mwananchi jana kwenye ofisi za timu hiyo zilizopo jijini Dar es salaam katibu mkuu wa Azam FC Nassor Idrissa alisema kuwa anategemea timu yake kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Majimaji ya Songea.

Alisema wao kama  Azam FC bado hawajakata tamaa ya kuwa mabingwa wapya wa Ligi kuu ya Vodacom licha ya kupoteza michezo mitatu ya Ligi hiyo kati ya Simba mabao 2-1, Kagera Sugar bao 1-0 na Toto African ya Mwanza kwa bao 1-0.

Kwa upande wa Majimaji kupitia kocha wao Peter Mhina, aliliambia Mwananchi kwa simu kuwa wanaifahamu Azam kuwa ni timu nzuri na wamejizatiti kukabiliana nao kwa kila hali ili kuhakikisha wanaibuka na pointi zote tatu na kujiweka katika nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa Ligi kuu.

Mchezo mwingine utazikutanisha timu zinashikilia mkia kwenye Ligi hiyo AFC ya Arusha dhidi ya Ruvu Shooting mchezo utakofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

AFC itabidi kupiga kufa na kupona ili kuhakikisha inashinda mchezo huo na kuanza kujiondoka kwenye hatari ya kurudi Ligi daraja la kwanza kwani ndiyo timu inayoshikilia mkia kwenye Ligi hiyo ikiwa imecheza michezo sita na kupoteza michezo mitano na kushinda mmoja dhidi ya JKT Ruvu kwa mabao 3-2 na ina pointi tatu.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages