Kamishna mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya aliyeteuliwa jana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli, Rogers Sianga ameahidi kushughulikia kwa karibu kesi za vinara wa ‘unga.’
Sianga aliyekuwa Moshi mkoani Kilimanjaro, alisema akifika Dar es Salaam atakutana na watendaji wengine waangalie cha kufanya katika namna ya kushughulika na vigogo na wafanyabiashara maarufu waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
“Ndiyo kwanza nimeteuliwa bado nipo Moshi nikifika Dar es Salaam, nitazungumza na wenzangu naamini tutashirikiana na tutashughulikia kwa msingi wa sheria,” amesema.
Pia, alitoa onyo kwa watu wanaolima mirungi au bangi nchini na kuwataka watafute kazi nyingine.
Dawa hizo nyingine za kulevya ni ghali na zinaletwa kutoka nje ya nchi, lakini mirungi na bangi tunajua inalimwa nchini hao wakulima waache walime mazao ya vyakula, maana dawa hizo zinaleta madhara makubwa kwa maendeleo ya taifa,” amesema.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais jana, Gerson Msigwa ilisema Sianga atasaidiwa na Mihayo Msikela atakayekuwa Kamishna wa Operesheni na Fredrick Kibuta atakayekuwa Kamishna wa Intelijensia.
Uteuzi huo umekuja siku chache baada ya Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema) kumtaka Rais Magufuli kuteua kamishna mkuu wa tume hiyo, ambayo imekaa bila kiongozi tangu Sheria ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya ilipotungwa mwaka 2015.
“Tusifanye siasa kwenye vita hii ya madawa ya kulevya, tusimwongopee Rais kwa kutaka kuhakikisha vyeo vyetu tumwambie ukweli.Ili kumsaidia Rais anapaswa kumteua kamishina wa hii tume maana tangu tulipopitisha sheria hiki chombo hakina kamishna, tutakapohakikisha hicho chombo kinapata kamishna kwa kumsaidia Rais tutakamata wale wanaoingiza dawa za kulevya, wale mapapa na si hao wanaokamatwa sasa hivi,” alisema Bulaya.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)