Warsha ya wachora vibonzo vijana.
Tarehe 7-9/6/2017, NMF itaendesha warsha ya siku tatu itakayofanyika katika ukumbi wa Nafasi Art Space, Dar es Salaam inakusudia kuwajengea uwezo wachora vibonzo vijana ambao tayari wanafanya kazi kwenye vyombo vya habari na wale ambao bado hawajapata nafasi hiyo.
Kutokana na mabadiliko ya teknolojia duniani, NMF inaamini kuwa kuna umuhimu wa wachora vibonzo wakapata mafunzo ya mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko hayo.
Warsha hiyo itafuatiwa na onesho la wazi la vibonzo vilivyochorwa katika warsha hiyo siku ya Jumamosi, tarehe 10/6/2017 kuanzia saa 10.00 alasiri mpaka 12 jioni katika katika ukumbi huo huo ambapo wakaazi mbalimbali wanakaribishwa. Hakutakuwa na kiingilio.
NMF inayoamini kuwa kipaji kinakuwa na maana pale tu kinapoibuliwa, endelezwa, nufaisha msanii na Taifa, inatoa shukrani kwa Ubalozi wa Uswis nchini Tanzania, Nafasi Art Space na RUKA Kipro kwa kuwezesha warsha hii kufanyika.
NMF inatoa wito kwa wadau mbalimbali kuiunga mkono hasa katika eneo la kuwajengea uwezo vijana wenye ndoto ya kuja kuwa wasanii hodari nchini.
Kifo cha Mzee Fransis Kanyasu Maige.
NMF inatoa pole kwa ndugu, familia na jamaa wa mchoraji mkongwe, Mzee Fransis Kanyasu Maige aliyefariki hivi karibu jijini Dar es Salaam.
NMF imesikitishwa na hali ya maisha aliyokuwa akiishi mkongwe huyo na kwamba hicho ni kiashiria tosha kuwa kuna changamoto nyingi kwenye mfumo wa sanaa nchini na kwamba umefika wakati sasa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikatoa ulinzi kwenye ubunifu kwa kutambua aina ya tatu ya mali yaani “Mali Isiyoshikika,” kwani wasanii wamekuwa wakitumika kuhamasisha maendeleo lakini kwa bahati mbaya wengi wao sanaa huwa haiwanufaishi!
Aidha, NMF inafahamu kuwa Serikali kwa kushirikiana na mashirikisho ya sanaa nchini ipo kwenye hatua ya awali ya ukusanyaji maoni kwa ajili ya “sera mpya ya sanaa” ambayo NMF inaamini itakuja na majibu yatakayotatua changamoto zinazowakabili wasanii na mfumo mzima wa sanaa.
NMF inaunga mkono hatua hiyo na inaiomba Serikali kuongeza nguvu hasa eneo la rasilimali fedha ili kuwezesha ukusanyaji wa maoni ikiwezekana nchi nzima.
Nathan Mpangala Foundation (NMF), No.5286, yenye makao yake jijini Dar es Salaam, ni asasi isiyokuwa ya kiserikali iliyosajiliwa mwishoni mwa mwaka jana kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ikiwa na malengo kadhaa ikiwemo mafunzo ya sanaa.
Imetolewa na;
Nathan Mpangala,
NMF, Mwenyekiti
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)