Wadau wa usafiri jijini Mwanza wakifuatilia mada wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Usinywe na Kuendesha inayofanywa na kampuni ya Bia ya Serengeti.
Mwanza, Januari 25, 2019-Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) imezindua kampeni inayolenga kutoa elimu kwa umma juu ya unywaji wa kistaarabu, ikiwa ni moja ya hatua muhimu inayochukuliwa na kampuni hiyo kuzuia ajali nyingi zinazosababishwa na madereva wanaoendesha wakiwa wametumia vilevi
Kampeni hiyo inayobeba ujumbe wa, “Usitumie Kilevi na Kuendesha Chombo cha Moto’ imezinduliwa jijini Mwanza leo na ilianza na kongamano lililojadili unywaji wa kistaarabu ambalo liliwaleta pamoja wadau kama vile Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani, Mamlakka ya Usafirishaji wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), madereva, abiria, na wadau wengine katika sekta ya usafirishaji
Akiongea wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika katika hoteli ya Gold Crest, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani (RTO) mkoani Mwanza Mkaddam Hamis Mkaddam, alisema kwa kulishirikisha jeshi la Polisi kampuni ya SBL imeiunga mkono serikali katika kuelimisha umma juu ya unywaji wa kistaarabu na kusisitiza umuhimu wa kutatua tatizo hilo.
Mkaddam alisema baadhi ya watu na haswa madereva hunywa kiasi kikubwa cha pombe pasipo kujali madhara yanayoweza kusababishwa na kitendo hicho na kuonya kuwa vitendo vya aina hiyo vinaweza kusababisha ajali mbaya.
“Sote tunafahamu kuwa matumizi ya vileo yana uhusiano mkubwa na uendeshaji mmbovu ambao unaweza husababisha ajali mbaya za barabarani zenye athari kubwa kwa jamii zetu. Athari zake siyo tu zinawagusa watumiaji wa vilevi bali hata maisha ya wengine na kusababisha upotevu wa maisha na ulemavu kwa watu ambao wangeweza kuchangia uchumi wa nchi,” alisema Mkaddam.
Alisema pamoja na kusababisha vifo visivyotarajiwa na majeraha, unywaji usiokuwa wa kistaarabu una maadhara makubwa kwenye sekta ya afya kwa kuwa kiasi kikubwa cha fedha kinatumika kwa ajili ya huduma, madawa na vifaa tiba kwa waathirika wa ajali za barabarani na hivyo kuwa ni mzigo kwa Serikali.
“Ajali hizi pia ni mzigo kwa vyombo vyetu vya utekelezaji wa sheria kwa kuwa maofisa wanalazimika kuzishughulikia wakati zinaweza kuzuilika ambazo zinasabishwa na madereva wanaondesha wakiwa wametumia vilevi,” Mkaddam aliongeza.
Akizungumzia namna kampeni hiyo itaisadia jamii, mkuu huyo wa usalama barabarani alisema, “sote kwa pamoja ikiwamo sisi polisi, madereva, jamii na wadau wengine tuna jumuku la kutafuta suluhisho la kumaliza tatizo la kutumia vilevi na kuendesha vyombo vya moto. Ninayo furaha kuona SBL pamoja na kwamba biashara yao ni kuuza vilevi, wameona wanawajibu wa kuhimiza unywaji wa kistarabu”.
Kampeni hii inalenga kuwafikia vijana na watu wengine na kuwaeliisha juu ya madhara ya unywaji usiokuwa wa kistaarabu huku ikiwataka kubadili tabia kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla
Akiongea wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa SBL John Wanyancha alisema kampeni ya unywaji wea kistaarabu inalenga kuielimisha jamii kuwa wanywaji wanapaswa kunywa kwa kiasi na kuhakikisha unywaji wao hauna madhara kwao na kwa watu wanaowazunguka.
“SBL imedhamiria kuungana na serikali na wadau wengine kuhakikisha kuwa jamii na haswa madereva ambao wanakunywa na kuendesha vyombo vya moto wanaelimishwa juu ya madhara ya vitendo hivyo na kutakiwa kubadilisha tabia,” alisema Wanyancha.
|
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)