Pages

Kamati ya Bunge yakoshwa na utendaji wa Benki ya NMB

NMB%2Bvs%2BKamti%2B5
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB - Ineke Bussemaker akizungumza katika kikao baina ya uongozi wa benki hiyo na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kilichofanyika Bungeni, jijini Dodoma Juzi. Na Mpigapicha Wetu


NMB%2Bvs%2BKamati%2B2
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB - Ineke Bussemaker akizungumza katika kikao baina ya uongozi wa benki hiyo na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kilichofanyika Bungeni, jijini Dodoma Juzi. Na Mpigapicha Wetu


NMB%2Bvs%2BKamati%2B6
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ineke Bussemaker akizungumza katika kikao baina ya uongozi wa benki hiyo na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kilichofanyika Bungeni, jijini Dodoma Juzi. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Raphael Chegeni. Na Mpigapicha Wetu 

·        Faida ya NMB ya Shilingi billion 93.5 ni sawa na theluthi moja ya jumla ya faida ya mwaka ya benki zote nchini
·        Wabunge wapendezwa na mpango wa kuongeza mikopo kwa sekta ya kilimo

KAMATI ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma imeelezea kufurahishwa kwake na utendaji wa Benki ya NMB na kuahidi kufanya kazi pamoja na taasisi hiyo ya fedha ili kuendeleza uchumi wa nchi.

Akizungumza katika chumba cha mikutano kilichopo ndani ya Ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni muda mfupi baada ya kuhudhuria semina iliyoandaliwa na NMB, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Raphael Chegeni alisema taarifa zinaonyesha benki hiyo imefanya vizuri katika nyanja zote.

“Kamati imefurahishwa na utendaji wa NMB na tumewataka waendelee kuwa wabunifu na kuboresha zaidi huduma kwa wananchi. Tumewataka waangalie zaidi sekta ya kilimo ambayo kwa mwaka jana ilipata asilimia tatu (3) tu ya mikopo yote iliyotolewa na benki za biashara kwa sekta mbali mbali za uzalishaji mali nchini,” alisema Dk Chegeni.

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa NMB kwa Kamati hiyo ya Bunge inaonyesha kuwa idadi ya wateja wa benki iliongezeka kwa asilimia 24 kutoka milioni 2.179 kwa mwaka 2016 na kufika milioni 2.7 mwaka jana.

Idadi ya mashine za kutolea fedha (ATMs) ziliongezeka kutoka 670 mwaka 2016 na kufika 770 mwaka jana huku idadi ya matawi yakiongezeka kutoka 188 na kufika 212 mwaka jana kabla ya kufika 220 hivi sasa.

Benki ya NMB pia imefanikiwa kuongeza idadi ya mawakala wake (NMB Wakalas) kutoka 785 mwaka 2016 na kufika karibu 4000 mwaka jana kabla ya kuongeza zaidi kufika 6000 hivi sasa.

Thamani ya mali za benki iliongezeka kwa asilimia 11 kutoka Shilingi trililioni 4.95 mwaka 2016 na kufika Shilingi trilioni 5.5 mwaka jana huku amana za wateja zikipanda kwa asilimia 14.

Mwaka jana, NMB ilipata faida ya baada ya kodi ya Shilingi bilioni 93.5 ambayo ni sawa na theluthi moja ya faida ya benki zote za biashara nchini kwa pamoja (NMB ikiwemo) ambayo ilikuwa jumla ya Shilingi bilioni 286.

Kutokana na faida hiyo, NMB imetoa gawio la jumla ya Shilingi bilioni 32 kwa wanahisa ambapo serikali – ambayo inamiliki asilimia 31.8 ya hisa za NMB – imepata mgao wa Shilingi bilioni 10.17.

Akizungumza baada ya Dk Chegeni, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Bi Ineke Bussemaker, alisema mazungumzo kati uongozi wa benki yake na Kamati ya Bunge yalikuwa mazuri na kuahidi kuyafanyia kazi mambo mengi yaliyopendekezwa na watunga sheria hao.

“Tumepokea ushauri mzuri sana kuhusu ni maeneo gani Wabunge wangetaka tupeleke nguvu zetu zaidi…Tukitilia mkazo katika kilimo tutaweza kuwafikia wakulima wengi zaidi nchini kote,” alisema Bi Bussemaker.

Mbali na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, wengine waliohudhuria semina hiyo ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Bi. Hawa Ghasia na makamu wake Bw. Jitu Soni.

Wengine ni: Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali, Bi. Naghenjwa Kaboyoka, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria Ndogo, Bw. Andrew Chenge na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Bw. Peter Serukamba.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)