NMB YADHAMINI TANZANIA TOP 100 MID-SIZED COMPANIES AWARDS KWA USD 50,000 - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

NMB YADHAMINI TANZANIA TOP 100 MID-SIZED COMPANIES AWARDS KWA USD 50,000

Mkuu wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya NMB, Abdulmajid Nsekela (katikati) akizungumza katika hafla ya uzinduzi msimu mpya wa 'Tanzania Top 100 Mid-Sized Companies Awards,’ iliyofanyika makao makuu ya Benki ya NMB jijini Dar es Salaam.

Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Bakari Machumu (wa kwanza kulia) akizungumza katika hafla ya uzinduzi msimu mpya wa 'Tanzania Top 100 Mid-Sized Companies Awards,’ iliyofanyika makao makuu ya Benki ya NMB jijini Dar es Salaam.

MSIMU wa nane wa Tuzo za Wafanyabiashara/Kampuni 100 Bora nchini ‘Tanzania Top 100 Mid-Sized Companies Awards,’ umezinduliwa jijini Dar es Salaam, huku Benki ya NMB ikisaini mkataba wa udhamini wenye thamani ya Dola za Marekani 50,000.

Uzinduzi huo umefanyika mchana, Makao Makuu ya NMB, ambako mwakilishi wa Kampuni ya KPMG, inayoratibu tuzo hizo, Ketan Shah, alisema pamoja na mambo mengine, Tuzo za Kampuni 100 Bora, zinalenga kutambua mafanikio na kuthamini mchango wa wafanyabiashara
nchini.

Shah amesema wanafurahi kuona Benki ya NMB ikikubali kudhamini tuzo hizo, ambazo hutumika kuwapa wafanyabiashara, wajasiriamali na makampuni, mbinu za mafanikio kutoka kwa waliofanikiwa zaidi, ikiwa ni pamoja na kuonyesha njia za kuongeza thamani ya bidhaa zao.

Amezitaja baadhi ya sifa kuu za kushiriki shindano hilo kuwa ni pamoja na Kampuni ama mfanyabiashara kuwa na pato linaloanzia Sh. Bilioni 1 hadi 20 kwa mwaka na kuwa na hati safi za ukaguzi wa mahesabu ya kampuni kwa miaka mitatu iliyopita.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wateja Wadogo na wa Kati wa NMB, Abdulmajid Nsekela, amesema benki ya NMB ina furaha kuwa sehemu ya shindano hilo, linaloratibiwa na KPMG, aliowataja kama wabobezi katika masuala ya utaalamu na ushauri chanya wa kibiashara.

Ameongeza ya kwamba, kwa miaka nane, KPMG imekuwa ikiratibu kwa mafanikio tuzo hizo, ambako wamekuwa wakifanya uchunguzi wa huduma mbalimbali za kibiashara na kuchangia ustawi, maendeleo na mafanikio ya kampuni shiriki na taifa kwa ujumla.

“Leo hii NMB tunapiga hatua kubwa zaidi kwa kuingia ubia na KPMG, ambao wanatarajia kufanya utafiti yakinifu na wa kina, ili kuwapata wafanyabiashara 100 bora nchini. Tunaamini kupitia mchakato huu itatoa fursa kwa washiriki hao kunufaika na huduma zetu,” alisema.

Ukiondoa NMB, wadhamini wenza wa tuzo hizo, ambazo pia hufanyika katika nchi za Kenya na Rwanda kwa miaka 10 sasa, ni pamoja na Kampuni ya Azam Media Ltd, Mwananchi Communication Ltd, Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na Hyatty Regency.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages