Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja kutoka benki ya NMB, Omary Mtiga (kulia) akizungumza katika tukio hilo. |
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Anastazia Mabula amezitaka taasisi za fedha pamoja na waendelezaji milki binafsi kushirikiana na Serikali ili kutatua changamoto iliyopo ya uhaba wa nyumba na makazi nchini.
Akihutubia katika ufunguzi wa maonyesho ya nyumba yaliyoandaliwa na benki ya NMB jana na kufanyika katika viwanja vya Kambarage jijini Dodoma, Mabula amesema serikali inauhaba wa nyumba za watumishi hususani baada ya serikali kuhamia jijini Dodoma.
Amesemakuwa Tanzania inaupungufu wa nyumba 3,000,000, hivyo ili kutatua changamoto hiyo, kunatakiwa kujenga nyumba zaidi ya laki mbili kila mwaka hivyo hawana budi kuwashirikisha wadau kikamilifu kama benki ya NMB ilikuziba pengo hilo.
Akizungumzia upande wa Dodoma, Mabula amesema mahitaji ni kuwa na nyumba zaidi ya elfu 23 lakini zilizopo ni nyumba 1329 tuhivyo maonyesho hayo yaliyowakutanisha wateja wa benki ya NMB, waendelezaji milki pamoja na wauzaji wa vifaa vya ujenzi yana tija kubwa kwani yanalenga kuiunga mkono serikali katika suala la maendeleo.
“Makazi bora ni haki ya kila mwananchi, na tukiri kuwa tuna changamoto ya uhaba wa nyumba nchini, lakini kupitia maonyesho haya tunaweza kukutana na wadau mbalimbali kama vile taasisi za fedha waendelezaji miliki na pia wauzaji wa vifaavya ujenzi ili kumaliza changamoto hiyo,” Alisema Mabula.
Amesema Serikali imeshaweka mazingira wezeshi yanayoruhusu taasisi za serikali pamoja na waendelezaji milki binafsi kushiriki katika kuzalisha nyumba ambazo wananchi wanaweza kununua kupitia mikopo inayotolewa na benki za biashara hivyo kuzitaka benki hizo kutoa mikopo kwa riba nafuu ambayo hata mwananchi wa kipato cha chini ataweza kuimudu.
“Taasisi za fedha ziangalie viwango vya riba, tusiwaumize wananchi, lakini kwa upande wa wadau wengine naomba msogeze huduma zetu karibu na jamii, sambamba na kujenga nyumba kwa kuzingatia mahitaji ya walaji, kuna wa chini, wa kati na wa juu, wote muwape huduma kulingana na halizao,” Alisisita Waziri huyo.
Naye Meneja wa NMB Kanda ya Kati - Nsolo Mlozi amesema lengo la maonyesho hayo ya sikumbili ni kuwakutanisha wateja wa benki hiyo pamoja wadau mbalimbali wa nyumba ili kuweza kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba na makazi iliyopo kwa sasa kwa kuzingatia kuwa sekta hiyo inakuwa kwa kasi.
“NMB tumeona hii ni nafasi ya kuhakikisha tuna uwezo wa kuwapa mikopo wateja lakini pia tuwalete karibu na wauzaji wabidhaa mbalimbali kwenye sekta hii ili wateja waweze kuona na kulinganisha,…hii ni katika ushindani wa kibiashara ili wateja waweze kupata kitu bora,” Alisema Mlozi.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja kutoka benki ya NMB, Omary Mtiga amewataka wateja wa benki hiyo kutumia fursa hiyo kwani wanatoa mikopo rahisi na yenye masharti nafuu na muda wa kurejesha ni mrefu.
Amesema tayari wameshatoa mkopo wa zaidi ya shilingi Bilioni 13 nchi nzima, na kwa mkoa wa Dodoma wametoa mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 700 na wanaendelea kutoa mikopo hiyo ili kuiunga mkono serikali katika azma yakustawisha makao makuu ya Serikali.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)