Pages

SERIKALI YADHAMIRIA KUFUNGUA UTALII WA KANDA YA KUSINI, YAPO MAPOROMOKO YA PILI KWA KUWA NA KINA KIREFU ZAIDI BARANI AFRIKA

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) akiteta
jambo na Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni ya Greens Construction Limited, nHamimu Bakari wakati akishuka kwenye ngazi maalum zinazojengwa na mkandarasi huyo kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. 


Na Hamza Temba - WMU
...............................................................
SERIKALI imesema imedhamiria kufungua utalii wa Kanda ya Kusini
ili kupanua wigo wa vivutio vya utalii nchini na hatimaye kuongeza idadi ya
watalii na kipato kwa Serikali na jamii kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga katika kijiji cha Kapozwa Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa wakati
wa ziara yake ya siku moja ya kutembelea Maporomoko ya Mto Kalambo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya Maporomoko ya Tugela yaiyopo nchini Afrika ya Kusini.

Alisema kwa sasa vivutio vingi vinavyotumika kwa utalii nchini ni vile vya ukanda wa Kaskazini hususan vya wanyamapori ambavyo vimeanza
kuelemewa kutokana na watalii wengi kutembelea ukanda huo zaidi kuliko Kanda ya Kusini ambayo pia ina vivutio mbalimbali vya asili.

Alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo benki ya Dunia kupitia mradi wa REGROW imepanga kuboresha
miundombinu ya vivutio vya utalii vya Kanda ya Kusini na kuvitangaza ili
kuimarisha sekta hiyo muhimu ambayo inachangia asilimia 25 ya mapato yote ya kigeni na asilimia 17.5 ya pato la taifa.

Katika ziara yake hiyo Mkoani Rukwa, alitembelea eneo la Hifadhi
ya Msitu ya Mto Kalambo na kukagua ujenzi unaoendelea wa ngazi maalum
zitakazowawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo ambacho ni mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. 

Alisema Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania
inajenga ngazi hizo ili kuongeza thamani ya maporomoko hayo huku akiagiza Wakala hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine kuongeza juhudi za uwekezaji ili kuimarisha utalii wa kivutio hicho na kupanua kanda yote ya kusini.

"Tumekusudia kupanua wigo wa vivutio vyetu vya utalii kwa kufungua Kanda hii ya Kusini ambayo ina vivutio vingi ambavyo havijachangia
ipasavyo kwenye uchumi wetu, maporomoko haya ni moja ya kivutio adimu katika ukanda huu. 

"Ni wakati muafaka sasa tushirikiane kuhamasisha wawekezaji kujenga mahoteli ya kisasa katika eneo hili, tuone uwezekano wa kuanzisha utalii wa 'cable cars' kuwezesha watalii kuona maporomoko kiurahisi, tujenge
maeneo ya kupumzikia ili kuweka mazingira rafiki ya kupata watalii wengi na mapato yaongezeke" alisema Hasunga.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi wa kijiji cha Kapozwa ambao wanaishi jirani na hifadhi hiyo kushirikiana na Serikali katika uhifadhi wa  uoto wa asili wa hifadhi hiyo pamoja na kudumisha tamaduni zao kwa kusajili
vikundi vya ngoma na kutunga nyimbo za kabila lao kwa ajili ya kutumbuiza
watalii watakaofika kuona maporomoko hayo na hivyo kujitengenezea kipato kupitia utalii wa Kiutamaduni.

Pamoja na Maporomoko hayo kivutio vingine kinachopatikana ukanda
wa kusini ni Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo ni ya pili kwa ukubwa nchini
baada ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti, hifadhi hii inasifika kwa kuwa na tembo wengi kuliko hifadhi nyingine nchini.

Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ni kivutio kingine katika ukanda huu ambacho sifa yake kubwa ni uwepo wa aina nyingi za maua ndwele ya asili ambayo
hayapatikani kwingineko duniani, sifa hiyo imesababisha wenyeji kuita hifadhi hiyo 'Bustani ya Mungu'. Wataalamu wa uhifadhi wanasema endapo maua yaliyopo Kitulo yangekuwa ni wanyamapori basi hifadhi hiyo ingeizidi wanyama waliopo Serengeti.

Vivutio vingine ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Katavi ambayo ni ya tatu kwa ukubwa nchini, Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa, Mikumi, Mahale,
Gombe, Pori la Akiba la Selous, Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Mlima Rugwe na Kimondo cha Mbozi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kushoto) akiteta
jambo na Katibu Tawala Wilaya ya Kalambo Frank Schalwe wakati akishuka kwenye ngazi maalum zinazojengwa kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. 
Meneja wa TFS Wilaya ya Kalambo, Joseph Chezue (kushoto) akimuonyesha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) ngazi maalum zinazojengwa kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18.
 Muonekano wa ngazi hizo kuelekea kwenye Maporomoko ya Mto Kalambo.
Muonekano wa ngazi hizo.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (katikati) akizungumza
na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kukagua ujenzi wa ngazi maalum zinazojengwa kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura. 
Baadhi ya washiriki wa ziara hiyo wakishuka kwenye ngazi ambazo ujenzi wake bado unaendelea. Ujenzi huo ukikamilika ngazi hizo zitakuwa na urefu wa mita 227.
Ngazi hizo zimejengwa kwenye ukingo wa korongo la Mto Kalambo.
Sehemu ya juu ya Maporomoko ya Mto Kalambo.
 Muonekano wa mto Kalambo ambao unaotengeneza Maporomoko ya Mto Kalambo (Kalambo Falls)
Taswira ya maporomoko ya mto Kalambo kutokea angani (Picha hii ni kwa hisani ya Mtandao)

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)