SUALA LA UKEKETAJI MKOANI MARA BADO NI PASUA KICHWA. - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

SUALA LA UKEKETAJI MKOANI MARA BADO NI PASUA KICHWA.

Baadhi ya wasichana wakitoka kukeketwa wilayani Tarime mkoani Mara, kumbuka mwezi Disemba, kila baada ya miaka miwili, ni msimu wa ukeketaji na tohara kwa baadhi ya Koo za Wakurya.
#BMGHabari

Pamoja na juhudi za Serikali, Wanaharakati na Watetezi wa haki za binadamu (Wanawake na Wasichana) katika kuhakikisha kwamba suala la ukeketaji linatokomezwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mikoa ya Mara na Arusha, bado suala hilo ni pasua kichwa kwani linafanyika, iwe kwa uwazi ama usiri.

Mtandao wa Binagi Media Group umeshuhudia baadhi ya wakazi wa wilaya ya Tarime wakisherehekea msimu huu wa ukeketaji (Mwezi Disemba kwa baadhi ya koo, ikiwemo Watimbaru) ambapo wasichana wadogo wanafanyiwa ukeketaji.

Shamra shamra zinafanyika hadharani licha ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga, kuonya kwamba yeyote atakayebainika kujihusisha na ukeketaji atachukuliwa hatua za kisheria.

Baadhi huamini kwamba msichana akikeketwa huleta heshima kwake na kwa familia na huwa tayari kwa ajili ya kuolewa na hivyo kuwapatia wazazi mahari (ng'ombe). Hatua hii husababisha baadhi ya mabinti kukosa fursa ya kuhitimu masomo yako na kujikuta wakiolewa, Aidha kwa kupenda ama kulazimishwa na wazazi/walezi wao. Suala la unyanyapaa miongoni mwa wasichana waliokeketwa na ambayo hawajakeketwa ni jambo ambalo pia huongeza msukumo wa wasichana kutaka kukeketwa. Mbaya zaidi, unyanyapaa huo huenda hadi kwa baadhi ya wanaume kukataa kuwaoa wale ambao hawajakeketwa na hivyo kusababisha ugumu wa kutokomeza suala hilo.

Tayari Ngariba mmoja aitwaye Angelina ppCharles (50) amehukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezaji kwa kosa la kumfanyia ukeketaji mmoja wa wasichana wilayani humo huku wengine wawili wakidaiwa kukabiliwa na kesi ya aina hiyo. Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Mhe.Martha Mpaze.

Wakati hayo yakiendelea, zipo kauli mbalimbali wilayani Tarime kwamba hivi sasa wasichana hawakeketwi kama zamani bali wakifika eneo la tukio hupakwa unga kwenye uso na maumbile yao na kufanyiwa matambiko ya kimila na shughuli huishia hapo na kinachofuata ni shamra shamra za kucheza ngoma ya ritungu na kurejea nyumbani.

Hata hivyo utafiti uliofanywa mwishoni mwa mwaka jana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na idadi ya watu duniani, UNFPA, kwenye mikoa 13 nchini ikiwemo Mara, umebaini kwamba katika maeneo mengi nchini, wanajamii wanazo mbinu mpya za kuhakikisha wanatimiza malengo yao ya kukumbatia mila potofu ikiwemo ukeketaji. Utafiti huo ulibaini kuwa, suala la kuwapaka unga usoni wasichana wilayani Tarime ni kuuficha tu ukweli kwamba wasichana hao hawakeketwi wakati ukweli ni kwamba hukeketwa.

Itoshe tu kusema kwamba, elimu zaidi inahitajika ili kuwanusuru wasichana wanaotoka kwenye makabila yanayojihusisha na ukeketaji kwani madhara yake ni makubwa ikiwemo kupoteza damu nyingi, kupata madhara kabla na baada ya kujifungua, kupoteza uwezo wa kufurahia tendo la ndoa, uwezekano wa kupata maambukizi ya magonjwa ikiwemo Virus vya Ukimwi na wakati mwingine kupoteza maisha.
Inaelezwa kwamba msichana anayekeketwa hulipia kiasi cha shilingi elfu 35 hadi 40 ambapo wazee wa kimila hugawana pesa hiyo na mangariba hivyo inawezekana suala hili linakuwa na ugumu kutokomezwa maana ni sehemu ya ujira kwa wazee na mangariba hao.
Inadhaniwa kwamba zaidi ya wasichana 3,000 kwa Koo moja ya kabila la Wakurya hukeketwa kwa kila msimu. Kabila la Wakurya lina Koo 13.
Wakazi wa Wilaya ya Tarime wanasema, msukumo wa ukeketaji umepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Wanasema suala la elimu juu ya madhara ya ukeketaji pamoja na mwingiliano wa makabila mbalimbali ya ndani na nje ya mkoa wa Mara, umesaidia japo kwa kiasi kidogo kupunguza ari ya ukeketaji.
Kataa Ukeketaji, haina umuhimu kufurahia mila na tamaduni zenye athari katika jamii. Vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuwakama na kuwafungulia mashtaka.
Wakati haya yanaendelea, zaidi ya wasichana 250 kutoka maeneo mbalimbali mkoani Mara na Arusha, wamehifadhiwa katika kituo cha kuwahifadhi wasichana waliokimbia ukeketaji cha Masanga kilichopo wilayani Tarime.

BMG inaamini kwamba, Imani humalizwa kwa Imani. Suala la Ukeketaji ni Imani hivyo itolewe elimu yenye uhusiano wa kiimani ikiwemo maandiko matakatifu (dini) hatua ambayo itasaidia kuwanusuru wasichana wengi na suala hilo la ukeketaji.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages