Mrembo wa Tanzania mwenye tamaa ya kuwa na himaya ya samani za kimataifa kupitia kampuni yake, kama alivyowahi kuelezwa na jarida la Forbes hivi karibuni, Jacqueline Ntuyabaliwe ametwaa tuzo mbili za ubunifu kupitia kampuni ya Molocaho by Amorette.
Ushindi wake huo unamuingiza katika kundi la watu wenye ubunifu mkubwa wa bidhaa za majumbani na katika maofisi, muda mfupi tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo.
Molocaho by Amorette kampuni ya kubuni na kutengeneza samani ilizinduliwa Septemba 2016. Miezi michache tu tangu kuundwa kwake inaonesha kukimbia na kufanikisha tuzo tatu za kimataifa.
Katika tuzo zenye ushindani mkali na heshima kubwa kwenye ubunifu za kimataifa zijulikanzo kama A-Prime Design (A'Design) zilizofanyika mjini Roma mwishoni mwa wiki Jacqueline amepata tuzo katika kategori mbalimbali na kuwa wa pili kategori nyingine.
Bidhaa zilizompatia tuzo ni samani na pia za mwanga.
Ngorongoro Settee ilimpatia medali ya shaba kwa upande wa samani na katika bidhaa za mwanga Sayari Lamp pia ilimpatia tuzo ya shaba. Nafasi ya pili ilipatikana katika kiti cha Flamingo.
Taarifa zilizofikia thebeauty zinasema kategori ya Furniture, Decorative Items and Homeware Design Category ya mwaka 2016 na kiti cha Ngorongoro na kategori ya Lighting Products and Lighting Projects Design Category ya mwaka 2016 ilikuwa na Sayari lamp.
Na Kiti cha Flamingo kilimpatia nafasi ya pili katika kategori ya Furniture, Decorative Items and Homeware Design Category ya mwaka 2016.
A-Prime Design Shindano aliloshiriki Jacqueline Mengi akiwa na kampuni yake ya Molocaho by Amorette la A’Design hushirikisha wabunifu, wagunduzi na makampuni yanayotengeneza bidhaa mbalimbali za ubunifu wa ndani.
Shindano la A' Design limeanzishwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba wabunifu wanakuja na bidhaa bora kabisa zenye ushindani mkali katika soko la kimataifa.
Kwa kawaida tuzo zake hutolewa katika kusanyiko kubwa la wabunifu linalofanyika Roma, Italia kwa kuratibiwa na OMC Design Studios SRL .
Jacqueline, Miss Tanzania (2000) hivi karibuni alishiriki tuzo za rais za CTI na ana mafunzo ya Interior Design kutoka Rhodec International.
Kampuni ya Molocaho by Amorette, kampuni ya Tanzania inajishughulisha na utengenezaji wa samani bora kwa namna mteja anavyohitaji, nyuzi, taa, urembaji, samani za nje na kwenye bustani.
Molocaho inatengeneza samani zenye mahadhi ya kiafrika ikichanganya utamaduni wa Tanzania katika mazingira ya kisasa na kumalizia na ubunifu wa kimataifa.
Molocaho, moja ya makampuni ya Afrika Mashariki ya samani yanayokua kwa kasi, imejipatia nafasi kubwa ya heshima kwa kuhakikisha kwamba inatumia mali ghafi na mbao njema pekee za Tanzania kutengeneza samani zenye kwenda kimataifa.
Katika mahojiano na jarida maarufu la Forbes alishawahi kusema kwamba anawania soko la kimataifa kutokana na ukweli kuwa bidhaa anazotengeneza zimejipambanua kwa wateja.
Jacqueline Ntuyabaliwe, pamoja na kuwa na ratiba yenye changamoto sana (Yeye ni balozi wa WildAid na yumo ndani ya bodi kadhaa; mama wa watoto pacha wavulana; mke kwa mfanyabiashara mwenye mafanikio makubwa na akiendesha taasisi ya hisani ya elimu), huhakikisha anakagua kila samani inayozalishwa kiwandani kwake kabla ya kuuzwa au kusafirishwa.
Mume wake, Reginald Mengi, ni tajiri mwenye mafanikio makubwa nchini Tanzania ambaye ameujenga utajiri wake kwa kufanya karibu kila kitu kuanzia uzalishaji wa kinywaji cha Coca-Cola hadi uchimbaji wa madini na kumiliki vituo vya televisheni na magazeti.
Kwa tuzo hizo Amorette, inajidhihirisha kuwa chata yenye mafanikio makubwa nchini Tanzania na huku ikipanda kwa kasi kimataifa.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)