Pages

UMMY MWALIMU – SERIKALI IMETENGA BILION TATU (3) KWA AJILI YA KUDHIBITI UKIMWI NCHINI


  Mkurugenzi wa mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) Bw. Richard Jordison, akisoma hotuba kwenye hafla ya uzinduzi wa Kili Challenge 2018, iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro iliyopo jijini Dar es salaam mapema mwishoni wa wiki iliyopita.
  Balozi wa GGM, Msanii Mrisho Mpoto akitumbuiza kwenye hafla ya uzinduzi wa Kili Challenge, iliyofanyika hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro iliyoko jijini Dar es salaam mapema mwishoni wa wiki iliyopita.


 Mheshimiwa waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Abel & Fernandes Communcations, Ms. Fatma Fernandes wa pili kutoka kulia, ambaye alinunua picha ya makamu wa Raisi Mheshimiwa Samia Suluhu katika mnada uliofanyika wakati wa uzinduzi wa Kili Challenge ili kukusanya fedha za kupambana na UKIMWI, jijini Dar es salaam mapema mwishoni wa wiki iliyopita.


Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, akikabidhi hundi yenye thamani ya shilingi milioni mia moja (100M) kwa watoto wa kituo cha moyo wa huruma kilichopo Geita ili kusaidia mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa TACAIDS, Dkt.Leornard Maboko, Mkurugenzi wa GGM, Bw. Richard Jordison na kulia, Mkurugenzi wa kituo cha Moyo wa Huruma Sister Adalbera Mukure.
 Mkurugenzi wa Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dkt. Leornard Maboko akisoma hotuba kwenye hafla ya uzinduzi wa Kili Challenge, katika hotel ya Hyatt Regency Kilimanjaro iliyoko jijini Dar es salaam.
    Mheshimiwa waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Ummy Mwalimu akishiriki katika harambe iliyofanyika kwenye uzinduzi wa Kilimanjaro Challenge ili kuchangia mfuko kwa ajili ya kudhibiti UKIMWI nchini.
  Makamu raisi wa GGM, Bw. Simon Shayo akizungumza katika uzinduzi wa Kilimanjaro Challenge ya mwaka 2018, jijini Dar es salaam mapema mwishoni wa wiki iliyopita.
Dar es salaam: Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa kushirikiana na Tume ya kuthibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) ilizindua zoezi la upandaji wa mlima Kilimanjaro (Kili Challenge 2018), na kuendesha harambee ya kuchangisha fedha kwa mwaka 2018 kwa ajili ya afua za UKIMWI nchini.  Shughuli hii ilifanyika tarehe 4 Mei 2018 mwaka huu katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Ummy Mwalimu, aliitikia wito wa kufika Dar es salaam, katika hafla ya uzinduzi wa Kili Challenge 2018, ambapo alifanya zozezi la ugawaji wa fedha zilizokusanywa mwaka mwaka jana 2017 zilizopatikana baada ya wadau mbalimbali kupanda na  kuendesha baiskeli kwa kuzunguzuka Mlima Kilimanjaro.



Kili Challenge ni mfuko unachangia juhudi za serikali  katika mapambano dhidi ya UKIMWI na kutoa elimu kwa jamii kuhusu maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU). Kili Challenge ni mfuko muhimu unaoshirikiana na taasisi za nje na ndani ya nchi katika kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI kwa jamii ya Kitanzania na Dunia kwa ujumla ili kuwapa matumaini ya kuhakikisha jamii inabaki bila kuathiriwa na VVU/UKIMWI katika miaka ijayo.



Mfuko huo pia unalenga kuisaidia Serikali kukabiliana na VVU//UKIMWI sambamba na kutoa nafasi kwa watalii wa ndani na nje kuupanda mlima Kilimanjaro. Uzinduzi huo ulishirikisha Tume ya kuthibiti UKIMWI, Tanzania TACAIDS, na mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) ambapo zaidi ya shilingi bilioni moja (1) zilikusanywa katika tukio hilo.



Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, ameitaka serikali kutumia mbinu mbalimbali na kuweka mikakati itayohakikisha fedha zinazotwengwa kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI zinatumika kwa kusudi hilo, na hivyo kuondokana na kutegemea misaada kutoka kwa wafadhili.



Mheshimiwa Ummy Mwalimu alisema fedha zilizopatikana kwenye harambee hiyo zinatakiwa zielekezwe moja kwa moja kwa wahusika na sio kutumika kama posho za vikao, huku zikionyesha jitihada zilizofanywa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu, pia akiendelea kusema, fedha hizo zinatakiwa kuisaidia nchi katika kuzipa nguvu sekta ndogo ili kuthibiti maambukizi ya UKIMWI nchini.
Katika harambee iliyofanyika wakati wa uzinduzi wa Kili Challenge Mheshimiwa Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, alisema harambee hiyo iliyoandaliwa ili kudhibiti UKIMWI, ni muhimu kwa lengo maalumu ili kuacha kuwa tegemezi wa misaada, huku akiendelea kusema serikali imetakiwa kuwa na ubunifu, kama kweli imedhamiria katika mapambano haya, na kusema moja ya mbinu ni kwa kushirikiana kwa ukaribu na sekta binafsi ili kutafuta namna ya kupambana na UKIMWI.
Aidha Mhe. Ummy Mwalimu aliwaomba wadau kuweka mbele moyo wa kujitolea na kuchangia mfuko wa Kili Challenge kwa manufaa ya wananchi. Alisema wahenga walisema  kutoa ni moyo na si utajiri. Kwa upande wa Serikali, tayari tumetenga fedha Bilioni tatu (3 bilioni) kwenye bajeti ya 2018/2019 ili iendelee kuchangia mfuko wa UKIMWI uliouanzishwa mwaka 2015.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa mgodi wa dhahabu geita (GGM), Bw. Richard Jordison alisema GGM kwa ushirikiano na Tume ya kuthibiti UKIMWI Tanzania, (TACAIDS) na washiriki wengine imekusudia kuona jamii yenye afya na nguvu ya kuzalisha kama ambavyo ni malengo ya serikali kuifanya Tanzania ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025. Pia akitumia fursa hiyo kuishukuru serikali ya Tanzania kwa niaba ya wafanyakazi wa GGM, kwa ushirikiano walioutoa tangu kuanza kwa Kili Challenge mwaka 2002.
Mkurugenzi wa Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania, (TACAIDS), Dkt. Leornard Maboko, alisema kutokana na kuendelea kuwepo kwa VVU na UKIMWI, ushiriki wa wadau mbalimbali nchini, hususani sekta binafsi umekuwa siku zote ukipewa kipaumbele na serikali. Hivyo kuendelea kutekelezwa kwa mfuko huu wa Kili Challemge hapa nchini siyo tu kumeongeza huduma kwa walengwa bali imesaidia utekelezaji wa dhima ya “Kili Challenge” ya kushirikisha wadau kuchangia kwa hali na mali katika udhibiti wa UKIMWI.



Dkt. Leonard Maboko amesema pamoja na hatua zilizofikiwa kwenye mwitikio dhidi ya VVU na UKIMWI tangia ugunduliwe, UKIMWI bado ni tatizo kubwa kijamii na kiuchumi nchini. Kwa mfano, bado kuna maambukizi mapya yanayokadiriwa kufikia 81,000 kila mwaka, ambapo kiwango cha maambukizi ni 4.7 %. Aidha takribani watu milioni 1.4 wanaishi na VVU nchini Tanzania, huku akieleza zaidi kuwa wanawake wa rika zote bado wanaathirika zaidi na UKIMWI kuliko wanaume. Hali hii inaonesha kuwa wanawake kwa kiasi kikubwa wanalemewa na mzigo wa ugonjwa wa UKIMWI. Katika jitihada za kujenga mwitikio kabambe wa kitaifa, Tume ya kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) imeendelea kushughulikia changamoto za unyanyapaa, usawa na Ukatili wa Kijinsia ili kulinda haki za watu walioathirika kwa njia moja au nyingine na janga la VVU na UKIMWI.



Mkurungenzi wa TACAIDS, Dkt. Leonard Maboko, amesisitiza wadau wengine kuendelea kujitokeza kuchangia mwitikio wa kitaifa dhidi ya UKIMWI ili mchango wa sekta binafsi uendelee kuongeza nguvu kwenye jitihada za serikali na kupunguza pengo linalotokana na mchango wa Serikali na Wahisani.



Vilevile, Mkurugenzi wa TACAIDS,  Dkt. Leonard Maboko, ameushukuru uongozi wa GGM kwa kushirikiana nao hadi kutimiza miaka 17 ya utekelezaji wa mfuko huu wa Kili Challenge huku akisema hiki ni kielelezo cha ushirikiano wa sekta binafsi katika udhibiti wa UKIMWI nchini.



Lakini pia mkurugenzi wa GGM, Bw. Richard Jordison alitoa shukrani zake kwa Balozi wa GGM Bw, Mrisho Mpoto kwa kazi nzuri anayoifanya, huku akisema, “Msanii huyu amekuwa Balozi mzuri kwenye masuala ya UKIMWI na hasa kuhamasisha uchangiaji wa fedha katika mfuklo wa Kili Challenge kwa kupanda au kuzunguka mlima wa Kilimanjaro kupitia baiskeli.”



Ili kushiriki GGM Kili Challenge, unaweza kuchangia mfuko huu kwa kujifadhili au kumfadhili mwingine kupanda au kuzunguka mlima Kilimanjaro. Kwa mawasiliano zaidi au kutoa mchango wasiliana nasi kupitia email: GGMkilichallenge@anglogoldashant.com, au tovuti www.geitakilichallenge.com.



Geita Gold Mine na TACAIDS tunatumia mwamvuli huu wa Kili Challenge katika kuelimisha jamii kuhusu janga hili la VVU/UKIMWI na tunatarajia siku moja Tanzania itatangaza kuisha kwa maambukizi ya VVU/Ukimwi kama takwimu zilizotolewa na Tume ya Kuthibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), zimeonesha kupungua kwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka asilimia 5.1 %  mwaka 2011/ 2012 hadi asilimia 4.7% mwaka 2016/17. Kwa maelezo zaidi tembelea tovuti ya www.geitakilichallenge.com

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)