Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa pamoja na
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya biashara ya Kenya KCB Bw. Moez Mir,
wakati ujumbe wa benki hiyo ulipofika ofisini kwake Migombani kwa ajili
ya kubadilishana mawazo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa benki ya biashara ya Kenya KCB Bw. Moez Mir, akitoa
ufanunuzi kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif
Hamad juu ya namna benki yake inavyoweza kushirikiana na Zanzibar
katika kusaidia huduma za kijamii, wakati ujumbe wa benki hiyo
ulipofika ofisini kwake Migombani kwa ajili ya kubadilishana mawazo.
Kulia ni mkurugenzi wa biashara wa benki hiyo Respige Kimath
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika
picha ya pamoja na ujumbe wa benki ya biashara ya Kenya KCB wakati
ujumbe huo ulipomtembelea ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar.
Kuliani kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Bw. Moez Mir
akifuatiwa na meneja biashara tawi la Zanzibar Bw. Abdul Mshangama.Picha
na Salmin Said Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
---
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameiomba benki
ya maendeleo ya Kenya KCB kuangalia uwezekano wa kusaidia sekta ya
michezo Zanzibar ili kurejesha hadhi ya michezo nchini.
Amesema
serikali ina nia thabiti ya kurejesha hadhi ya michezo Zanzibar na
kufufua michezo ya asili ikiwemo ya ndani (Indoor games), lakini
imekuwa ikikwazwa na ufadhili mdogo katika michezo mbali mbali ukiwemo
mchezo wa soka.
Maalim
Seif ametoa changamoto hiyo huko ofisini kwake Migombani alipokuwa na
mazungumzo na ujumbe wa benki hiyo ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji
Moez Mir.
Amesema
serikali inajipanga kwa ajili ya kujenga uwanja wa michezo ya ndani,
na kwamba iwapo lengo hilo litafanikiwa hadhi ya michezo Zanzibar
inaweza kurejea katika hali yake ya awali ambapo ilikuwa ikisifikana
kwa michezo mbali mbali ikiwemo table tennis na golf.
Amefahamisha
kuwa miongoni mwa matatizo yanayokwaza sekta ya michezo kwa sasa ni
upungufu wa viwanja vya michezo hasa ya ndani, pamoja na kuendeleza
vipaji vya vijana vinavyoibuliwa kutoka maskulini na maeneo mengine ya
michezo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo bw. Moez Mir amesema
benki yake inalichukua wazo hilo na kulifanyika kazi sambamba na
kuwasiliana na wadau wengine wa michezo ili kuona namna ya kuleta
ufadhili wa michezo mbali mbali na kuinua hadhi ya michezo Zanzibar.
Amesema
kitu cha msingi ni mashirikiano katika sekta hiyo, na kwamba benki
yake pia inalizingatia suala hilo akielezea matarajio yake kuwa
linaweza kutatuliwa kwa mashirikiano baina ya serikali na wadau
wengine.
Wakati
huo huo Bw. MIR amesema benki yake iko tayari kushirikiana na Zanzibar
katika jitihada zake za kukabiliana cha changamoto inazozikakabili
ikiwemo dawa za kulevya, watu wenye ulemavu na uchafuzi wa mazingira.
Amesema
benki yake ambayo imekuwa ikiunga mkono shughuli za kijamii hasa
katika sekta za elimu na mazingira, itaendelea na jitihada hizo na
kuongeza maeneo mengine ya kusaidia ili kuhakikisha kuwa maendeleo ya
kijamii yanaimarika Zanzibar.
Nae
Makamu wa Kwanza wa Rais ameipongeza benki hiyo kwa mwamko wake wa
kusaidia huduma za kijamii zikiwemo elimu, na kuiomba kuangalia
uwezekano wa kuangalia maeneo mengine ya kusaidia yakiwemo mapambano
dhidi ya dawa za kulevya na masuala ya watu wenye ulemavu.
Maalim
Seif amesema Zanzibar inafarajika kuona taasisi za fedha ikiwemo benki
ya KCB zinashirikiana na serikali katika kusaidia kutatua kero
zinazowakabili wananchi, na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa
taasisi hizo, ili ziweze kuendesha shughuli zake kwa ufanisi zaidi.
Mapema
meneja wa biashara wa benki hiyo tawi la Zanzibar Bw. Abdul Mshangama,
ameiomba serikali kuzitumia kikamilifu fursa zinazotolewa na benki
hiyo ili iweze kunufaika na fursa hizo ambazo zitasaidia maendeleo ya
wananchi na taifa kwa jumla.
Na
Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)