TPDC YAIMARISHA SEKTA YA AFYA KIDUNDAI, LUSHOTO - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

TPDC YAIMARISHA SEKTA YA AFYA KIDUNDAI, LUSHOTO

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kidundai, Ndg. Waziri Mdoe (Kushoto) akipokea mfano wa hundi ya shilingi milioni nne kutoka kwa mwakilishi wa TPDC, Ndg. Asiad Mrutu (Kulia). Makabidhiano hayo yalifanyika mbele ya jengo la zahanati inayoendelea kujengwa katika Kijiji hicho.

Na Mwandishi Wetu.

Katika jitihada endelevu za utekelezaji wa dhana ya uwajibikaji kwa jamii, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ambalo ni Shirika la Mafuta la Taifa kwa mujibu wa Sheria ya Petroli (2015) limeendelea kuitekeleza dhana hiyo kwa vitendo kwa kutoa vifaa vya ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Kidunda Wilayani Lushoto Mkoani Tanga.

Katika tukio hilo lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, TPDC imeweza kukabidhi hundi ya Shilingi milioni nne ambazo Kijiji kiliomba kusaidiwa ili kuwezesha ujenzi wa zahanati hiyo ambapo kwa mujibu wa serikali ya Kijiji, fedha hizo zitawezesha manunuzi ya mizunguko ya nondo 40 yenye futi 40 kila moja, mifuko ya saruji, matofali na gharama za kumlipa fundi ambapo mpaka kufikia hapo zahanati itakuwa imefanikiwa kuezekwa.

Akizungumza na mwandishi wa habari mara baada ya kumaliza makabidhiano, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kidundai kilichopo Kata ya Vuga, Waziri Mdoe alisema “kwa niaba ya halmashauri ya kijiji, tunayo furaha isiyo kifani kwa ndugu zetu kutoka TPDC kwa moyo wa kutoa walioonyesha kwa kusaidia ujenzi wa zahanati yetu ambayo ilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi wa kijiji hicho ili kuondokana na adh ya kutembea umbali wa kilomita nane ili kupata huduma ya afya”.

Mdoe aliongezea kuwa, ni matumaini ya kijiji kwamba TPDC litaendelea kuwa mdau mkubwa wa maendeleo katika Kijiji cha Kidundai kwani mahitaji yao ni mengi yakiwemo maji, barabara na shule

Akikabidhi mfano wa hundi kwa Mwenyekiti wa Kijiji kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Asiad Mrutu ambaye ni Mjiolojia alisema “kipekee nimshukuru Mwenyekiti na Wajumbe wa Serikali ya Kijiji kwa ushirikiano waliouonyesha toka tulipofika siku ya kwanza katika Kijiji hiki tukiwa na lengo la kutafuta eneo la uwekezaji, niseme tu kuwa huu ni mwanzo na tutaendelea kushirikiana bega kwa bega kusukuma gurudumu la maendeleo ya Kidundai mbele.”

Pamoja na kukabidhi hundi hiyo, Mrutu aliusisitiza uongozi wa Kijiji kuchanganua gharama za miradi ya maendeleo iliyopo katika mipango ili kurahisisha pale ambapo mdau wa maendeleo anaetaka kuchangia kufahamu ni kiasi gani kitatosha badala ya kueleza mahitaji kwa ujumla, hii itasaidia kupata msaada kirahisi na pia kupata msaada unaokidhi mahitaji ya mradi husika.

Mchango wa ujenzi wa zahanati hiyo umekuja baada ya TPDC kufanikisha zoezi la kupata ardhi kwa ajili ya miradi ya kimkakati ya utafiti wa mafuta na gesi hapa nchini kwa lengo la kuongeza kiasi cha gesi asilia nchini ambacho kwa sasa ni futi za ujazo trilioni (TCF 57.538) na upatikanaji wa mafuta ili kuweza kulihakikishia taifa nishati ya kutosha kwa ajili uzalishaji wa umeme, vyombo vya usafiri, matumizi ya nyumba na kuhakikishia nishati ya kutosha kwa maendeleo ya viwanda nchini.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages