SHULE ZATAKA PEDI KWA AJILI YA WANAFUNZI WA KIKE SHINYANGA,DC AOMBA MSAMAHA WA KODI - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

SHULE ZATAKA PEDI KWA AJILI YA WANAFUNZI WA KIKE SHINYANGA,DC AOMBA MSAMAHA WA KODI

Pamoja na jitihada zinazofanyika kuhakikisha kuwa na vyumba maalum kwa ajili ya watoto wa kike kujisitiri wanapokuwa katika hedhi lakini bado changamoto kubwa ni upatikanaji wa vitambaa wakati wa hedhi "pedi"kwa watoto wa kike hasa kwa watoto wasio na uwezo.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya waandishi wilayani Kishapu walipotembelea shule mbalimbali kuangalia hali ya upatikanaji wa vyumba kwa ajili ya kujisitiri watoto wa kike wanapokuwa katika hedhi na upatikanaji wa vitambaa ‘pad’ ili kuimarisha usafi wa mtoto wa kike anapokuwa shuleni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walimu wa wakuu wa shule za msingi na walimu walezi wa wanafunzi wa kike wilayani Kishapu walisema wamejitahidi kuwa na vyumba maalumu kwa ajili ya watoto wa kike kujistiri wanapokuwa kwenye hedhi lakini changamoto ni upatikanaji wa pad kwani watoto wengi hawana uwezo wa kununua pedi.


Walisema shule nyingi hazina uwezo wa kifedha kuweza kununua pedi na kuzigawa bure kwa wanafunzi hivyo kuwaomba wadau mbalimbali wa watoto kujitokeza kusaidia watoto wa kike kwani wazazi wengi wamekuwa wakidai hawana uwezo wa kununua vitambaa hivyo.


Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nyenze iliyopo katika kata ya Mwadui Lohumbo,Yohana Saraton alisema changamoto waliyonayo sasa ni upatikanaji wa vitambaa ‘pad’ kwa ajili ya watoto wakiwa katika hedhi.

“Sisi tuna chumba maalum kwa ajili ya watoto wa kike kujisitiri lakini pad hazipo tunaomba mashirika na wadau mbalimbali wajitokeze kufadhili ugawaji wa pad katika shule hiyo”,alisema Saraton.

Naye Mwalimu Mlezi wa wanafunzi wa kike katika shule hiyo Leanita Kalinjuna alisema ukosefu wa pad unawafanya baadhi ya wanafunzi wa kike kutohudhuria masomo wanapokuwa katika siku zao ‘hedhi’.

“Kutokana na kukosekana kwa vitambaa hivyo wanafunzi huwa wanatoa taarifa kama wapo hedhi na huwa tunawapa ruhusa,tunaomba kupatiwa vifaa hivyo maana sisi tuna chumba maalum na tuna vifaa vya kuhifadhia pad zilizotumika”,aliongeza mwalimu Kalinjuna.

Kwa upande wake Ofisa Elimu wa mkoa wa Shinyanga Mohamed Kahundi alisema ni kweli kuna tatizo la upatikanaji wa vitambaa hivyo kwani bajeti inayotolewa na serikali haijitoshelezi kuhudumia wanafunzi wote wa kike katika shule kwa kuwanunulia pedi.

“Asilimia 10 ya fedha za huduma ya kwanza katika shule haitoshi kuhudumia wanafunzi wote kwani shule zetu zina wanafunzi wengi lakini tunaendelea kuangalia namna ya watoto hawa ili waweze kuhudhuria masomo yao ikiwemo kuwahamasisha walimu walezi wa wanafunzi hao kuwa karibu na watoto wa kike”,aliongeza Kahundi.

“Kuweka chumba maalum katika shule ni sera mpya tuliyoianzisha kupitia mradi wa “School Wash” ambao unatekelezwa kila halmashauri ya wilaya zote japokuwa siyo katika shule zote,pale tunajenga vyoo vipya tumeamua tuwe tunatenga chumba kwa ajili ya watoto wa kike ili kupunguza utoto shuleni”,alieleza Kahundi.

Mkuu wa wilaya ya Kishapu Nyabaganga Talaba alishauri vifaa kwa ajili ya watoto wa kike visamehewe kodi vinapoingizwa nchini kwa sababu vina gharama kubwa ukilinganisha kuwa watoto hao hawana ajira.

“Ukisema kwamba shule zitumie pesa za vifaa zinunue haviwezi,kila mtu aangalie kuwa ni jukumu lake kuwahudumia watoto wa kike ,jamii kama jamii ituone sisi wanawake kuwa tuna mahitaji mengine ambayo yanahitaji yaonwe kwa jicho la ziada”,aliongeza Talaba.

Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Vyoo vya wanafunzi (kushoto) na cha walimu (kulia) katika shule ya msingi Nyenze iliyopo katika kata ya Mwadui Lohumbo wilayani Kishapu
Choo cha wanafunzi katika shule ya msingi Nyenze ambacho kina chumba kimoja maalum kwa ajili ya wanafunzi wa kike kinachotumiwa na wanafunzi hao wanapokuwa katika hedhi
Chumba maalumu kwa ajili ya watoto wa kike/wanafunzi wa kike wanaosoma katika shule ya msingi Nyenze.Pamoja na kuwepo kwa chumba hicho lakini hakuna kifaa chochote kwa ajili ya watoto wa kike wanapokuwa katika hedhi
Chumba maalumu kwa ajili ya wanafunzi wa kike kikiwa hakina pedi yoyote.Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages