Ndugu
Mwakilishi kutoka Benki ya NMB,
Waandishi
wa habari,
Kwa niaba ya Chama cha
Wamiliki/Waendeshaji wa Mitandao ya Kijamii nchini 'Tanzania Bloggers Network'
(TBN) napenda kuwashukuru kwa kujitokeza katika mkutano huu muhimu. TBN inajua
kuwa mnamajukumu mengi ya kuujuza umma masuala anuai, lakini mmechagua kuja
kwetu ili kutusikiliza tulichowaitia na baadae tunaamini mtaujuza umma juu ya
tukio letu.
Ndugu
Wanahabari,
Katika mkusanyiko huu
wanatasnia watapewa semina juu ya uendeshaji mitandao ya jamii kwa manufaa,
upashaji habari kwa kutumia mitandao yao kwa kuziangatia maadili na namna ya
kunufaika na mitandao hiyo kwa waendeshaji (kujipatia kipato) hasa ukizingatia
kuwa wapo baadhi yetu tunaifanya kama ajira nyingine. Kimsingi lazima tukubali
kuwa mitandao hii imekuwa tegemeo kubwa la kusambaza habari mbalimbali tena kwa
muda mfupi tangu kutokea kwa tukio fulani, hivyo kuna kila sababu ya kuendelea
kuwapiga msasa wanaoiendesha ili kupunguza matumizi mabaya ya mitandao hii.
TBN inaamini njia pekee
ya kupambana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ni kuendelea kutoa elimu
kwa waendeshaji na watumiaji ili mwisho wa siku wasikubali kutumika vibaya au
kuitumia vibaya mitandao hii katika kutoa taarifa. Kwa dunia ya sasa hakuna
atakayepinga kuwa mitandao hii imekuwa ikielimisha umma, ikikosoa jamii na
kiburudisha juu ya masuala anuai ya kijamii.
TBN inapenda kutoa
shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Nne na Tano chini ya Mh. Rais John Pombe
Magufuli kwa ushirikiano alioanza kuuonesha hasa kwa kutambua mchango wa
mitandao hii ya kijamii na hata kuitumia katika utoaji wa taarifa zao. Kimsingi
hii ni hatua nzuri na ya kuigwa hasa katika ulimwengu huu ambapo dunia imekuwa
kama kijiji kutokana na hatua ya maendeleo ya habari na mawasiliano.
Ndugu
Wanahabari,
Kwa kulitambua hili
mnaweza kuona hata taasisi nyeti kama Ikulu nayo ina Blogu maalumu kwa ajili ya
kutoa taarifa kwa umma, Idara ya Habari Maelezo nayo ina Blogu kwa ajili ya
kutoa taarifa kwa umma juu ya masuala mbalimbali yanayopaswa kutolewa kitaarifa
kwa jamii. Jambo la kujivunia zaidi kwa maendeleo ya mitandao hii hata Waziri
wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Nape M. Nnauye amekuwa
mstari wa mbele kuona umuhimu wa mitandao ya kijamii hasa blogu na hata
kuzitumia katika kupasha habari umma. Hata katika mkutano wetu wa kesho kutwa
ndiye tunayemtarajia kuwa mgeni rasmi atakayetufungulia mkutano huo.
Ndugu
Wanahabari,
Kwa namna ya pekee TBN
inapenda kutoa shukrani za pekee kwa Benki ya NMB kwa kukubali kuwa wadhamini
wa kuu wa mkushanyiko huo wa 'bloggers' kutoka maeneo mbalimbali ya mikoa yetu.
Kitendo cha kujitolea kufanikisha jambo hili kinaonesha namna gani NMB
inavyowajali wananchi katika masuala mbalimbali ikiwemo hili la upashanaji
habari kwa jamii.
Imetolewa
na; Mwenyekiti wa Muda wa TBN
Joachim
E. Mushi
0756469470
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)