NMB SASA KUSAIDIA KILIMO CHA MICHIKICHI MKOANI KIGOMA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

NMB SASA KUSAIDIA KILIMO CHA MICHIKICHI MKOANI KIGOMA

E79A5388
Mkuu wa Idara ya Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB- Filbert Mponzi (kulia) akitoa maelezo ya huduma za kifedha zinazotolewa na benki hiyo kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) alipotembelea Banda la Benki hiyo jana Jijini Dodoma kwenye monyesho ya Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT). Benki ya NMB imetoa kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kufadhili mkutano huo, ikiwa ni kwa mwaka wa sita mfululizo sasa. Wakishuhudia ni Meneja wa NMB Kanda ya Kati - Nsolo Mlozi pamoja na Meneja Mwandamizi wa Biashara za Kilimo wa NMB -Isaac Masusu.

mponzi%2Balat
Mkuu wa Idara ya Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Bw. Filbert Mponzi akiwasilisha mada kwa wajumbe wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) wakati wa mkutano mkuu wa 34 wa jumuiya hiyo unaoendelea jijini Dodoma.


BENKI ya NMB Plc imesema itashirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kusaidia kilimo cha zao la michikichi mkoani Kigoma.

Mpango huo ulielezwa jana na Mkuu wa Idara ya Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Bw. Filbert Mponzi wakati wa mazungumzo mafupi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea banda la benki hiyo kwenye  Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) unaoendelea jijini Dodoma.

Mponzi alisema kwa sasa NMB inawasaidia zaidi ya wakulima wadogo wadogo milioni moja nchi nzima, na kwamba benki itaendelea kutenga fedha za kutosha ili kusaidia wakulima wengi zaidi.

“Kwa sasa, NMB imetenga zaidi ya shilingi billioni 500 kwa ajili ya kusaidia wakulima hapa nchini lengo likiwa kusaidia jitihada za serikali ya awamu ya tano ya uchumi wa viwanda kupitia sekta ya kilimo.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu alisema kwa sasa Serikali inapeleka nguvu zake katika kukuza kilimo cha zao la mchikichi mkoani Kigoma, na hivyo akaitaka benki ya NMB kuisaidia Serikali katika kufanikisha azma hiyo kwa kuwasaidia wakulima wa michikichi mkoani humo.

“Tumekuwa tukiwashawishi wakulima mkoani Kigoma kujikita katika kilimo cha michikichi lakini kwa bahati mbaya wakulima wengi hawana mitaji ya kulima michikichi kwa wingi. Nitafurahi kama benki yenu kupitia mikakati yake itawawezesha wakulima wa michikichi,” alisema.

Aidha, Waziri Mkuu ameomba kukutana na uongozi wa benki ya NMB mapema wiki ijayo mkoani Kigoma ili kwa pamoja waweze kupanga mkakati kazi wa kuwasaidia wakulima mkoani humo kulima michikichi kwa ufanisi na wingi zaidi.

“Kwa sasa tunapambana ili kuhakikisha mazao yote ya biashara yanayostawi hapa nchini yanalimwa kwa kiwango kikubwa ili kuchochea kasi ya uchumi wa viwanda kupitia rasilimali za ndani. Ningependa tukutane Kigoma ilituone namna ya kuwezesha zao la michikichi kulimwa kwa wingi,” Majaliwa alieleza.

Akielezea mikakati mingine ya benki, Mponzi alisema NMB itaendelea kutanua wigo wa huduma zake ili kuhakikisha watanzania wengi zaidi wananufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo.

“Hivi karibuni tumezindua mfumo ambao unamwezesha mteja au mwananchi yeyote kufungua akaunti kupitia simu yake ya mkononi, ambapo namba yake ya simu ndiyo inakuwa namba yake ya akaunti. Ni matarajio yetu kwamba kwa kupitia mfumo huu shirikishi watanzania wengi zaidi, hususani wakulima wa vijijini,” aliongeza.

Pamoja na hayo, alieleza kuwa NMB itaendelea kushirikiana na mamlaka za Serikali za mitaa hapa nchini katika kuleta maendeleo chanya. NMB imekuwa mdhamini mkuu wa mikutano ya mwaka ya ALAT, na kwa mwaka huu, benki imetoa kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuwezesha mkutano huo muhimu uliyowakutanisha zaidi ya wajumbe 500 kutoka mikoa mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages