Mbunge wa Jimbo la Ubungho(CHADEMA)mheshimiwa John Mnyika
---
Juzi
jumapili tarehe 6 Mei 2012 nimekabidhi zaidi ya vitabu mia saba (700)
kama ishara ya kuanzisha Programu ya Taarifa iitwayo “Toa Kitabu
Kisomwe”, hii ni miezi mitatu baada ya kusambaza kwa wananchi wa jimbo
la Ubungo vitabu 4500 ikiwa ni pamoja na nakala za katiba ya nchi na
vitabu kuhusu mchakato wa katiba mpya; na kufanya jumla ya vitabu
ambavyo nimesambaza mpaka sasa kuwa zaidi ya elfu tano (5,000).
Lengo ya Programu ya Taarifa ya “Toa Kitabu Kisomwe” ni kusambaza jumla
ya vitabu visivyopungua elfu hamsini (50,000) ndani ya Manispaa ya
Kinondoni katika kipindi cha mwaka ili kuchochea uhuru wa kifikra na
kuchangia katika ustawi wa wananchi.
Kwa mtazamo wangu akili na vipaji ambavyo kila mwanadamu amejaliwa
ndiyo mtaji mkuu wa kujikwamua kimaisha. Hivyo kushirikiana kuwezesha
elimu bora na uhuru wa kifikra ni msingi muhimu wa kuchochea maendeleo
ya wananchi na nchi kwa ujumla.
Elimu bora sio majengo pekee bali ni pamoja na walimu bora na mazingira
bora ya kusomea na kujifunzia yenye vifaa vya kujifunzia na vitabu vya
kiada na ziada.
Hivyo, harakati za kusimamia uwajibikaji wa serikali kuu, serikali za
mitaa na mamlaka nyingine zinazohusika na sekta ya elimu hususani kwenye
shule, vyuo na vyuo vikuu vya umma zinapaswa kuendelezwa.
Tuendelee kuhakikisha rasilimali zinazotengwa ikiwemo ruzuku ya elimu
ya msingi na sekondari na mikopo ya elimu ya juu zinakuwa za kutosha,
zinatolewa kwa wakati na zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa kwa
kudhibiti mianya ya ufisadi.
Wakati, tukisimamia uwajibikaji huo wa serikali tutambue masuala matatu
muhimu; mosi, jukumu la kuboresha mazingira ya elimu kwenye elimu
rasmi ya darasani sio wa serikali pekee bali ni wajibu wa wote katika
jamii.
Pili, izingatiwe kuwa sehemu kubwa ya wananchi hawajapata elimu rasmi
hivyo ni muhimu kuwa na mifumo ya elimu kwa njia nyingine mitaani na
vijijini ili kuchochea zaidi maendeleo.
Tatu, hata kwa wenye elimu rasmi inafahamika kuwa elimu haina mwisho
hivyo kila mmoja ana wajibu wa kujisomea ili kuendeleza uhuru wa
kifikra.
Katika muktadha wa masuala hayo matatu, niliungana na Asasi ya
Maendeleo Ubungo (Ubungo Development Initiative-UDI) kuzindua Programu
ya Taarifa inayohusisha kukusanya vitabu vya kiada na vya ziada kutoka
wa watu mbalimbali na taasisi mbalimbali na kuvisambaza katika taasisi
za elimu kwa ajili ya wanafunzi kusoma na maeneo maalumu kwa ajili ya
wananchi kujisomea.
Mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema kwamba ukimpa mtu samaki umemlisha
kwa siku moja lakini ukimfundisha kuvua umemlisha kwa maisha yake yote.
Nikisisitiza mantiki ya msemo huo naweza kusema pia kwamba ukimpa mtu
chakula cha kawaida umemshibisha kwa muda mfupi lakini ukimpa chakula
cha kifikra umemuwezesha kwa muda mrefu; huu ndio msingi utakaoongoza
Programu ya Taarifa; “Toa kitabu kisomwe”.
Kupitia programu hii tunaomba taasisi au mwananchi yoyote mwenye kitabu
chochote popote ambaye yuko tayari kukitoa ili kisomwe iwe ni cha
kiada au cha ziada awasiliane UDI ili iweze kufikisha kitabu hicho kwa
walengwa.
Ukipenda unaweza kuweka saini kwenye kitabu hicho kama kumbukumbu kuwa
taasisi yenu au wewe ndiye uliye “Toa kitabu Kisomwe” au unaweza pia
kutueleza kitabu hicho unapendekezwa kipelekwe wapi ndani ya Manispaa ya
Kinondoni ili kiweze kusomwa kwa ufanisi.
Sisi mpango wetu ni kusambaza vitabu hivyo kwenye maktaba za shule za
msingi, sekondari na vyuo vikuu kwa upande wa elimu ya kiada na
kusambaza kwenye maktaba za jumuia, ofisi za serikali za mtaa, taasisi
za kijamii na vijiwe vya kudumu kwa upande wa elimu ya ziada.
Naamini kwamba kwenye kaya mbalimbali za Manispaa ya Kinondoni vipo
vitabu makabatini au masandukuni ambavyo ama ni vya kiada vilivyoachwa
baada ya walengwa wa awali kupanda ngazi moja ya elimu kutoka ile ambayo
walikuwa wakisoma au ni vya ziada ambavyo tayari wahusika
walishavitumia na vinaweza kuwa na mchango mkubwa kwa walengwa wengine
wenye kuvihitaji hivyo; “Toa Kitabu Kisomwe'' Kwa habari zaidi Mtembelea
Mbunge wa Ubungo(CHADEMA)Mh, John Mnyika kupitia
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)