WANANCHI wa Kata ya Mkata Wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga wanatarajia kunufaika na huduma mbalimbali za kibenki ikiwemo mikopo kwa wafanyabiashara baada ya Benki ya NMB kuzinduwa tawi jipya la Benki hiyo eneo la Mkata.
Akizinduwa tawi hilo hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh. Martine Shigella aliwataka wakazi wa Mkata na maeneo ya jirani kuacha sasa kuhifadhi fedha nyumbani na badala yake kuhifadhi benki. Aliongeza uzinduzi wa tawi hilo ni fursa kubwa kwa wakazi wa Mkata na maeneo ya jirani kuzitumia huduma za kifedha.
Aliongeza kuwa Mkata ni eneo lenye mzunguko mkubwa wa kifedha kutokana na kuwa na wafanyabiashara mbalimbali, wakulima, wafugaji, wafanyabiashara wa matunda na biashara nyingine hivyo wanategemea kwa kiasi kikubwa huduma ya benki katika utunzaji wa fedha na usalama wao.
Mh. Shigella alisema kuwa NMB Benki imesaidia sana wananchi kwa kutoa mikopo na misaaada mingine ya kijamii hivyo ni vyema kuitumia benki hiyo kwani kwa kufanya biashara na NMB ni kufanya biashara na serikali kwa sababu kwa upande mwingine NMB ni Serikali ambapo fedha zinazowekwa ndizo zinazorudi kwenye jamii kwa mtindo wa mishahara, ujenzi wa miundo mbinu na huduma nyingine za kijamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ineke Bussemaker, alisema kuwa NMB kwasasa inaendelea kupanua huduma zake ili ziweze kuwafikia wananchi kote nchini hususani wale wa vijijini. Bussemaker, alisema kuwa miaka 12 iliyopita NMB haikuwa na ATM wala huduma za kibenki za kwenye simu lakini kwasasa huduma zimepanuka mpaka kufika matawi ya kibenki nchini 213,ATM 700 na wakala 4,100.
Naye Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Salie Mlay, alisema kuwa mpaka sasa kanda yake ina matawi 33 ambapo kati yake Handeni Mjini lipo moja na Mkata moja huku Tanga Mjini yakiwa matawi mawili.
Mlay, alisema kuwa kwasasa benki hiyo inafanya jitihada za kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi wote hususani wale waliopo katika maeneo ya Vijijini ambapo amewataka wananchi kuendelea kutumia benki hiyo kwa manufaa yao na hata Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe ameshukuru uongozi wa NMB kwa kuona umuhimu wa kufungua tawi eneo la Mkata ambalo litawasaidia wakazi wa eneo hilo na jirani kutotembea urefu wa KM54 kufuata huduma za benki kwa kuzingatia kwamba eneo la Mkata linawafanayabiashara wengi na mzunguko wa fedha ni mkubwa.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh. Martine Shigella (wa tatu kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ineke Bussemaker (wa pili kushoto), pamoja na viongozi mbalimbali wakizinduwa tawi jipya la Benki ya NMB Kata ya Mkata Wilayani Handeni.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga –Martin Shighela (kwanza kulia) akijadili jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa NMB Bank PLC-Bi Ineke Bussemaker wakati wa uzinduzi rasmi wa tawi la NMB Mkata mkoani Tanga.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)