Mwekezaji mpya katika klabu ya Simba, Mohammed Dewji MO amesema amejipanga kushirikiana na wanahisa wenzake wa klabu hiyo kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kupitia kampuni ya Simba Sports Club Limited.
Dewji aliyasema hayo wakati akitoa salamu kwa wanachama na mashabiki wa Simba kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa klabu hiyo, baada ya kutangazwa na kamati maalum ya kusimamia mchakato wa kumpata mwekezaji katika klabu ya Simba, kuwa mshindi wa tenda ya kuwekeza katika klabu hiyo.
Alisema klabu ya Simba inampongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuongoza serikali ya awamu ya tano, na wao wamedhamiria kuhakikisha wanakwenda sambamba na kasi yake kupitia mchezo wa mpira kwa kutoa ajira kwa Watanzania kwenye kampuni mpya itakayosimamia timu hiyo katika mfumo wa hisa.
Mwekezaji mpya katika klabu ya Simba, Mohammed Dewji MO akizungumza kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa klabu hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere.
"Tamati yangu nielekeze kwa sisi sote kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayofanya ya kuongoza taifa hili. Wote tumtakie kila la kheri, baraka na fanaka tele katika utumishi wake uliotukuka,
"Pamoja na kupongeza sera yake ya ujenzi wa viwanda nchini, ambapo sisi kwa upande wetu, klabu ya Simba inamuunga mkono kwa ujenzi wa kiwanda kikubwa kabisa cha soka yaani Simba Sports Club Limited, ambacho licha ya kuongeza ajira lakini pia tutaendelea kulipa kodi kwa mujibu wa sheria za nchi," alisema Dewji.
Dewji ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mohammed Entreprises, alitumia mkutano huo kuelezea mipango ambayo wameipanga ili kuiwezesha Simba kuwa klabu kubwa zaidi barani Afrika kuliko ilivyo sasa, huku malengo ikiwa ni kuwania mataji makubwa barani Afrika.
Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah akimkabidhi cheti cha ushindi wa tenda ya kuwekeza katika klabu ya Simba mfanyabiashara na mwanachama wa muda mrefu wa klabu hiyo, Mohammed Dewji MO kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa klabu hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere.
"Katika mwaka wa kwanza, nawaahidi kwa kushirikiana na ninyi tutakuwa na kiwanja cha nyasi asilia, na kiwanja cha nyasi za bandia ambapo viwanja hivi tutavitumia kwa mazoezi kwa kadri ya mahitaji ya mechi tunayokwenda kucheza,
"Pia tutajenga hosteli ambayo itakuwa na vyumba 35 ambavyo wataishi wachezaji 30 na support staff, kila chumba kitakuwa na ukubwa wa 35 square- meter... ili kufanya eneo hilo kuwa bora kwa wachezaji wetu," alisema Dewji na kuongeza.
"Wote tunaopenda mpira, tunajua kama ukitaka kuwa na wachezaji bora lazima utumie pesa. Nia yetu kwa mwaka wa kwanza, tunatarajia kiwango cha chini cha pesa ya usajili iwe bilioni moja. Pia tumetenga milioni 500 kuboresha benchi la ufundi, kwa kushirikiana na benchi liliopo sasa."
Hata hivyo Dewji, alisema klabu ya Simba itajenga kituo cha kukuzia vipaji ambacho kitakuwa na wachezaji vijana. Jambo ambalo litaisaidia Simba kuwa na wachezaji bora vijana ambao wamefundishwa kucheza soka katika kituo cha timu hiyo.
"Ili kuwa na wachezaji bora kwa miaka ijayo tunahitaji kuwa na kituo cha kukuzia vipaji kwa wachezaji wa umri chini ya miaka 14, 16, 18. Na mipango yetu ya baadae ni kushirikiana na timu kubwa za ulaya kutuongoza na kutuelemsha jinsi gani ya kujenga kituo chenye hadhi ya kimataifa na mungu akipenda tutakuwa na kituo bora barani Afrika." alisema Dewji.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)