Pages

RC KAGERA AONGOZA UZINDUZI WA MASHAMBA DARASA WILAYANI MISSENYI

 Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu  (wa tatu kulia), akikata utepe kuashiria uzinduzi  rasmi wa mashamba darasa ya kilimo bora cha mihogo na migomba iliyozalishwa kwa njia ya chupa (tissue culture), kwa ufadhili  wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia (OFAB) katika vijiji vya  Bunazi na Kashaba wilayani Missenyi mkoani humo leo. Shamba hilo litasimamiwa na Kikundi cha Ushirika cha Batekaka. Kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Luteni Kanali, Denis Mwila, Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Belington Kyokwete, Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, Shaban Hussein na Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Missenyi, Projestus Tegamaisho.
 Miche ya migomba ikiwa tayari kupandwa.
 Ofisa Ugani wa Kata ya Kasambya, Hakika Ibrahim, akizungumza kataika uzinduzi huo.
 Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, Shaban Hussein, akizungumza katika uzinduzi huo.
 Mtafiti kutoka OFAB, Dk. Beatrice  Lyimo akizungumza katika uzinduzi huo.
 Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti cha ARI-Maruku akielezea mbegu hiyo mpya ya migomba. 


  Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu (wa tatu kulia),  Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, Shaban Hussein na Mkuu wa  Mkuu wa Wilaya hiyo, Luteni Kanali, Denis Mwila (kulia), pamoja na Mwenyekiti wa Kikundi cha Ushirika cha Batekaka, Belington Kyokwete, wakiwa wameshika mmoja wa mche wa mgomba katika uzinduzi huo. 


 Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu , akipanda mche wa mgomba kwenye shamba darasa katika Kijiji cha Bunazi.
 Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, Shaban Hussein, akipanda mgomba kwenye shamba darasa hilo.




   Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu , akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Kashaba kabla ya kuzindua shamba darasa la zao la mhogo.
 Usikivu katika uzinduzi huo. Kutoka kulia ni Mtafiti kutoka OFAB, Dk. Beatrice  Lyimo, Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Adam Swai na Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, Shaban Hussein, akipanda mgomba kwenye shamba darasa hilo.
 Wananchi wa Kijiji cha Kashaba wakiwa kwenye uzinduzi huo.
 Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu , akimpongeza kijana, Shafii Idrisa wa Kijiji cha Kashaba ambaye ameamua kujishughulisha na kilimo kijijini hapo badala ya kukimbilia mjini na kuendesha bodaboda kama walivyofanya wenzake.



 Mtafiti wa mazao ya jamii ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti cha ARI-Maruku, Jasmeck Kilangi, akimueleza Mkuu wa Mkoa namna ya upandaji wa zao la mihogo.
  Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu, akipanda mbegu ya mhogo katika shamba darasa katika Kijiji cha Kashaba.
Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Missenyi, Projestus Tegamaisho, akitoa shukurani baada ya uzinduzi huo.




Na Dotto Mwaibale, Missenyi Kagera

WAKULIMA  wilayani Missenyi Mkoani Kagera wametakiwa kuyatumia matunda ya tafiti za kisayansi yanayoletwa na wataalamu kuboresha kilimo chao na kuongeza tija kwenye mazao mbalimbali ili kuweza kuchangia  malengo ya nchi kufikia uchumi wa kati.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu,  Salumu Mustafa Kijuu wakati akizungumza na wanakikundi cha Batekaka kwenye Kijiji cha Bunazi na kikundi cha Obumo wa Kijiji cha  Kashaba  kwenye uzinduzi wa zoezi la utoaji wa Mbegu bora za zao la migomba  iliyozalishwa kwa njia ya chupa na Mihogo yenye ukinzani na magonjwa ya batobato na michirizi ya kahawia zoezi lililofadhiliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo Tanzania (OFAB).

Alisema Kilimo pekee ndicho kinachoweza kuwakwamua wananchi kutokana na wimbi la umasikini lakini akasisitiza kuwa kilimo hicho lazima kizingatie mbinu zote za kilimo bora ambacho kitamuwezesha mkulima kulima eneo dogo na kupata mavuno makubwa na kuchana na kile cha zamani na mazoea cha kulima bila kutumia mbinu za kisayansi.

“Tafiti nyingi zinafanyika hapa nchini lakini zinaishia kwenye makabati na haziwafikii wakulima ambao ndio walengwa wa tafiti hizo lakini nawashukuru COSTECH kwa kushirikiana na watafiti wetu kwa kutuletea mbegu hizi bora mlizozitafiti na kujihakikishia kuwa zinauwezo wa kutatua changamoto za wakulima wetu na kuongeza tija”Alisema Mkuu huyo wa mkoa wa Kagera.

Mkuu huyo wa mkoa wa Kagera ameshukuru COSTECH kwa kuamua kusaidia kuwafikishia wakulima mbegu bora za MIhogo na Migomba na kuanzisha mashamba darasa kwenye wilaya zote za mkoa huo ambayo yatawezesha wakulima wengi zaidi kujifunza kwa vitendo na hatimae kuweza kuinga mbinu hizo za kisasa zilizotafitiwa na kwenda kuzitumia kwenye mashamba yao baada ya kuona matunda yatokanayo na mshamba hayo.

Meja Jenerali Mstaafu Kijuu pia alibainisha kuwa hivi sasa mkoa umejipanga kuhakikisha kila wilaya inakuwa na kiwanda kimoja kikubwa cha kuchakata zao moja na kila wilaya kuwa na zao moja la biashara hali ambayo itasaidia katika kuwahakikishia masoko ya uhakika wa mazao ya wakulima na hivyo kuongeza ari ya uzalishaji kwenye maeneo mengi.

Aliwataka maofisa ugani kuwasaidia wakulima katika kutumia mbinu bora za kilimo ili kuweza kuzalisha kwa tija na kuwataka kila mmoja kuwa na shamba lake ambalo wakulima wataweza kuona na kujifunza kwao badala ya kuwa wazungumzaji tuu bila wao kuonyesha mfano.

Awali akizungumza malengo ya mpango huo wa ugawaji mbegu na malengo yake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa COSTECH, Shabani Hussein alisema kuwa mpango huo ni moja ya utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo kwa mujibu wa sheria ya uanzishwaji wake ya kuhakikisha matokeo mazuri ya sayansi na teknolojia yanawanufaisha walengwa kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Alisema kuwa ili kuweza kufikia adhima ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa Tanzania ya viwanda ni lazima suala la kilimo lipewe msisitizo wa kutosha ili kuweza kuzalisha malighafi za kutosha kulisha vwanda vitakavyojengwa  lakini bila kilimo mpango huo unaweza kukwama.

Alisema pamoja na COSTECH kuwa mshauri mkuu wa serikali katika masuala yote yanayohusu sayansi,teknolojia na uvumbuzi lakini pia wanashirikiana na watafiti na vituo vya utafiti katika kusaidia kufikisha matunda hayo ya tafiti kwa wakulima ili kusaidia kuongeza tija na kuwakwamua wakulima katika wimbi la umasikini.

‘’Naamini mbegu hizi tulizozileta leo na mashamba darasa haya yatakuwa chachu kwa wakulima wengine kuona na kujifunza mbinu bora za kilimo kwenye maeneo yao na baadae mbinu hizo kusambaa kwa wakulima wengine kwenye maeneo ya jirani" alisistiza Hussein

Mwakilishi huyo wa Mkurugenzi mkuu wa COSTECH alisema mbegu hizo bora za Migomba safi isiyo na magonjwa pamoja na mbegu bora ya mihogo aina ya Kiroba yenye ukinzani na magonjwa ya batobato kali na michirizi ya kahawia itagaiwa kwenye vikundi kwenye wilaya zote za mkoa huo wa Kagera na kupewa mbinu bora za kilimo kutoka kwa wataalamu.

Mkuu wa WIlaya ya Missenyi, Luteni Kanali Denis Mwila amewapongeza COSTECH na OFAB kwa kutimiza ahadi yao ya kuwaletea wakulima mbegu hizo na kuwaahidi kuwa watasimamia mashamba darasa hayo vizuri hadi kuvuna ili wakulima waweze kuona umuhimu wa sayansi na mbinu bora za kilimo kwenye uzalishaji.

“ Tumepata bahati kubwa sana wana Missenyi uzinduzi huu kimkoa kufanyika kwenye wilaya yetu maana zipo wilaya nyingi lakini bahati imetuangukia sisi hivyo tuyatunze mashamba na mbegu hizi na tusiwaangushe COSTECH waliotuletea mbegu hizi bora” alisema Mwila.

Pia ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kutoa ruzuku za pembejeo mara mbili kwa mwaka kwenye mkoa wa Kagera kutokana na kuwa na misimu miwili ya kilimo badala ya kuwapatia pembejeo msimu mmoja pekee sawa na mikoa mingine yenye msimu mmoja.

Ameahidi kushirikiana na COSTECH na wataalamu katika kila aina ya teknolojia na mbinu bora inayowafaa wakulima wa wilaya yake ili kuwawezesha kuzalisha chakula kingi na mazao ya biashara ambayo wananchi watauza na kujipatia kipato.

Kwa upande wao wakulima kwenye vikundi hivyo wameahidi kuyatunza na kuyalinda mashamba hayo na mbegu hizo ili kuzizalisha kwa wingi na kuweza kuwasambazia wakulima wengine kwenye maeneo yao ili kujihakikishia usalama wa chakula kwa kulima zao bora la muhogo na kulima migombo bora iliyozalishwa kwa njia ya chupa baada a migomba yao kushambuliwa sana na ugonjwa hatari wa mnyauko.



Pia wakapaza sauti zao kwa serikali kuhakikisha wanawapelekea mbegu bora za mahindi na mazao mengine kwa wakati kupitia mpango wa serikali wa kutoa ruzuku ya pembejeo maana kilimo mbili za mbegu bora ya mahindi wananunua kwa wastani wa shilingi 15  bei ambayo ni kubwa kwa wakulima wengi.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)