Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakiwa ukumbi wa mikutano Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) jijini Dar es Salaam leo kupata taarifa ya mfumuko huo wa bei kwa mwezi Machi.
Ofisa Habari wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Veronica Kazimoto (kulia), akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwapatia taarifa hiyo.
Na Dotto Mwaibale
MFUMUKO wa Bei wa Taifa kwa mwezi Machi, 2017 umeongeza hadi kufikia asilimia 6.4 kutoka asilimia 5.5 mwezi Februari 2017.
Hayo yamebainishwa katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa hali hiyo inamaanisha kuwa, kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Machi 2017 imeongezeka ikilinganishwa na kasi ya upandaji ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi wa Februari 2017.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 108.44 mwezi Machi 2017 kutoka 101.93 mwezi Machi 2016.
Mfumuko wa Bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Machi 2017 umeongezeka hadi asilimia 11.0 kutoka asilimia 8.7 ilivyokuwa mwezi Februari 2017.
Taarifa hiyo imeonesha kuwa kuongezeka kwa mfumuko wa Bei wa mwezi Machi 2017 kumechangiwa na kuongezeka kwa bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Machi 2017 zikilinganishwa na bei za mwezi Machi 2016.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)