Mwekezaji katika klabu ya Simba, Mohammed Dewji anapenda kutoa taarifa kuwa ameanzisha tuzo ambazo zitakuwa zikitolewa kwa wachezaji, viongozi na mashabiki wa klabu ya Simba ambazo amezipa jina la Mo Simba Awards.
Kwa mara ya kwanza tuzo hizi zitatolewa siku ya Jumatatu, tarehe 11 Juni, 2018 katika hoteli ya Hyatt Regency – Kilimanjaro iliyopo Jijini Dar es Salaam.
Tuzo hizo zitakuwa na vipengele 16, ambavyo ni Mchezaji Bora wa Mwaka, Goli Bora la Mwaka, Golikipa Bora wa Mwaka, Beki Bora wa Mwaka, Kiungo Bora wa Mwaka, Mshambuliaji Bora wa Mwaka, Shabiki Bora wa Mwaka na Tuzo ya Heshima.
Tuzo zingine ni Mchezaji Bora Mwanamke wa Mwaka, Mchezaji Bora Mdogo wa Mwaka, Tuzo ya Benchi la Ufundi, Kiongozi Bora wa Mwaka, Tuzo ya Wasimamizi wa Mchakato wa Mabadiliko, Mhamasishaji Bora wa Mwaka katika Mitandao ya Kijamii, Mhamasishaji Bora wa Mwaka na Tawi Bora la Mwaka.
Washindi wa tuzo hizo watatokana na kura ambazo zitapigwa na mashabiki kupitia mitandao ya kijamii na tovuti ya mosimbaawards.co.tz na kamati maalumu ya tuzo ambayo itahusisha wadau mbalimbali wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.
Akizungumza kuhusu tuzo hizo, Dewji amesema ameanzisha tuzo hizo kwa lengo la kutambua mchango wa wachezaji, viongozi na mashabiki ambao juhudi zao zimeiwezesha Simba SC kupata mafanikio iliyonayo sasa.
Dewji amesema tuzo hizo ni sehemu ya mikakati yake ya kuifanya klabu ya Simba kuwa timu kubwa barani Afrika, ambayo itakuwa na uwezo wa kifedha ambao utaiwezesha kuwa na wachezaji na benchi la ufundi bora ambalo litaiwezesha kushinda mataji makubwa.
“Simba ni timu kubwa inastahili kuwa na tuzo zake ambazo zitakuwa zinatolewa kwa kutambua mchango wa wenzetu ambao umetuwezesha kupata mafanikio haya ikiwepo kushinda taji la Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Ni jambo ambalo litawatia moyo kuendelea kujituma lakini hata kwa ambao watakosa itawatia hamasa na hivyo kuongeza juhudi,” amesema Dewji.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo itakuwa mbashara kupitia Azam.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)