Chama cha watu wenye ualbino Tanzania (TAS) kimelaani vikali vitendo vya ufukuaji wa makaburi ya watu wenye ualbino vinavyoendelea kujitokeza nchini hali inayowafanya waishi kwa hofu kubwa katika nchi yao.
Inaelezwa kuwa tangu kuibuka kwa mauaji ya watu wenye ualbino mwaka 2007 takribani makaburi 22 nchini Tanzania yamefukuliwa na watu wasiojulikana.
Chama hicho kimeiomba serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais John Pombe Magufuli kuweka mkazo katika mapambano dhidi ya ukatili wa watu wenye ulemavu wa ngozi kama ilivyoonesha nguvu za kutosha katika vita ya dawa za kulevya na pombe aina ya viroba.
Akizungumza juzi kwenye kikao cha viongozi wa chama watu wenye ualbino kutoka mikoa ya kanda ya Ziwa ambayo ni Mara,Mwanza na Shinyanga na wanachama wengine Afisa mahusiano na habari TAS taifa Josephat Torner vitendo vya kufua makaburi ya watu wenye ualbino yanatishia amani yao
Torner alisema wanaiomba serikali kuelekeza nguvu katika masuala ya mauaji na ufukuaji wa makaburi ili kuwafanya watu wenye ualbino waishi kwa amani ndani ya nchi yao.
“Katika suala la mauaji ya watu wenye ualbino ambao wamekuwa wakiishi kwa hofu tunaomba serikali hata kuwataja kwa majina wanunuzi hao kama ilivyotokea kwenye masuala ya vita ya dawa zakulevya na uuzaji bombe aina ya viroba”,alisema Torner.
Aidha alisema wanalaani kitendo cha kufukuliwa kwa kaburi la Nelson Msogole (50) aliyekuwa akiishi mji wa Songwe baada ya kufariki tarehe 28/3/2011 na kaburi lake kuonekana kufukuliwa tarehe 20/3/2017na watu wasiojulikana.
“Matukio haya yanaendeshwa kwa usiri hivyo tunahoji kwanini imeshindikana ikiwa kwenye dawa za kulevya wameweza kutaja na kumepiga hatua?”,alihoji Torner.
Alisema Tangu kuanze kuibuka mauaji ya watu wenye ualbino mwaka 2007 makaburi 22 nchini yamekwisha fukuliwa katika mikoa ya Mbeya ,Tabora,Mwanza,Mara ,Kagera,Rukwa, na Shinyanga.
Aliiomba serikali ya awamu ya tano iweke mikakati ya uelewa kwenye jamii kwani huenda hawana uelewa na watuhumiwa wakibainika waadhibiwe kwa mujibu wa sheria.
“Hiki ni kipimo cha serikali ya awamu ya tano kwa sauti ya wanyonge kwani kuna baadhi ya watu wanaishi kwenye nchi yao kwa hofu na unyonge na kuondolewa utu wao hivyo tuna imani serikali itaweka nguvu kubwa kuliko kipindi cha nyuma”,aliongeza Torner.
Naye Mwenyekiti wa chama hicho kutoka mkoani Mwanza Alfredy Kapole alisema mkoa wa Mwanza unaongoza kwa mauaji ya vifo vya albino zaidi ya 17 vimetokea tangu mwaka 2007 hivyo aliiomba serikali kuweka ulinzi mkubwa kwa watu hao kwani wanakiuka katiba ya nchi kwani kila mtu anastahili kuishi.
Mwenyekiti wa chama hicho kutoka mkoani Mara Joseph Sinda alisema kitendo cha kufukua kinawafanya waishi kwa hofu kubwa na kuitaka serikali ijaribu kuchunguza chanzo chake ni nini na kuthibiti kama kwenye madawa ya kulevya na pombe aina ya viroba walivyofanya ili waweze kuishi kwa amani.
Mwanaharakati kutoka mkoani wa Shinyanga Eunice Zabroni aliiomba serikali wawaimarishie ulinzi na elimu itolewe kwani wanaishi kwa hofu kwa kukosekana ulinzi imara kuanzia ngazi ya vitongoji,vijiji kata na wilaya hadi mkoa.
Habari na Kareny Masasy- Malunde1 blog
Katikati ni Afisa mahusiano na habari wa chama cha watu wenye ualbino nchini Tanzania (TAS )Josephat Torner akizungumza wakati wa kikao cha viongozi na wanachama wa chama hicho ambapo walilaani vitendo vya ufukuaji wa makaburi ya watu wenye ualbino.Kulia ni Mwenyekiti TAS mkoa wa Mara Joseph Sinda,kushoto ni mwenyekiti TAS mkoa wa MwanzaAlfred Kapole -Picha zote na Suzy Butondo-Malunde1 blog
Afisa mahusiano na habari wa chama cha watu wenye ualbino nchini Tanzania (TAS )Josephat Torner ambapo alisema chama hicho kinaiomba serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais John Magufuli kuongeza kasi katika mapambano dhidi ya ukatili wa watu wenye ualbino
Baadhi ya wanachama wa chama cha watu wenye ualbino nchini Tanzania wakiwa katika kikao hicho.
Picha na Suzy Butondo-Malunde1 blog
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)