Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkinga,Mhandisi Michael Ndunguru (wa tatu kutoka kushoto) akiongoza wadau mbalimbali kufungua bomba wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji wa Mkinga mkoani Tanga.
Wadau wa mradi wa maji wa Mkinga wakibeba ndoo kwa pamoja wa hafla ya uzinduzi wa mradi.
Mratibu wa Huduma za Maendeleo wa Shirika la Water Missions International Tanzania, Isack Abdiel, akielezea mradi huo kwa waandishi wa habari.
Baadhi ya wanafunzi na wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi huo.
Kisima cha maji kilichokuwa kinatumika kabla ya mradi mpya.
Sehemu ya miuondombinu ya mradi mpya.
Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na kusambaza huduma za maji la Water Missions International Tanzania, mwishoni mwa wiki limezindua mradi mkubwa utakaonufaisha vijiji 7 vya wilaya ya Mkinga mkoani Tanga utaowawezesha wananchi kuwa na uhakika wa kupata maji safi na salama kwa matumizi yao na matumizi mengineyo na shughuli za kiuchumi.
Kwa kipindi cha muda mrefu wilaya ya Mkinga imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji salama, kutokana na kutokuwepo na vyanzo vya uhakika vya maji katika eneo hilo.Vijiji 4 vya Mkinga, Mtenguleni, Mwakihonda and Karoyo vimekuwa vikitegemea kupata maji ya bomba kutoka tanki la zamani la kusambaza maji kutoka kijji jirani cha Parangukasere, ambalo limekuwa halitoshelezi mahitaji ya maji kwa wakazi wa vijiji hivyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkinga,Mhandisi Michael Gregory Ndunguru,ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi huo alisema “Leo ni siku ya kihistoria kwa wakazi wa Mkinga,kuzinduliwa kwa maradi huu wilayani hapa kutawezesha wananchi kupata maji safi ya uhakika wakati wote,kwa niaba ya serikali nalishukuru shirika la Water Missions International Tanzania kwa kuunga mkono jitihada za serikali ya Tanzania ya kukabiliana na changamoto za uhaba wa maji katika maeneo mbalimbali nchini”.
Mhandisi Ndunguru, alisema mradi huu utanufaisha maisha ya mamia ya wananchi wakazi wa Mkinga na kupunguza adha kwa wanawake ambao wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya kifamilia . Alitoa wito kwa wakazi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano wa shirika hilo sambamba na kutunza miundo mbinu itakayowekwa katika maeneo yao ili kuwezesha mradi kuwa endelevu.
“Mradi huu muhimu hapa Mkinga pia utaimarisha afya na kupunguza uwezekano wa kutokea magonjwa mbalimbali yanayosababisha na ukosefu wa maji na matumizi ya maji yasiyo salama kwa kuwa hivi sasa tuna uhakika wa kupata maji salama,”alisisitiza.
Kwa upande wake,Mratibu wa Huduma za Maendeleo wa Shirika la Water Missions International Tanzania ,Isack Abdiel alisema “Tunayo furaha kuzindua mradi wa maji katika wilaya ya Mkinga ,ukiwa ni mwendelezo wetu wa kuunga mkono serikali ya Tanzania kuboresha upatikanaji wa maji ya uhakika na salama kwenye jamii zenye upungufu wa maji nchini,tunayo imani wananchi mmeupokea vizuri na mtaulinda ili uwe mradi endelevu ili unufaishe mpaka vizazi vijavyo”.
Aliwashukuru watendaji wa serikali,mashirika yasiyo ya kiserikali inayoshirikiana nayo na wadau wote ambao wamefanikisha jitihada za kuanzisha mradi huu wilayani Mkinga.
Shirika la Water Missions International Tanzania,lilianza kufanya kazi nchini mnamo mwaka 2013, likiwa limejikita katika kuendesha miradi ya kuondoa kero ya maji kwenye jamii ,sambamba na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu miradi ya maji.Hadi kufikia sasa shirika limefanikisha miradi ya maji katika mikoa zaidi ya 6 nchini,ikiwemo mikoa ya Dodoma, Arusha, Geita, Kagera na Tanga.
Ofisi za makao makuu ya Water Missions International Tanzania nchini yapo jijini Dar es alaam na ndipo inaporatibiwa miradi yote ya maji inayoendeshwa na shirika nchini .Tanzania ni nchi ya 10 kuwa na miradi ya shirika hili.Baadhi ya nchi nyingine linapoendesha miradi ya maji ni Kenya, Uganda, Malawi, Haiti, Honduras, Mexico, Peru, na Belize.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)