WADAU wa mradi wa kuwawezesha mabinti na wanawake vijana katika sekta ya elimu wamekutana katikati ya wiki kujadili mpango kazi wa utekelezaji wa mradi wa UNESCO kwa kushirikiana na UNWomen pamoja na UNFPA unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Korea (KOICA).
Mradi huo ambao umelenga kuondoa vikwazo vya elimu kwa wasichana na wanawake kwa kuangalia sera, sheria na kanuni zinazowezesha maendeleo kwa wanawake kwa kuzingatia matakwa ya Umoja wa Mataifa na makubaliano ya kimataifa ambayo Tanzania imetia saini ulianza mwaka 2016.
Mradi huo unaotarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kwa kusimamiwa na Ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN Women) na Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya Watu ( UNFPA) unatarajia kuiwezesha Tanzania kuwezesha elimu kwa kutumia mbinu mtambuka kwa kutambua watu wa pembezoni.
Mradi huo unatarajiwa kuwawezesha wasichana na wanawake vijana kuwa na uwezo wa kuingia katika utuuzima bila kuvurugwa utaratibu wa upatikanaji wa elimu.
Mradi huo unatekelezwa katika wilaya nne za Ngorongoro, Sengerema, Kasulu na Mkoani huko Pemba.
Mkutano huo wa kamati ya ufundi ya mradi ulilenga kutoa ratiba ya utekelezaji wa mradi baada ya mada mbalimbali kuwasilishwa za utafiti uliofanyika na hali halisi iliyopo nchini kuhusu wasichana na wanawake kwa kuangalia sharia zilizopo, utamaduni na tabia.
Akizungumza katika mkutano huo Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria (OUT) Kitivo cha Elimu, Dk. Felix Mulengeki alisema kwamba mradi huo utafanikiwa kutokana na ukweli kuwa sharia na katiba za nchi zipo vizuri huku sera nazo zikitambua haki ya kusoma.
Wakati mradi unabuniwa ilionekana kwamba kutoeleweka kwa katiba na sheria zilizopo zinazomlinda mtoto wa kike, uelewa hafifu umekuwa ukikwamisha maendeleo kielimu kwa watoto wa kike.
Dk. Mulengeki alisema kwamba hali ya sera na sheria nchini Tanzania ni salama zaidi kilichobaki utekelezaji wa mradi huo umelenga kukusanya pia takwimu kwa ajili ya kutumika kutengeneza sera.
Katika mradi huo unatarajiwa kuongeza uelewa zaidi wa elimu ya afya ya uzazi na kutengeneza mifumo ya kuelimisha watu.
Mada mbalimbali zilizojadiliwa ziliwezeshwa kupata muda wa utekelezaji wa vipengele mbalimbali ambavyo vilipaswa kufanyika ili kuondokana na tabia mbaya ambazo zinamnyima binti wa Kitanzania kukamilisha elimu yake.
Naye Kaimu Mkuu wa ofisi na Mkuu wa kitengo cha Elimu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) ofisi za Dar es Salaam, Faith Shayo amesema kwamba mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo na kwamba kamati ya ufundi ya mradi huo ilikutana mara ya kwanza Mei mwaka jana.
Naye Ofisa wa Kitaifa anayeshughulikia Elimu ya Afya na Ukimwi ofisi za Unesco Dar es Salaam, Mathias Herman anasema kwamba kuna matokeo chanya ya mradi huo.
Anasema kwamba madhila mengi ya mabinti katika wilaya hizo zinazofanyiwa utekelezaji wa mradi yamepungua na hali zao kuwa bora kutokana na taasisi mbalimbali zinazohusika na elimu na usalama wa watoto wakike kushirikiana kukabili matatizo waliyonayo.
Pia amesema katika suala la elimu ya afya ya uzazi na Ukimwi kumekuwa na mabadiliko kwani taarifa zinakwenda kwa wakati na zinafanyiwa kazi inavyotakiwa na sekta mbalimbali zikiwemo taasisi za kiserikali katika kumsaidia mtoto wa kike
Aidha amesema kwamba vitini vya kufundishia elimu mbalimbali ambazo zimo katika mradi zimeshafanyiwa kazi na kusambazwa.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)