Pages

SERIKALI YALIPA FIDIA YA BIMA YA AMANA KWA WATEJA WA BENKI YA FBME SH. MILIONI 728

SERIKALI imetumia kiasi cha Sh. Mil 728 kuwalipa amana zao wateja zaidi ya 695 wa Benki ya FBME ambayo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeifutia leseni ya kufanya shughuli za kibenki hapa nchini.

Hayo yamesemwa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), wakati akijibu maswali ya Mbunge wa Viti Maalum Mhe.  Rukia Kassim Ahmed (CUF), aliyetaka kufahamu, pamoja na mambo mengine, hatma ya wateja wa Benki hiyo baada ya kufutiwa leseni yake ya kujihusisha na masuala ya kibenki Mei 8, 2017.

Mhe. Ahmed alitaka kufahamu msimamo wa Serikali endapo fedha za kuwalipa wateja hao zinazotokana na kuuza mali, makusanyo ya madeni na fedha zilizowekezwa kwenye taasisi nyingine na Benki hiyo hazitatosha.

Aidha, alihoji kuhusu uamuzi wa Bodi ya Akiba ya Amana ambao unaeleza kuwa hata kama mteja aliweka amana yake kwa fedha za kigeni katika benki hiyo, watalipwa kwa fedha za kitanzania kwa kiwango kilichokuwepo wakati Benki hiyo inafilisiwa Mei 8, 2017.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji alisema kuwa malipo ya wateja yanalipwa kutokana na sheria ya mabenki na Taasisi za fedha ya mwaka 2006 kifungu cha 39, na kwamba kinachofanyika hivi sasa ni utekelezaji wa sheria hiyo.

 “Serikali haina mpango wa kumuonea mteja yoyote, madeni yatakusanywa  na fedha zitalipwa kwa kila mteja kulingana na amana alizojiwekea, Serikali inalisimamia jambo hilo kwa  umakini wa kiwango cha juu.” alisema Dkt. Kijaji.

Katika swali lake la msingi Mhe. Rukia Kassim Ahmed (CUF), alitaka kujua hatma ya wateja walioweka fedha zao katika Benki ya FBME, baada ya Benki Kuu ya Tanzania kuifutia leseni ya kufanya shughuli zake za kibenki na kuiweka chini ya ufilisi wa Bodi ya Bima ya Amana kuanzia Mei 8, 2017.

Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa hatua ya kwanza kwa mujibu wa sheria ni malipo ya fidia ya Bima ya Amana ya kiasi kisichozidi Sh. 1,500,000 kutegemea na kiasi cha salio la amana wakati beki inafungwa.

“Fedha za kulipa fidia hiyo zinatoka katika Mfuko wa Bima ya Amana (Deposit Insurance Fund) unaosimamiwa na Bodi ya Bima ya Amana (Deposit Insurance Board (DIB))” alisema Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji aliongeza kuwa wateja waliokuwa na amana zisizozidi kiwango cha juu cha fidia cha Sh. 1,500,000 wakati benki inafungwa watapata fedha zao zote.

“Kiasi kitakachozidi kiwango hicho kitalipwa kutegemea kiasi cha fedha kitakachopatikana kutokana na mauzo ya mali, makusanyo ya madeni na fedha zilizowekezwa katika Taasisi nyingine”.alisema Dkt. Kijaji.

Imetolewa na:                                              

Benny Mwaipaja
Mkuu wa  Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)