Pages

BALOZI WA CHINA ATETA NA DK MENGI, AAHIDI KUSAIDIA MABADILIKO

 Balozi wa China nchini Tanzania, Mh. Wang Ke (kushoto) akiwa kwenye mazungumzo na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dk. Reginald Mengi kuhusu ushirikiano wa kibiashara baina ya makampuni ya China na Tanzania ofisini kwa mwenyekiti huyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dk. Reginald Mengi akifafanua jambo kwa Balozi wa China nchini Tanzania, Mh. Wang Ke (kushoto) wakati wa mazungumzo kuhusu ushirikiano wa kibiashara baina ya makampuni ya China na Tanzania ofisini kwa mwenyekiti huyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
 Balozi wa China nchini Tanzania, Mh. Wang Ke akisoma muonekano wa mbele wa kitabu kinachozungumzia maisha ya Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dk. Reginald Mengi ulioandikwa “I Can, I Must, I Will - The Spirit of Success” wakati wa mazungumzo yao kuhusu ushirikiano wa kibiashara baina ya makampuni ya China na Tanzania ofisini kwa mwenyekiti huyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
 Balozi wa China nchini Tanzania, Mh. Wang Ke  akimkabidhi Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dk. Reginald Mengi zawadi  ya kasha la majani ya chai (China Green Tea) kutoka nchini China mara baada ya mazungumzo kuhusu ushirikiano wa kibiashara baina ya makampuni ya China na Tanzania ofisini kwa mwenyekiti huyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dk. Reginald Mengi akiagana na Balozi wa China nchini Tanzania, Mh. Wang Ke ambapo alimshukuru kwa kufika ofisini kwake na kufanya mazungumzo kuhusu ushirikiano wa kibiashara baina ya makampuni ya China na Tanzania ofisini kwa mwenyekiti huyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Na mwandishi wetu
CHINA imetaka watanzania kutumia fursa ya kuwa na maji mengi na ardhi ya kutosha kufanya shughuli za kilimo na kuzalisha mazao mengi ambayo wanaweza kuyauza nchini humo na pia kuyatumia kama malighafi kwa viwanda vya ndani.

Taifa hilo kubwa kiuchumi duniani, limesema kwamba ufunguo wa maendeleo ya viwanda upo katika kilimo na biashara ya kilimo hivyo ipo haja kwa watanzania kufanya bidii katika kufanikisha kilimo.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke kwenye mazungumzo na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dk Reginald Mengi, ofisini kwa mwenyekiti huyo mwishoni mwa wiki.

Katika mazungumzo hayo Dk Mengi aligusia zaidi kuhusu China kuona haja ya kusaidia kuinua kilimo cha Tanzania kutokana na mabadiliko yanayofanywa Tanzania ya kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.

Alisema uchumi huo utawezekana kwa kutumia rasilimali za kilimo kama malighafi na kilimo cha Tanzania kinahitaji sapoti kubwa ya kukifanya kuwa cha biashara.

Balozi wa China alikiri kwamba ipo haja ya kukibadili kilimo cha Tanzania ambacho kwa sasa ni cha kifamilia zaidi na kuwa cha biashara na kusema wapo tayari kushiriki katika ndoto za watanzania kwenda kwenye uchumi wa viwanda kwa kutegemea malighafi za kilimo.

Hata hivyo alisema kwamba China inahitaji sana mazao ya kilimo kutoka Tanzania, kasoro ni kuwa uzalishaji bado ni mdogo sana.

Alitolea mfano wa kuwepo kwa kiwanda cha mafuta ya kula ya alizeti kwamba mbegu huwa hazitoshi na hivyo kiwanda hicho cha Wachina kulazimika kuagiza mbegu kutoka nje.

Alisema kwa sasa kiwanda hicho kinatengeneza tani elfu 10 za mafuta wakati uwezo wa kiwanda ni tani laki moja kwa mwaka.

Aidha alisema ipo haja ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kama malighafi ya viwanda.

Balozi Wang Ke alisisitiza uzalishaji kwa wingi wa mazao mbalimbali ya kilimo kwa ajili ya viwanda vya Tanzania na kuuza nchini China, kwa vile nchi hiyo inahitaji kiwango kikubwa cha bidhaa za kilimo kutoka Tanzania.

“China inapenda kununua bidhaa za kilimo kutoka Tanzania, lakini tatizo kubwa ni kupata wenye uwezo wa kulima kibiashara watakaozalisha na kusafirisha kiasi kikubwa cha bidhaa kulingana na mahitaji ya soko la nchi hiyo lenye idadi kubwa ya watu” alisema Wang Ke.

Kuhusu kasi ya maendeleo ambayo China imeyapata katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Balozi huyo aliyeambatana na Msaidizi wake Bw. Wang Qiang katika mazungumzo hayo alisema umetokana na uwekezaji mkubwa katika rasilimali watu.

Kuna msemo nchini China kwamba kama unataka kuwa tajiri ni lazima ujikite katika ujenzi wa miundombinu na kutumia rasilimali kwa ujuzi wa hali ya juu na kusema Tanzania ipo katika njia njema kutokana na juhudi za serikali ya awamu ya tano.

Aidha alisema uwekezaji mkubwa kielimu, sera nzuri za maendeleo na juhudi za mtu mmoja mmoja katika kufanya kazi ndiyo yamesababisha mageuzi makubwa yaliyofanywa kuleta mafanikio yao.

“Najua watanzania ni wachapakazi wanachotakiwa ni kuongeza juhudi” alisema Balozi huyo ambaye alisisitiza kwamba mabadiliko ya kweli yatatokana na uchapakazi.

Alisema anatambua kwamba Rais John Magufuli ni mchapakazi na anaamini watanzania watamuiga katika harakati hizo na kwa kuweka rasilimali vizuri na mazingira bora ya biashara na uzalishaji.

Kwa upande wake Dk Mengi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini TPSF amemwomba balozi huyo amsaidia kumwunganisha na makampuni ya China anayoweza kushirikiana nayo kuwekeza kwa ubia katika miradi mbalimbali.

Alitaja miradi hiyo kuwa pamoja na uanzishwaji wa Taasisi ya IPP ya Uendelezaji Teknolojia (IPP Institute of Technology and Innovation), uwekezaji katika kilimo cha kibiashara na kuanzisha kiwanda cha kuunganisha magari yanayotumia umeme.

Katika shughuli za kilimo, Dk Mengi aligusia mtu wa kushirikiana naye kuzalisha maparachichi.

Katika mkutano huo Dk Mengi alimzawadia mgeni wake kitabu alichokiandika ambacho kitakazinduliwa hivi karibuni, huku Balozi akimzawadia mwenyeji wake kasha la majani ya chai kutoka nchini China.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)