SERIKALI YAHIMIZA UNAWAJI MIKONO NA SABUNI - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

SERIKALI YAHIMIZA UNAWAJI MIKONO NA SABUNI

Wanafunzi wa Shule za Msingi  zilizopo Kata ya Kiwalani wakishiriki igizo lenye lengo la kuelimisha   jamii umuhimu wa kunawa mikono na majisafi na sabuni wakati wa kilele   cha wiki ya unawaji mikono kwa  maji na sabuni yaliyofanyika Kiwalani Dar es Salaam mwishoni mwa wiki

                               
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imewataka wananchi kuunga mkono juhudi za usafi  kwa kunawa 
mikono na sabuni ili kujikinga na maradhi yatokanayo na uchafu ili 
kujenga Taifa lenye watu wenye afya bora.

Akizungumza katika kilele cha wiki ya unawaji mikono kwa maji na sabuni 
iliyofanyika Kata ya Kiwalani, Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam 
mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Ubora wa Mamlaka ya Majisafi na 
Majitaka Dar es Salaam(DAWASA), Dk  Sufiani Masasi alisema kama Taifa ni
muhimu kuwekeza nguvu katika kuelimisha jamii hasa umuhimu wa kunawa  
mikono na majisafi na sabuni ili kujenga Taifa lenye afya bora.

Akizungumza na jumuiya ya wananchi, waalimu na wanafunzi wa shule za 
msingi  Umoja, Yombo, Mwale na Bwawani, Dk Masasi alisema DAWASA ni mdau 
muhimu wa usafi wa mazingira ndio sababu waliamua kuadhimisha wiki hiyo 
kwa kutoa elimu kwa walimu 44 kutoka katika shule hizo pamoja na baadhi 
ya viongozi wa serikali ya mtaa ili wawe mabalozi 
wazuri katika kuwaelimisha wanafunzi juu ya umuhimu wake.

Alisema kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni ‘Mikono safi kwa 
manufaa ya sasa na baadae’ inaikumbusha jamii kuona umuhimu wa kunawa  
mikono na sabuni ili kujikinga na maradhi yatokanayo na uchafu.

Hivyo alitaka juhudi za pamoja zichukuliwe kuhakikisha wanafunzi 
wanaelewa umuhimu wa kunawa mikono kwani wao ndio wazazi wa siku zijazo  
na kwamba DAWASA itaendelea kuunga mkono kampeni za usafi hasa kwa  
kuendelea kubuni na kutengeneza miundombinu ya majisafi katika Maeneo  
mbalimbali ya jiji.

Dk Masasi alisema tayari DAWASA imefanikiwa kufikisha mradi huo wa 
majisafi kwa shule hizo ambapo utanufaisha wanafunzi 5123 pamoja na 
zahanati ya eneo hilo na kwamba itaendelea kufadhili miradi ya aina hii 
ili kuunga mkono juhudi hizo za usafi wa mazingira.

Mkufunzi wa mafunzo kwa walimu wa shule hizo, Juhudi Nyambuka ambaye ni  
Afisa Afya Manispaa ya Temeke alipongeza juhudi za DAWASA katika 
kusaidia jamii kupata huduma za majisafi na kueleza zitasaidia kupunguza
magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa maji.

Katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma rasmi za maji ya bomba 
DAWASA, jumuiya za wananchi pamoja na wadau wa maendeleo wamekuwa  
wakijenga miradi ya maji kupitia programu ya maji na usafi wa mazingira  
kwa jamii. 


Miradi hiyo ipo katika maeneo mbalimbali kama vile Ukonga, Yombo, Kitunda, Mbagala, Kijichi, Feri,Kigamboni Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages