SERIKALI KUPITIA DAWASA KUJENGA MITAMBO MITATU YA KISASA YA KUCHAKATA MAJI TAKA JIJINI DAR ES SALAAM - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

SERIKALI KUPITIA DAWASA KUJENGA MITAMBO MITATU YA KISASA YA KUCHAKATA MAJI TAKA JIJINI DAR ES SALAAM


 Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam, (DAWASA), Bi. Modester Mushi(kushoto), akifafanua jambo leo Januari 15, 2018 kwa kutumia ramani ya mradi wa ujenzi wa mitambo mitatu ya kuchakata maji taka jijini Dar es Salaam, kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, jijini, Mhe. Ali Hapi, wakati alipotembelea eneo la Kilongawima, Mbezi Beach jijini ambako patajengwa moja kati ya mitambo hiyo. Katikati ni Meneja Uhusiano wa Umma wa DAWASA, Bi. Neli Msuya.

NA K-VIS BLOG/Khalfan Said
WIZARA ya Maji na Umwagiliaji, kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka, Dar es Salaam (DAWASA), inajiandaa kujenga mitambo mitatu ya kisasa ya kuchakata maji taka, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kuboresha hali ya mazingira jijini.

Hayo yamesemwa leo Januari 15, 2018 na Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi wa DAWASA, Bi. Modester Mushi wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa mitambo hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinodnoni jijini Dar es Salaam, Mhe. Ali Hapi, wakati alipotembelea moja ya maeneo ya mradi huo huko Kilongawima, Mbezi Beach.

“Ujenzi wa mitambo hii utakwenda sambamba na ujenzi wa mfumo wa ukusanyaji maji taka katika jiji la Dar es Salaam ambapo lengo ni kulaza jumla ya kilomita 563 za mabomba ya ukubwa mbalimbali ya ukusanyaji na usafirisha maji taka kutoka sehemu mbalimbali za jiji na kuyamwaga kwenye mitambo mikubwa mitatu itakayojengwa hapa Kilongawima,(Mbezi Beach), Jangwani na Kurasini.” Kaimu Mkurugenzi huyo amemueleza Mkuu wa Wilaya Mhe. Hapi.

Kuhusu ukubwa wa mitambo hiyo, Bi. Modester alisema, Mtambo wa Kilongawima (Mbezi Beach) utakapokamilika, utakuwa na uwezo wa kuchakata maji taka yenye mita za ujazo 16,000 kwa siku, wakati ule wa Jangwani utakuwa na uwezo wa kusafisha (kuchakata) maji taka yenye lita za ujazo 200,000 kwa siku na ule wa Kurasini utakuwa na uwezo wa kuchakata maji taka yenye lita za ujazo 11,000 kwa siku. “Ujenzi wa mitambo hii utaanza muda wowote mwaka huu wa 2018 na utagharimu kiasi cha
dola za Kimarekani Milioini 65.” Alisema.

Akifafanua zaidi jinsi mitambo hiyo ya kisasa itakavyofanya kazi, Bi.Modester Mushi alisema, mitambo hiyo pia itazalisha gesi asilia na umeme kwa ajili ya kujiendesha, na hivyo kupunguza matumizi na gharama za umeme.

“Lakini pia maji yatakayokuwa yamesafishwa yatauzwa na kutumika katika shughuli mbalimbali kama vile kupoozea mitambo na umwagiliaji wa bustani wakati tope litakalobaki baada ya mchakato huo wa usafishaji maji taka litaweza kutumika kama mbolea kwa ajili ya kilimo lakini pia kuendesha bustani za miti ya kivuli na hivyo kulipendezesha jiji.” Alifafanua Bi. Modester na kuongeza, Katika eneo la Jangwani , bustani ya kisasa itakayokuwa na miti ya kivuli, maua  na viti vya kupumzikia itajengwa ili kuboresha taswira ya eneo hilo la Jangwani na hiyo itakuwa ni mchango wa DAWASA katika kuunga mkono harakati za Serikali za kuboresha usafi wa mazingira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya Mhe. Ali Hapi, aliwapongeza DAWASA kwa hatua wanazochukua hususan kazi ya kuanza mradi huo na kuwataka waharakishe utekelezaji wa mradi. “Changamoto kubwa ambayo tubnakabiliana nayo sisi viongozi wa serikali hatuelewi sana ni ucheleweshwaji wa mradi,tunatamani kuona vitu vinatokea na hasa mnapotuhakikishia kuwa fedha zipo, kama mnachangamoto zozote ni vizuri kuzifikisha kwenye mamlaka zinazohusika ili ziwasaidie kutatua changamoto hizo ili kwa pamoja tuweze kuwaletea wananchi maendeleo.” Alisema  Mhe. Hapi.

Mheshimiwa Hapi pia alitembelea kituo cha kusukuma maji taka cha Shoppers Plaza, Mikocheni pamoja na kutembeelea maeneo korofi yanayovuja maji taka kwenye eneo la Mikocheni na Mwenge na kuitaka Kampuni nayosimamia uendeshaji wa kuondoa maji taka DAWASCO kuhakikisha wahandisi wake wanatoka maofisini na kukagua maeneo korofi ili kuchukua hatua za kuyarekebisha. “Nasisitiza tena Wahandisi watembelee maeneo ambayo kazi zao zipo, watembelee barabara zetu, Halmashauri zinatumia fedha nyingi kurekebiusha barabara zetu, zikirekebisha baada ya mwezi mmoja chemba zinapasuka na kuharibu barabara, hatuwezi kuendelea na utaratibu huu, ni lazima tutafute suluhu.” Alisema. 
 Mhe. Hapi akizungumza kwenye moja ya maeneo korofi ya chemba ya maji taka Mikocheni jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara hiyo.
 Mhe. Hapi akizunghumza kwenye eneo korofi la chemba ya maji Taka Mikocheni jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara hiyo.
 Mhe. Hapi (kushoto), akitazama ramani hiyo.
 Mkuu wa Wilaya Mhe. Ali Hapi, (kulia), akifafanua jambo wakati alipotembelea eneo lililopangwa kujengwa mtambo wa kuchakata maji taka huko Kilongawima, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, leo Januari 15, 2018. Kulia ni Meneja Uhusiano wa Umma wa DAWASA, Bi. Neli Msuya.
 Bi. Modester akimsikilkiza kwa makini Mkuu wa Wilaya Mhe. Ali Hapi (hayupo pichani).
 Mkuu wa Wilaya Mhe. Hapi, (kulia), akibadilishana mawazo na Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi wa DAWASA, Bi. Modester Mushi, (kushoto) na Meneja Uhusiano wa Umma, Bi., Neli Msuya.
 Mhe. Hapi akizungumza mbele ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwenge jijini Dar es Salaam, Bw.Bashiri Hoza, (kulia) na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mwenge, alipotembelea kuona maeneo korofi ambayo chemba za mitaro ya maji taka hufumuka mara kwa mara kwenye eneo hilo jirani na soko la Mwenge.
 Mhe. Hapi akizungumza mbele ya wananchi alipotembelea maeneo korofi ambayo chemba za maji taka hufumuka mara kwa mara eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Hapi, akitoa maelekezo alipotembelea eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam kuona miundombinu ya maji taka.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages