Pages

Saa 144 za Maxence Melo ndani ya mahabusu

Maxence Melo akifikishwa mahakamani Ijumaa, Desemba 16, 2016. (Picha kwa hisani ya Michuzi Blog).

Na Daniel Mbega
HATIMAYE leo saa 5:15 asubuhi ya Jumatatu, Desemba 19, 2016 Maxence Melo ametoka kwa dhamana. Mungu ametenda.

Lakini ni baada ya Mkurugenzi huyo Mtendaji wa kampuni ya Jamii Media Limited inayomiliki mtandao maarufu wa JamiiForums, kusota mahabusu kwa takriban saa 144 – yaani saa 72 katika mahabusu ya polisi na saa 72 nyingine kwenye Gereza la Mahabusu la Keko.

Leo amefanikiwa kutimiza masharti ya dhamana katika kesi namba 457 ya mwaka 2016 ambayo iko mbele ya Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, ambayo iliitwa tu kwa ajili ya kushughulikia dhamana.

Kesi hiyo imepangwa kuitwa Alhamisi, Desemba 29, 2016.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Msomi Mohammed Salum, uliieleza mahakama kwamba kesi hiyo ilikuwa imeitwa kwa ajili ya dhamana baada ya upande wa utete kushindwa kutimiza masharti ya dhamana wakati kesi hiyo iliposomwa kwa mara ya kwanza Ijumaa, Desemba 16, 2016.

Jopo la mawakili wa utetezi linaongozwa na Peter Kibatala, akiwa pamoja na Jeremiah Mtobesya, Benedict Ishabakaki, Jebra Kambole, Hassan Kyangiro na James Malenga, ambapo ilielezwa kwamba wadhamini wamepatikana na kukidhi vigezo vya dhamana ya maneno ya Shs. 5 milioni kila mmoja.

Hakimu Mwambapa alikubali kutoa dhamana na kumtaka mshtakiwa asitoke nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama.

Melo alikamatwa Jumanne, Desemba 13, 2016 saa 5 asubuhi – tena alikwenda mwenyewe baada ya kupigiwa simu na Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Camillius Wambura.

Walichoelezwa hata waliokuwa wamekwenda naye ni kwamba, waondoke hapo polisi watakutana mahakamani kesho yake, yaani Desemba 14, 2016. Hakupelekwa mahakamani wala hakuchukuliwa maelezo.

Kwa siku mbili mfululizo kati ya Desemba 14 na 15 nilishinda katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati, jijini Dar es Salaam, nikiwa na wadau mbalimbali tukitafuta namna ya kumwekea dhamana. Haikuwezekana.
Hii ndiyo gharama ya kusimamia unachokiamini pamoja na maadili yanayokuongoza. 

Na wakati jitihada za kumpata mdhamini katika kesi mojawapo, upande wa Jamhuri ukawa umeondoka na wakati huo huo Maxence akapelekwa mahabusu ya Keko yapata saa 5 asubuhi. Hawakusubiri hadi saa 8 kama ilivyo kawaida ili kuwapandisha mahabusu wote kwenye karandinga, jambo ambalo likazua maswali mengi yasiyo na majibu.

Lakini hatimaye Max ameiona nuru, ambayo ameikosa kwa saa 144, japo kwa muda kwa sababu kesi hizi zinaendelea.

Kesi ya kwanza, ambayo ni namba 456, iko mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa mahakama hiyo, Thomas Simba, ambapo upande wa Jamhuri ulieleza kwamba, katika siku na tarehe tofauti kati ya Aprili 1, 2016 na Desemba 13, 2016 katika eneo la Mikocheni ndani ya Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Melo akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media Co. Ltd ambayo inaendesha mtandao wa JamiiForums, wakati akijua kwamba Jeshi la Polisi Tanzania linafanya upelelezi wa jinai kuhusiana na mawasiliano ya kimtandao yaliyochapishwa kwenye mtandao wake, kwa nia ya kuvuruga uchunguzi, alikaidi kwa makusudi amri ya kutoa taarifa ambazo alikuwa nazo, kinyume na kifungu cha 22(2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao (Cyber Crimes Law) namba 14 ya mwaka 2015.

Katika namba 457,  ambayo alikosa mdhamini, ilielezwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwambapa kwamba, katika siku na tarehe tofauti kati ya Mei 10, 2016 na Desemba 13, 2016 katika eneo la Mikocheni ndani ya Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Melo akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media Co. Ltd ambayo inaendesha mtandao wa JamiiForums, wakati akijua kwamba Jeshi la Polisi Tanzania linafanya upelelezi wa jinai kuhusiana na mawasiliano ya kimtandao yaliyochapishwa kwenye mtandao wake, kwa nia ya kuvuruga uchunguzi, alikaidi kwa makusudi amri ya kutoa taarifa ambazo alikuwa nazo, kinyume na kifungu cha 22(2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao (Cyber Crimes Law) namba 14 ya mwaka 2015.

Aidha, katika kesi namba 458, ambayo iko mbele ya Hakimu Nongwa, Melo anakabiliwa na shtaka la kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa nchini Tanzania (domain) kinyume na kifungu cha 79(c) cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Namba 3 ya mwaka 2010 ikisomwa pamoja na Kanuni ya 10 na 17 (4) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Namba 428 za mwaka 2011.

Upande wa Jamhuri ulieleza katika kesi hiyo kwamba, katika siku na tarehe tofauti kati ya Desemba 9, 2011 na Desemba 13, 2016 katika eneo la Mikocheni ndani ya Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Melo akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media Co. Ltd iliyosajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa Kampuni (Sura ya 212 kama ilivyorejewa mwaka 2002) yenye hati ya usajili Namba 66333 amekuwa akiendesha na kutumia tovuti inayojulikana kama jamiiforums.com ambayo haijasajiliwa kwenye code za Tanzania (country code Top Level Domain - ccTLD), inayofahamika kama do-tz.

Yaliyompata Max ni mwanzo tu wa yale ambayo yanaweza kutupata sote, hususan waandishi wa habari wa mtandaoni na watumiaji wengine wa mitandao.

Hii inatokana na kuwepo kwa Sheria ya Makosa ya Kimtandao (Cyber Crimes Law) ya mwaka 2015, ambayo ilipitishwa Aprili Mosi, 2015.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)